Rais Putin: Nchi za Magharibi zinalaghai mataifa ya Afrika!

23Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Rais Putin: Nchi za Magharibi zinalaghai mataifa ya Afrika!

RAIS wa Urusi, Vladmir Putin, amesema nchi yake inaweza kuisaidia Afrika bila masharti ambayo huambatanishwa kwenye misaada ya mataifa ya Magharibi.

Rais Vladimir Putin wa Urusi. PICHA: MTANDAO

“Tunaona jinsi mataifa ya Magharibi yanavyotoa shinikizo na vitisho dhidi ya serikali huru za Kiafrika, wanatumia njia hizo ili kurejesha nguvu ya ushawishi na utawala kwenye makoloni yao ya zamani na kulinyonya Bara la Afrika,” anasema Rais Putin katika mahojiano na Shirika la habari la Urusi TASS, kabla ya mkutano na viongozi wa Afrika.

Urusi inatarajia kuwa mwenyeji wa viongozi 47 wa Afrika katika mkutano wa siku mbili Oktoba 23 hadi 24 unaofanyika mjini Sochi.
Rais Putin amesema uhusiano na Afrika umeimarika, akiainisha makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya silaha, ambapo Urusi imefanikiwa kushawishi mataifa zaidi ya 30 kusambaza silaha zake.

Rwanda ni moja ya nchi ambazo zimekuwa na uhusiano mzuri na Urusi.

Baraza la Mawaziri la Rwanda hivi karibuni liliridhia makubaliano na Urusi katika masuala ya matumizi ya nishati ya nyuklia maalumu kwa matumizi ya amani, limeripoti Gazeti la The East Africa.

Teknolojia hii itatumika katika uzalishaji wa nishati na utunzaji wa mazingira, ripoti inasema.

USHAWISHI WA NCHI ZA MAGHARIBI KWA AFRIKA

Marekani imekuwa ikipoteza ushawishi barani Afrika, lakini mwanadiplomasia wa juu wa nchi hiyo kwa Bara la Afrika, anataka kubadili hali hiyo.

Rais Donald Trump alishawahi kuripotiwa kuyataja mataifa ya Kiafrika kuwa ni ‘nchi chafu’ na kuongelea Afrika kama sehemu ambayo marafiki zake wanakwenda kujaribu kutajirika.

“Kwa muda mrefu wakati wawekezaji walipokuwa wakibisha milango na Waafrika wakifungua, mtu pekee aliyekuwa hapo ni Mchina,” Tibor Nagy, mjumbe wa masuala ya Afrika wa Marekani, aliiambia BBC.

Biashara ya China na Bara la Afrika imeifunika Amerika katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, na mwaka 2018 ilikuwa kubwa mara tatu zaidi.

Marekani imekuwa chanzo kikubwa cha uwekezaji wa moja kwa moja barani Afrika, lakini mchango wake umekuwa ukipungua.
Mwaka 2018, China ilitangaza uwekezaji wa thamani ya dola za kimarekani bilioni 60 kwa ajili ya miradi ya miundombinu.

Ben Abdallah anasema kuwa biashara kati ya Marekani na mataifa ya Afrika imeshuka kwa sababu ya ongezeko la uhitaji si tu China, lakini nchi nyingine kama vile Urusi na Uturuki.

“Nafikiri ni kwa sababu ushindani kutoka kwa nchi nyingine umeongezeka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita,” anasema.
Ukuaji wa uchumi wa China umeonyesha dalili za kushuka hivi karibuni, hali ambayo itaathiri biashara na uwekezaji katika Afrika siku za usoni.

Lakini kutokana na ushindani kutoka duniani kote wa kufanya biashara na nchi za Kiafrika, Marekani inapambana kurejesha uhusiano na bara hilo kwa kujihusisha na nchi za uchumi unaochipukia.

BBC

Habari Kubwa