Rais Samia anapokaripia wabunge…

21Apr 2021
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Rais Samia anapokaripia wabunge…

KAULI ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwataka wabunge kujadili maslahi ya nchi na siyo mipasho, inaelezwa kuwa ni maagizo ya kuliamsha bunge kujitafakari na kujihoji iwapo linafanya kazi yake ipasavyo.

Mwishoni mwa wiki, Rais alisema anaona kama mijadala bungeni inatoka nje ya kile kinachokusudiwa na kinachochojiri  ni mashambulizi ya mtu dhidi ya mwingine, viongozi na  kulumbana zaidi badala ya kuleta hoja na fikra za kuishauri na kuikosoa serikali.

Akizungumzia onyo hilo kwa wabunge, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Bob Wangwe, anasema wawakilishi hao wa wananchi wanatakiwa wazungumzie  maslahi ya nchi siyo hoja ambazo hazina manufaa kwa taifa.

Anasema kauli ya Rais inakuja ikitanguliwa na maoni ya wana harakati, asasi za kiraia na hata aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Profesa Mussa Assad, kuwa limeonekana kuwa lina udhaifu.

Anasema udhaifu huo unaanzia kwenye katiba kwa vile haijawapa wananchi mamlaka ya kuwawajibisha wabunge wanapoona hawatimizi wajibu ipasavyo au kufanya wapendalo.

Wangwe anasema udhaifu huo kikatiba unachangia wabunge kutojali na kufanya wapendalo kwa vile wanafahamu wapigakura hawawezi kuwafukuza na wana uhakika wa kudumu kwa miaka mitano.

“Kwa kuona upungufu huo, ni wakati wa serikali kuona umuhimu wa kurejea tena mchakato wa kuandikwa katiba mpya ili kuongeza uwajibikaji bungeni na kuwapa wapigakura mamlaka ya kuwaondoa wale wasiotimiza wajibu …” anashauri.

Akizungumzia madai kuwa wakati wa bunge la vyama vingi, wapinzani walilichelewesha na kulikwamisha bunge kufanya uamuzi na mijadala inayohusu maendeleo ya nchi bila sababu kwa vile muda wote walipinga na kusoa, alisema :

“Waliokuwa na hisia hizo sasa wameona kuwa upinzani unahitajika uwepo bungeni.”

Anasema ni wakati wa serikali na wapigakura kuhakikisha kuwa kunakuwa na uwakilishi wenye maoni na mtizamo tofauti ili kuendeleza na kudumisha demokrasia na mijadala inayolenga kuikosoa, kuisimamia na serikali na kutetea maslahi ya nchi.

Anapoulizwa anadhani nini Rais Samia atakasema bungeni kesho wakati akilihutubia bunge, alisema anatarajiwa kutoa mwekeo wa taifa katika kipindi cha uongozi wake, ataeleza miradi inayokusudiwa kutekelezwa kuomba uungwaji mkono na wabunge.

KUKUMBUSHWA WAJIBU

Akizungumzia maelekezo ya Rais Samia kwa bunge, mbunge wa zamani wa Moshi Vijijini, Thomas Ngawaiya, anasema, amelenga kuwakumbusha wabunge kuzingatia wajibu wao wawapo bungeni.

Anasema, bungeni ni sehemu ambayo kuna mijadala ya hoja zilizo muhimu na zinazoletwa mbele yao, kupaza sauti za wapigakura, kusimamia na kuishauri serikali na siyo malumbano yasiyo ya tija kwa taifa.

"Bungeni si sehemu ya mipasho, matusi, kejeli, lugha ya kuudhi kama ambavyo baadhi ya wabunge wamekuwa wakifanya na ni jambo jema kuwa Rais ameliona hilo na kulikemea," anasema Ngawaiya.

Ngawaiya anasema, alikuwa mmojawapo wa watu waliokuwa wakikerwa na kile kilichokuwa kikifanyika bungeni na kwamba amefurahishwa na hatua ya Rais Samia kutuliza hali ya hewa mapema.

Mwanasiasa huyo anasema, kanuni za bunge haziruhusu mbunge kutumia lugha ya kuudhi, na kwamba alishangaa kusikia baadhi ya wabunge wakiambiana hawajasoma au wewe ni wa darasa la saba.

