Rais Mzungu wa kwanza kuongoza dola huru Afrika

05Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Rais Mzungu wa kwanza kuongoza dola huru Afrika

GUY Scott, raia wa Scotland aliyeiongoza Zambia kuanzia Oktoba 2014 hadi Januari 2015, akiingia Ikulu baada ya kifo cha Michael Sata, rais wa taifa hilo, ameacha historia kuwa mtu mweupe wa kwanza kuongoza dola huru Afrika Kusini ya Jangwa Sahara.

Scott akiwa Rais wa Zambia katika kipindi cha mpito mwaka 2014. PICHA: MTANDAO.

Scott aliyekuwa Makamu wa Rais alichaguliwa kuwa Kaimu Rais wa Zambia aliyeliongoza taifa hilo kwa miezi mitatu ya mpito kwenye kipindi ambacho uchaguzi mkuu ulitarajiwa kufanyika ndani ya siku 90.

Alikuwa kaimu rais baada ya kifo cha rais Michael Sata kilichotokea London, Uingereza Oktoba 28, 2014 na kumfanya kuwa kiongozi wa kwanza Mzungu kuliongoza taifa huru la Kiafrika.

Michael Sata aliyekuwa na miaka 77 aliondoka Zambia kuelekea jijini London kwa matibabu ya ugonjwa ambao haukutajwa na baadaye kufariki dunia.

Sata alimteua kuwa Makamu Rais mwaka 2011 baada ya chama chake cha Patriotic Front (PF)kushinda uchaguzi mkuu wa nchi hiyo na kuanzia wakati huo alikuwa akishiriki mikutano na majukwaa mbalimbali ya viongozi wa Afrika akimuwakilisha Rais Sata.

Guy Scott akiwa na miaka 70 kwa wakati huo, kwa asili alikuwa mkulima mtoto wa masetla kutoka Scotland lakini pia ni mchumi, aliyetinga Ikulu ya Zambia na kupata heshima zote za dola licha ya kwamba kulikuwa na kipengele cha katiba kinachoagiza kuwa rais wa taifa hilo ni lazima awe raia wa kuzaliwa Zambia ambaye ni sharti awe mtoto wa kizazi cha tatu cha wazazi wote wawili ambao ni lazima wawe wazawa wa nchi hiyo na si vinginevyo.

Hivyo, ili mgombea awe rais wa taifa hilo ni lazima ithibitike kuwa kizazi chake kuanzia mababu wanaowazaa babu na bibi wazaa babu na bibi zake ambao ni wazazi wa baba na mama yake ni lazima wawe wamezaliwa Zambia ili ufanikiwe ni lazima uwe kizazi cha tatu.

Kutokana na kikwazo hicho Guy Scott hakuweza kuwa Rais wa Zambia kwa sababu wazazi wake walitokea Scottland. Kulingana na katiba ya Zambia, kiongozi wa nchi hiyo ni lazima awe Mzambia kamili kwa maana ya kwamba wazazi wake wote wawili wanapaswa kuwa wamezaliwa nchini humo.

Mwanazuoni wa sayansi za siasa nchini Zambia Lee Habasonda akinukuliwa na vyombo vya habari baada ya Scott kuchaguliwa alisema wapinzani wake wangetumia kipengele cha uraia kwenye katiba kumweka pembeni kiongozi huyu mwenye asili ya Scotland.

“Scott anaweza kuiongoza Zambia kipindi cha mpito na kwa hakika ana sifa zote, kwani katiba inasema pale rais aliyeko madarakani atakapofariki dunia makamu wake anaongoza nchi katika kipindi cha siku 90 ambacho ndani yake uchaguzi mkuu utafanyika. Kwa Scott hilo halina kipingamizi kwani kuanzia mwaka 2011 alikuwa makamu wa rais.” Habasonda alisema.

KIKWAZO KIKATIBA

Baada ya kifo hicho cha Sata Wazambia walianza kutafuta kile kinachomkwamisha Makamu Rais kuwa kiongozi wa taifa hilo na kubaini kuwa kipengele cha wazazi kuwa wazawa kiliwekwa kwenye katiba na rais Frederick Chiluba, wakati alipoingia madarakani wakati wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1990.

Lengo lake lilidaiwa kuwa ni kumdhibiti mpinzani wake Kenneth Kaunda, mpigania uhuru na baba wa taifa hilo aliyeleta ukombozi miaka 1960 anayesadikiwa kuwa baba yake mzazi ni raia wa Malawi.

Lengo la Chiluba lilikuwa kumdhibiti Kaunda na kuhakikisha kuwa anaondoka kwenye nyanja za kisiasa na uongozi wa taifa hilo na hivyo hadi sasa kiongozi huyo mwanzilishi wa chama ukombozi cha UNP na mpigania uhuru pekee anayeishi barani Afrika hajaomba tena kupewa ridhaa ya kuliongoza taifa hilo.

HISTORIA YA SCOTT

Kiongozi huyo alizaliwa mwaka 1944 nchini Zambia, wakati huo ikiitwa Northern Rhodesia baada ya baba yake kuondoka mjini Glasgow na kuja Afrika kufanyakazi kama daktari kwenye mashirika ya reli.

Scott alisoma uchumi katika Chuo Kikuu cha Cambridge na baada ya miaka mingi ya kilimo na shughuli za uzalishaji alijitosa katika siasa mwaka 1990 na kuwa mwanachama wa chama cha MMD ambacho kilishinda uchaguzi kwenye uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini humo.

Kwa upande wa uongozi Scott si mgeni, aliwahi kuwa Waziri wa Kilimo aliyeinusuru Zambia na matatizo ya ukame mkali uliolikumba taifa hilo mwaka 1992 hadi 93 na kusababisha hali ngumu kwa taifa hilo kiuchumi na kwa upande wa chakula.

Alihama chama cha MMD na kujiunga na Patriotic Front (PF) mwaka 2001 kilichokuwa kinaongozwa na Michael Sata aliyemteua kuwa Makamu wa Rais Septembar 2011 baada ya PF kushinda kwa kishindo wakati huo Sata akijulikana kwa jina la utani kama King Cobra.

Hata hivyo, Scott asingeweza kuwa au kuwania urais kwa sababu katiba ya Zambia haimruhusu na kwa kuwa wazazi wake si wazawa.

Scott anaingia katika historia ya Afrika kutokana na ukweli kuwa ni kiongozi wa kitaifa wa kwanza mwenye asili ya Kizungu kuongoza dola baada ya kuanguka kwa utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini, lakini hakuweza kupanda ngazi zaidi kwa kuwa wazazi wake ni masetla wa kikoloni walioiongoza Zambia wakati wa utawala wa Waingereza.

Itakumbukwa kuwa wakati wa kampeni za PF Sata alianzisha kampeni za kupinga masuala ya kuwapo wageni nchini humo hasa Wachina, wakati wa kampeni zake alisimama kidede na kutaka wazawa wapewe nafasi.

Wakati akisimamia kampeni hizo China imekuwa mshirika mkubwa wa shughuli za kiuchumi za Zambia ikijenga miundombinu, kuchimba madini na miradi mikubwa inayohitaji mitaji na uwekezaji mkubwa. Baadhi ya Wazambia wanaadaiwa kuwa waliuona uwekezaji huo kuwa ni aina ya ukoloni wa kiutandawazi.

MITANDAO

Habari Kubwa