RC Songwe acharuka uzembe wa maliasili kuharibiwa na wazawa

23Jun 2022
Ibrahim Yassin
Songwe
Nipashe
RC Songwe acharuka uzembe wa maliasili kuharibiwa na wazawa

 
SUALA la umuhimu wa utunzaji mazingira katika vijiji mkoani Songwe, limeendeleza sintofahamu, kisa kikuu ni wakazi kutojua umuhimu wake, licha ya elimu kutolewa na viongozi husika, kukishuhudiwa uvamizi na ukataji miti, pia kuharibu rasilimali hizo.

Mandhari ya mazingira ya Ziwa Rukwa.

Hapo athari inajitokeza katika uharibifu na kuzorotesha mazingira kwa njia ya kupunguza rasilimali kama vile hewa, maji na udongo na kupotea wanyamapori, uharibifu wa mazingira kwa hasa makazi ya asili na maliasili yanatumiwa vibaya.

Uharibifu wa mazingira uko katika orodha ya vitisho 10 vinavyotajwa na Benki ya Dunia, pia Umoja wa Mataifa na mashirika yake ya Rasilimali Duniani, Mpango wa Mazingira na Mpango wa Maendeleo, zote zikitoa ripoti kwa umma kuhusu afya na mazingira duniani, mnamo Mei Mosi, mwaka 1998.

Kuhusu mazingira na afya ya binadamu, sehemu maalum katika ripoti hiyo inaeleza jinsi magonjwa yalivyo na mtazamo uliopo, ni iwapo kuna marekebisho makubwa katika afya ya binadamu, maana yake mamilioni ya watu wataishi muda mrefu na wenye afya bora.

Katika Ziwa Rukwa, tarafa ya Kwimba, wavuvi wanalia kukosa kitoweo, huku halmashauri yao kupitia kata ya Udinde, ikikosa mapato kutokana na samaki kutoweka, vijana wengi wanakimbilia kwenda kuvua Sumbawanga.

Wilayani Mbozi, kijijini Nyamwaga penye msitu wa asili, nako imekatwa na kutumika kuchoma mkaa.

Msitu wa Longort, wenye miti mingi ya aina tofauti na ya asili, nao umeharibiwa na miti yake kuchomwa mkaa, hali inayomuamsha kiongozi wa mila, kwenda kushitaki kwa mkuu wa mkoa.

Chifu Mleshelwa Nzunda, amefika kwa Mkuu wa Mkoa kutoa ombi, akitaka kutiliwa mkazo uharibifu wa mazingira, akidai hali iliyopo ikiendelea, kuna shaka misitu yote itamalizika na mkoa kuingia kwenye majanga.

Anafafanua kwamba, wao wazee wa mila wapo tayari kuisaidia serikali kutumia nyoka maalum kulinda misitu kwenye maeneo yote, ili kuwadhibiti wanaoleta madhara kwenye msitu.

“Watoto wetu shuleni wanakaa chini kwa upungufu mkubwa wa madawati uliopo kwenye shule zetu,” anasema Nzunda na kuendelea:

“Leo hii, miti hiyo badala ya kutumika kutengenezea madawati, watu wanakata bila utaratibu na ushauri kisha wanachomea mikaa,waturuhusu tuingize nyoka kwa ulinzi.

“Hata sisi wazee wa mila tunakosa mahala pa kufanyia matambiko, kutokana na misitu kukatwa ovyo. Tunaomba serikali itupe kibali, nyoka zilizopo katika misitu hiyo zitumike kwa ulinzi.’

VIONGOZI WAKERWA

Costina Kibona, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbozi, anaomba sheria iwachukulie hatua wananchi wanaokata kuni msituni, kwani wamekuwa wakidhalilishwa na maofisa misitu, lakini wameshindwa kuwadhibiti waharibifu wakubwa.

Cosmas Nshenye, Mkuu wa Wilaya Mbozi, anasema uharibifu wa mazingira katika wilaya hiyo umewashtua wengi, kwani kumekuwapo watu wanaovamia na kukata miti, pia kuchoma mkaa bila ya kujali kuwa ni kosa.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omari Mgumba, anasema baada ya kufanya ziara katika maeneo ya misitu, ameona uharibifu mkubwa wa miti na uchomaji mkaa, akishangaa kuwapo matanuru makubwa ya mikaa.

Katika hilo, anamuagiza mtendaji wake, Katibu Tawala kuwasimamisha kazi viongozi husika; Ofisa Misitu wa Mbozi, Ofisa Tarafa wa Vwawa, pamoja na Mkuu wa kitengo cha Usafi wa Mazingira na hatua hiyo, pia ielekezwe kwa watendaji wote wanaozunguka msitu wa Namwanga, kwa kushindwa kudhibiti uharibifu huo.

Pia, Mgumba anaagiza polisi kuwasaka watu sita waliotajwa kuhusika na ukataji miti na kuwateka waandishi wa habari na viongozi wa serikali waliofika kuona uharibifu huo.

‘Siwezi kukubali ‘nitumbuliwe’ na Rais aliyeniteua, kwa ajili ya uzembe wa viongozi wengine wanaoshindwa kusimamia majukumu yao. Nitahakikisha waharibifu wote wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,” anasema Mgumba.

Ziara ya ukaguzi wa mazingira katika baadhi ya wilaya mkoani humo, iliangukia Siku ya Mazingira Duniani, ambayo kimkoa ilifanyikia wilayani Mbozi.

Mgumba anatumia nafasi hiyo kukemea baadhi ya vitendo vya wakazi wa Mbozi, wanapotajwa kuhusika na uharibifu wa mazingira na wanalipa visasi kuharibu mali za viongozi  wa vijiji, kwa madai ‘wamewachongea’ kwa viongozi wa juu mkoani.

VIVUTIO NA MALIASILI

Mkuu wa Mkoa Mgumba, anasema mkoa wa Songwe umekuwa na vivutio vingi vinavyopaswa kutunzwa, ili mazingira yake yawe bora na wezeshi kuvutia watalii.

Anataja baadhi yake, ni Kimondo cha Mbozi,Unyayo na michoro ya watu wa kale kwenye kijiji cha Nkangamo wilayani Momba na Kanisa la Kale katika kijiji cha Mkulwe wilayani Momba.

Maeneo mengine ni katika kijiji cha Nanyara kilichopo Mbozi, maeneo yaliyoko wilayani Momba ni: Bwawa la Chumvi kijijini Itumbula; madaraja ya kunesa, maarufu ‘vitepu tepu’, Kamsamba na sehemu za kutengenezea udongo kuwa chuma zilizoko Kapele, Zaka na Ikana.

Aidha, anataja vivutio vilivyoko Momba na mlima Kwimba unaotumika kwa matambiko ya jadi, mbuga za wanyama za Lwati Songwe na jua linaloakisi mwanga Ibwembingu, pia maporomoko ya maji kwenye mto ulioko wilayani Ileje.

Vingine ni ngoma za asili Ing’oma kwa makabila ya Ileje kama vile Lipango, Ndili na Namlala.

Mwandishi anapatikana kwa mawasiliano: baruapepe; [email protected] na simu + 255 766 936392 na 0718 382817.