Anasema, kwa kuwa Rais anajiandaa kuhutubia bunge kesho , anaamini hotuba yake itakuwa na maelekezo mengi na kwamba, ataweka wazi misimamo mingi ya serikali yake na kile anachotaka kifanyike.

"Tutarajie makubwa katika hotuba ya Rais wetu ambayo yataligusa bunge na mengi na serikali yake kwa ujumla inayopanga kuyafanya kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii na watu wake," anasema.

Anaongeza kuwa anaweza kuwaweka sawa wabunge ambao wamekuwa wakienda nje ya mstari wanapochangia hoja bungeni na kusababisha malumbano yasiyo na tija wapigakura wao na taifa kwa ujumla.

"Hadi rais kufikia kuzungumzia kilichokuwa kikiendelea bungeni, ni wazi hakufurahishwa nacho na ingawa si mtu wa kufoka, hatua hiyo inaonyesha hakupendezwa na uendeshwaji wa muhimili huo ambao pamoja na kutunga sheria, kupitisha bajeti na kuishauri serikali unawajibu pia wa kujiendesha kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu," anasema.

Mbunge huyo wa zamani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (CEGODETA), anasema, hotuba ya rais pia inaweza kujikita kwenye suala la utawala bora kwa kwa sababu, hatua yake ya kukemea yale yaliyokuwa yakiendelea bungeni, ni wazi anapenda utawala bora, hivyo ninaamini suala hilo litagusiwa pia.

KUBADILI GIA

Katika mjadala huo, mchambuzi wa masuala ya kisiasa Abdul-Karimu Atiki, anasema ni wakati wa bunge kujiongeza na kujua upepo umebadilika na kujielekeza kwenye mwelekeo mpya, ili kuwa na mijadala yenye tija.

Anawakumbusha wabunge kuwa katika awamu zilizopita kuna mambo yaliyofanyika ambayo wananchi wanayakubali na mengine wanayapinga, hivyo hakuna sababu ya kuyaibua na kuyajadili zaidi bungeni kwa sababu tayari yanajulikana yasiendelezwe kwa vile ni kupoteza muda.

“Wabunge waende na wakati wajue kuwa zama zimebadilika siyo kuendelea kubaki nyuma na kushikilia misimamo iliyopita,” anasema mchambuzi huyo.

Anasema kukumbushwa na Rais kunaonyesha kuwa pengine kuna walakini kwenye kutimiza wajibu wake kikatiba, hivyo muhimili huo ujikite kushauri, kuelekeza serikali masuala yenye tija yanayoleta maendeleo.

Akizungumzia ukosoaji uliotolewa na baadhi ya wadau kuwa bunge halina meno, anasema udhaifu unaozungumziwa ni hatua ya muhimili huo kushindwa kuiwajibisha serikali au taasisi zinazofanya makosa hasa yanayoibuliwa na ofisi ya CAG.

Anasema udhaifu unaonekana kwenye kushindwa kukemea na kuchukua hatua unapotajwa upungufu na badala yake kuendelea kunyamaza au kutokujali ndiko kunakofanya chombo hicho kionekana kuwa ni dhaifu.

Anakumbusha kuwa kusema bunge ni dhaifu au halina meno wakati mwingine si sahihi kwa vile haliwezi ‘kuiuma serikali’ bali wanaofanya hivyo ni wananchi wanaofanya maamuzi kutokana na kile wanachoona hakiwaridhishi.

“Wenye meno ni wapigakura siyo wabunge. Hata hivyo bunge ni la kichama linaundwa na vyama na kile chenye uwakilishi mkubwa ndicho kinachounda serikali.”

Atiki anaeleza kuwa wabunge hao wenye serikali hawawezi kuiondoa serikali yao madarakani ndiyo maana wakati mwingine linaweza kuitwa dhaifu lakini wanajua namna bora ya kuishauri na kuikosoa serikali yao.

Mchambuzi huyo anashauri wabunge kuibua hoja zenye tija, mitizamo na zenye kutetea maslahi ya nchi na ikibidi wakubali kunahitajika tija kwenye kutimiza wajibu huo.

Habari Kubwa