RC: Nimekuja na mpango mkakati mpya kulinda mipaka ya nchi Songwe

23Jul 2021
Nebart Msokwa
Dar es Salaam
Nipashe
RC: Nimekuja na mpango mkakati mpya kulinda mipaka ya nchi Songwe

AKIWA anahesabu miezi tangu alipoteuliwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba, ameweka bayana vipaumbele vyake katika utendaji kazi ndani ya mkoa huo.

Hapo kipaumbele chake, kinaangazia kulinda usalama wa wananchi, mali na mipaka ya nchi. Mgumba anaiambia Nipashe kwamba mkoa huo ni mchanga kuliko mingine yote nchini na unapakana na nchi mbili za Zambia na Malawi, hivyo ulinzi kwenye mipaka yake muhimu kwa usalama wa nchi.

Hapo katika nafasi yao pekee, unatajwa mpaka wa Tunduma, kati ya Tanzania na Zambia ambao ni nyenzo nyeti katika uchumi wa nchi kihistoria.

Anataja kipaumbele chake cha pili ni kuimarisha sekta ya kilimo kwa lengo la kuinua kipato cha wananchi wa mkoa huo na kuhakikisha kunakuwapo usalama wa chakula mkoani humo na hata kwa taifa zima.

Anasema Songwe, ni mkoa wa tatu kitaifa kwa uzalishaji mkubwa wa zao kahawa, nyuma ya Kilimanjaro na Kagera.
Katika hilo, anataja dhamira yake inasimamia kuhakikisha kilimo cha zao hilo, pamoja na mazao mengine ya kibiashara kwa ajili ya uchumi wa wananchi.

“Pia Mkoa huu ni wa tatu kitaifa kwa uzalishaji wa mazao ya chakula, hususani mahindi. Kwa hiyo, hiki ni kikapu cha taifa, tunategemewa kwa ajili ya kulisha taifa hili, lazima tusimamie kilimo ili tujilishe sisi wenyewe na tulishe na watu wengine,” anasema Mgumba.

Anaendelea: “Mkoa wetu pia unapozungumzia Songwe unazungumzia uvuvi maana tuna Ziwa Rukwa, ambalo lipo ndani ya mipaka yetu. Tutahakikisha tunasimamia uboreshaji wa sekta ya uvuvi, ili iwaingizie kipato wananchi wetu.”

Vilevile, Songwe imo katika mikoa ambayo wananchi wake ni wafugaji na anasisitiza kwamba, atasimamia wananchi wake wanaachana na ufugaji wa asili na kuhamia ufugaji wa kisasa, hata ukaongeza tija kimkoa.

Mgumba ambaye kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo, anasema mkoa anaouongoza una maeneo mengi yanayofaa kwa ufugaji nyuki, hasa katika misitu iliyoko wilayani Songwe, hivyo analenga kusimamia na kuimarisha sekta, ili iwasaidie wananchi kuongeza kipato.

Ahadi yake ni kuhakikisha kwamba, atasimamia vyema sekta hizo na kuzisaidia kuimarisha lishe, kwa wananchi, ili kukabiliana na tatizo la udumavu ambalo linakabili sehemu ya jamii.

SEKTA MADINI

Mgumba anasema kipaumbele chake ni kusimamia sekta ya madini, ili kuhakikisha inawanufaisha wananchi wa mkoa huo na taifa, kwa maelezo kuwa sekta hiyo ni muhimu na miongoni mwa shughuli zinazoziingizia taifa fedha nyingi.

Hapo anawapa moyo wachimbaji wadogo wa madini, kwa kuwahakikisha anawalinda na kuwagawia maeneo ya uchimbaji, ili wayamiliki na kufanya kazi zao kwa uhuru.

“Tunataka wachimbe, wauze, wajiongezee kipato na walipe kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa, madini haya ni kwa ajili ya taifa zima.

“Lakini nawakazania zaidi wananchi wa Songwe kwa sababu mkoa huu ni kitindamimba kimuundo na tunatakiwa tuujenge,” anasema Mgumba.

