Rais wa zamani wa Misri azikwa baada kufariki dunia mahakamani

19Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Rais wa zamani wa Misri azikwa baada kufariki dunia mahakamani

RAIS wa zamani wa Misri, Mohammed Morsi, alizikwa jana, baada ya kuanguka mahakamani juzi na kuaga dunia.

Rais wa zamani wa Misri, Mohamed Morsi aliyezikwa jana baada ya kufariki dunia juzi. PICHA: MTANDAO

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yametaka kufanyika uchunguzi huru, kufahamu sababu halisi ya kifo chake.

Wakili wa rais huyo wa zamani anasema Morsi alizikwa jana asubuhi katika makaburi ya Medinat Nasr Mashariki mwa mji mkuu, familia yake ikiwepo.

Televisheni ya taifa hilo imesema kifo chake kilisababishwa na mshtuko wa moyo.

Morsi, Rais wa kwanza wa kiraia wa Misri, ambaye ni wa kwanza pia kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, alianguka katika kizimba chake mahakamani baada ya kujieleza, na aliwahishwa hospitalini ambako ilitangazwa kuwa alikuwa tayari amekata roho.

Tangu alipoangushwa katika mapinduzi ya kijeshi Julai 2013, aliyekuwa waziri wake wa ulinzi Abdel Fattah al-Sisi amechukua hatamu za uongozi wa nchi hiyo, akipambana vikali na maelfu ya wanachama na wafuasi wa kundi la Udugu wa Kiislamu (Muslim brotherhood), huku miongoni mwao wakikabiliwa na hukumu ya kifo.

SERIKALI YANYOOSHEWA KIDOLE

Watetezi wa haki za binadamu wanakosoa mazingira ya wafungwa magerezani nchini Misri.

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Misri wanasema yumkini mazingira mabaya gerezani yamesababisha kifo cha Morsi, hali ambayo wanasema ni ukiukaji wa haki za binadamu.

Mmoja wao, Amr Magdi wa Shirika la Human Rights Watch anasema:

“Tunaamini kwamba mazingira mabovu na ya kutengwa aliyowekwa Morsi yanakidhi vigezo vya utesaji kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa (UN) na kanuni za msingi za hali ya wafungwa, ambazo serikali ya Misri ilizipuuza kabisa.”

Mwanaharakati huyo anaongeza kuwa anadhani serikali ya al-Sissi imeonyesha dharau ya kupindukia dhidi ya haki za msingi za binadamu.

Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu, anasema pia kwa muda mrefu Morsi amekuwa akilalamikia ukosefu wa matibabu yanayofaa kwa ugonjwa wa kisukari aliokuwa nao na kunyimwa ruhusa ya kumuona daktari wake.

Awali, mtoto wa Morsi, Abdullah Mohammed Morsi, aliiambia DW kwamba mara ya mwisho familia iliruhusiwa kumtembelea baba yake Septemba mwaka jana.

MORSI SHAHIDI

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambaye ni mshirika wa kundi la Udugu wa Kiislamu amemshambulia Rais al-Sisi kwa kifo cha Morsi aliyemuita shahidi, na kuzikosoa nchi za Magharibi kufumbia macho rekodi yake mbaya kuhusu haki za binadamu.

Naye Katibu Mkuu wa Tawi la Kijeshi la Udugu wa Kiislamu, Murad Adeileh, akizungumza kutoka nchini Jordan anasema kifo cha Morsi kimetokana na uhalifu, na akataka ufanyike uchunguzi wa kimataifa.

Iran na kundi la Kipalestina la Hamas pia wametoa salamu zao za rambirambi.

Morsi amekuwa jela kwa miaka mitano iliyopita, na mwaka 2015 alihukumiwa kifo, kwa hatia za ujasusi na kushirikiana na magaidi. DW

Habari Kubwa