RC Pwani: Mwaka huu tumepania mazito kwenye uzalishaji korosho

20Nov 2020
Julieth Mkireri
Kibiti
Nipashe
RC Pwani: Mwaka huu tumepania mazito kwenye uzalishaji korosho
  • Azindua na kufuatilia sentensi zake

KOROSHO ni moja  ya mazao ya biashara yanayotegemewa kukuza uchumi katika Mkoa wa Pwani ikifuatiwa na ufuta na inaelezwa, wastani wa asilimia 80 hadi 90 ya wakazi Mkoa wa Pwani, ama wanalima au kujishughulisha nalo.

Mhandisi Evarist Ndikilo, akiangalia namna korosho zinavyokatwa kutenganisha nzima na zisizofaa katika ghala la Mkuranga. PICHA: JULIETH MKIRERI.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, mbali ya kujikita kuhamasisha ujenzi wa viwanda na kuufanya mkoa huo kuongoza ajenda hiyo, sasa ameamua kuvalia njuga korosho.

Ndikilo amekuwa na vikao na wadau wa korosho na amevitumia kusisitiza usafi mashambani, pia uhifadhi mzuri ili soko la korosho kimkoa, uwe na thamani kubwa ndani na nje ya nchi.

Anasema sio kazi rahisi kushuhudia korosho za mikoa mingine katika minada yake zikiuzwa kwa bei ya juu, huku Pwani ikikosa soko, jambo analoahidi hatokubaliana nalo hata kidogo.

"Ninachokitaka ni wakulima kufuata taratibu na kanuni za uhifadhi wa korosho, ili zinapofika kwenye maghala wanunuzi wavutiwe nazo nisingependa kusikia tumekosa soko kutokana na ubora wa korosho zetu, hili kwa Pwani tunalipinga na nitapambana lisitokee," anaahidi.

Mkuu wa Mkoa, kila mara amekuwa akiagiza katika vikao vyake na wadau wa korosho na kukutana na maofisa ugani wa halmashauri za mkoa, anawatembelea wakulima na kuwaongezea elimu ya kilimo cha zao hilo, hata namna ya kuzihifadhi zinapotoka shamba.

Anasema ili kupata Korosho bora maandalizi yake yanatakiwa kufanyika tangu zikiwa shambani na mkulima kuwa makini kwa kila hatua kwa kufanya hivyo, zitapatikana zenye daraja la juu zitakazouzika kwa urahisi.

“Ninasisitiza utunzaji mzuri wa korosho kuwa na sehemu safi na salama za kuhifadhia kabla ya kuziweka kwenye magunia hii itasaidia kuwa na Korosho bora," anatamka.

STAKABADHI GHALANI

Akielezea kuhusiana na mfumo wa stakabadhi ghalani ulivyoleta faida katika misimu miwili iliyopita, Mhandisi

Ndikilo anasema: "Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ulianza katika mkoa rasmi mwaka 2017/2018, ambayo tani 20,650.03 zilikusanywa na kuingiza zaidi ya Sh. bilioni 59"

Ndikilo anasema, katika msimu wa mwaka 2018/2019 uzalishaji uliongezeka kufikia tani 23,266.7 zilizokusanywa na kuingiza shilingi billion 63.

Anasema, mafanikio hayo yalitokana na njia bora katika maandalizi na hifadhi ya korosho sokoni na katika Msimu uliopita, anataja uzalishaji uliyumba kutokana na hali mbaya hewa, upepo na mvua nyingi zilizonyesha, hata kuufanya mkoa kuishia kukusaya jumla ya tani 16,317.170  na kuingiza Sh. bilioni 9.9.

MSIMU ULIOZINDILIWA

Katika uzinduzi wa mnada msimu uliopo, korosho daraja la kwanza liliuzwa kwa Sh. 2153 huku daraja la pili likisubiri mnada mwingine kutokana na wakulima kutoridhia bei ya Sh.1400.