Mkuu wa Mkoa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, anawataka wachimbaji wadogo wachangamkie fursa ili wanufaike na sekta hiyo, kwa maelezo neema imeshaanza kufunguka.

UBORESHAJI BIASHARA

Mkuu wa Mkoa Mgumba, anasema katika mkoa huo mchanga, biashara ni miongoni mwa shughuli zao kuu za kiuchumi, zinazofanyika na zinahitaji usimamizi wa karibu.

Ahadi yake ni kuhakikisha kwamba, anasimamia kwa umakini shughuli na hasa mpakani katika mji wa Tunduma, ambao wakazi wake wengi shughuli yao kuu ni biashara, pia kutokana na kukosa nyingine kutokana na uhalisia wa vikwazo mazingira.

“Wakazi wa Tunduma hawalimi, hawafugi, hawachimbi madini na wala hawavui samaki, shughuli zao ni biashara, tutahakikisha tunawawekea mazingira mazuri ya biashara ili wapate faida, wakuze mitaji yao na walipe kodi ya serikali,” anasema Mgumba.

Mkuu wa Mkoa anapaza sauti kwa wafanyabiashara wanaotaka kwenda mkoa humo, kwamba amejipanga anawasaidie ufanisi upatikane, katika mazingira ya utulivu.

FURSA UWEKEZAJI

Mgumba ambaye kitaaluma ni mtaalamu wa usimamizi wa biashara, anasema mkoa wa Songwe una fursa mbalimbali za uwekezaji, ikiwamo kwenye sekta za kilimo, uvuvi, madini na biashara na kwamba kila moja ina eneo maalumu linalofaa shughuli hizo.

Anafafanua, kuwapo fursa za uwekezaji kwenye viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali, ukiwamo mpunga unaolimwa katika Bonde la Kamsamba wilayani Momba, mahindi pamoja na mazao mengine.

Mkuu wa Mkoa anasisitiza: “Vipaumbele vyote nilivyovitaja ni fursa kwa wawekezaji kutoka katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kuja mkoani kwetu kuwekeza na sisi kama serikali tutaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji kuja kuwekeza.”

Anasema kuna vipaumbele vilivyoainishwakwa kushirikiana na sekta binafsi katika kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo, hivyo atahakikisha wawekezaji wanaandaliwa maeneo ya kuwekeza.

SHIDA YAKE

Mgumba anasema, mkoa wake wenye wilaya nne na halmashauri tano, unakabiliwa na tatizo la kukatika kwa nishati ya umeme, hali inayowakatisha tamaa baadhi ya wawekezaji.

Anasema tatizo hilo linasababishwa na mkoa huo kuendelea kutumia njia moja pamoja na Mkoa mama wa Mbeya hali inayosababisha umeme ukikatika Mbeya lazima ukatike na maeneo yote ya mkoa wake.

Anafafanua kwamba, hivi sasa tayari wanaendelea na ujenzi wa njia mpya ya umeme kutoka jijini Mbeya ambayo itatenganishwa na ile inayotumika Mbeya ili kusiwapo na uhusiano wa moja kwa moja kati ya njia hizo.

Mgumba anasema ujenzi wa njia hiyo baada ya kukamilisha, watagawa tena njia hizo ili kila wilaya ya mkoa huo iwe na njia yake jambo ambalo litasaufanya nishati hiyo ikikatika kwenye wilaya moja nyingine iendelee kupata.

“Lakini, tutaendelea kusambaza umeme kwenye vijiji vyote vya mkoa wetu kupitia mradi wa REA, ili sasa tuvutie wawekezaji wa viwanda, tunataka watu waweke viwanda vya kuchaka mazao mpaka vijijini.

“Tunataka tuache kusafirisha mpunga kutoka Kamsamba na badala yake watu wajenge viwanda vya kuchakata mpunga mpaka Kamsamba ili tuache kusafirisha mazao ghafi,” anasema Mgumba.

Anaahidi atahakikisha anaendeleza mema yote yaliyoanzishwa na watangulizi wake ambao ni Luteni Mstaafu Chiku Galawa na Brigedia Jenerali Nicodemas Mwangela.

Habari Kubwa