Akizungumza na wakulima viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) Mhandisi Ndikilo, anaeleza kuwapo mambo yanayotakiwa kutekelezwa na wahusika, pasipo visingizio, mahsusi akitaja usimamizi wa ukusanyaji mzuri wa korosho.

Mhandisi Ndikilo anawataka viongozi wa ngazi zote kulisimamia hilo na kuhakikisha korosho zinaelekezwa kwenye mfumo wa Stakabadhi Ghalani, pasipo kutoa nafasi kwa njia zisizo rasmi.

Katika mnada huo uliozinduliwa Novemba 11, huko Kibiti, anawaonya viongozi wa AMCOS na hasa makatibu wake, kuwa makini na kujiepusha na ubadhilifu wa korosho za wakulima.

"Upotevu wa korosho za wakulima kwa kisingizio cha ‘unyaufu’ haukubaliki na wahusika wote watawajibishwa. Kinachotakiwa ni wakulima wanaoleta korosho jina na kilo zao ziwekwe wazi," anaelekeza Ndikilo.

Mkuu huyo wa mkoa, pia anatumia nafasi hiyo kuwaasa wakulima kuendeleza ubora wa korosho na kujiepusha na kuchanganya vitu vingine.

Anatoa agizo pia kwa wakuu wa wilaya kuhimiza Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA), kuhakikisha hali ya barabara zinazotoka shambani hadi kwenye maghala ziko vizuri, kurahisisha usafirishaji wa korosho.

Ndikilo pia, anahimiza Chama Kikuu cha Ushirika (CORECU) na AMCOS, kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati baada ya korosho zao kuuzwa.

Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Shangwe Twamala, anasema hadi kufikia Novemba 10  (iliyopita) vyama vya msingi vimekusanya jumla ya kilo 3,709,167 kutoka Mkuranga ni kilo 909,375; Kibiti 1,519,700; Rufiji 1,174,592; Mafia kilo 3,200; Kisarawe 52,300; na Kibaha 50,000.

RAS MSAIDIZI

Anasema hadi kufikia Novemba 11 maghala makuu yanayofanya kazi ni Ikwiriri Wilaya ya Rufiji, Kibiti na Mwanambaya Mkuranga.

Twamala anabainisha kuwa mnada huo ulihusisha uuzaji wa kilo 2,073,293 sawa na asilimia 55.9 ya korosho zote zilizokusanywa na AMCOS na kilo 1,740,054, zipo kwenye maghala makuu ya Ikwiriri (kilo 770,677, Kibiti 482,132 na Mkuranga kilo 487,245.

Aidha, kilo 333,239 zinaelezwa zipo katika ghala la kampuni ya Biotan Mkuranga, akifafanua kuhusiana na madaraja ya korosho, akieleza kwamba, kati ya kilo 2,073,293 zilizolengwa kuuzwa, kuna 512,786 za daraja, ikiwa ni asilimia 24.7 na 1,560,507 na daraja la pili sawa na asilimia 75.3.

WAKULIMA

Rashid Mohamed, ni mkulima wa Njopeka Rufiji, rai yake kwake anamuomba mkuu wa mkoa kusimamia pembejeo zifike kwa wakati lakini pia changamoto zinazosababisha kushuka kwa madaraja ya zao hilo.

Naye, Abdul Idd, mkazi wa Rufiji, aliwashauri wakulima kuridhia bei iliyotajwa na wanunuzi na zilizobaki ziuzwe katika mnada wa pili.

Katika mnada huo wa korosho msimu uliopita, mauzo ya korosho Mkoa wa Pwani, kilo zilizoingia sokoni kwa daraja la kwanza ni 260,558; daraja la pili ni kilo 1,479,496 kwa bei ya juu Sh.2, 153 ya chini Sh. 2,052.

Aidha, korosho daraja la kwanza ziliuzwa zote huku la pili likisubiri mnada wa awamu ya pili kutokana na wakulima kutoridhishwa na bei iliyotajwa na wanunuzi.

Habari Kubwa