Rekodi 8 kali imba ikitwaa ubingwa

26Jul 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Rekodi 8 kali imba ikitwaa ubingwa

HATIMAYE Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21 ilimalizika rasmi Julai 18 na Simba kukabidhiwa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu.

Timu hiyo yenye maskani yake Msimbazi, siku ya mwisho iliichapa Namungo mabao 4-0 na kumaliza ligi ikiwa na pointi 83, kwa mechi 34 ilizocheza.

Katika mechi hizo ilishinda michezo 26, sare tano na kupoteza michezo mitatu.

Ubingwa huo umeipatia tena nafasi ya kwenda tena kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao, ambapo msimu huu iliishia hatua ya nusu fainali.

Kwenye makala haya, tunaangalia rekodi mbalimbali ambazo Simba imeweka msimu huu kwenye Ligi Kuu.
#1 Kutwaa mara nne mfululizo

Simba imetwaa ubingwa mara nne mfululizo baada ya miaka 42 kupita. Mara ya mwisho ilikuwa ni mwaka 1979 ilipotwaa mara nne mfululizo kuanzia mwaka 1976. Timu hiyo pia iliendelea kutwaa ubingwa hata msimu uliofuata wa 1980, kabla ya kunyang'anywa mwaka 1981 na Yanga, hivyo kuweka rekodi ambayo inayo hadi leo ya kutwaa mara tano mfululizo.

#2 Kufunga mabao mengi

Imetwaa ubingwa ikiwa imefunga mabao mengi zaidi kuliko timu nyingine yoyote ile. Simba imeweka nyavuni mabao 78 kwenye Ligi Kuu msimu huu, ikifuatiwa kwa mbali na watani zao wa jadi Yanga ambao walifunga mabao 52 tu.

#3 Imefungwa mabao machache

Mbali na kutwaa ubingwa, Simba imeweka rekodi nyingine ya kuwa timu iliyofungwa mabao machache zaidi. Imefungwa mabao 14 tu kwa mechi 34 ilizocheza, ikifuatiwa na Yanga ambayo imefungwa mabao 22.

#4 Straika wake atwaa kiatu

Rekodi nyingine ambayo imeweka Simba ni kwamba straika wao, John Bocco ametwaa kiatu cha dhahabu. Bocco, aliyesajiliwa na klabu hiyo mwaka 2017, amekuwa mfungaji bora wa msimu baada ya kukwamisha wavuni mabao 16.

#5 Mastraika wake wafuatana kileleni

Nusura wachezaji wa timu hiyo wawili, Bocco, na Chriss Mugalu wagongane kwa mabao 15 ambapo ingekuwa ni rekodi ya aina yake, kabla ya Bocco kupata bao kwa mkwaju wa penalti dakika za mwisho kwenye mechi dhidi ya Namungo na kuwa wa 16.

Msimu huu Simba imeweka rekodi ya wao kufuatana kileleni kusaka kiatu cha dhahabu na ilikuwa ni vigumu kutabiri nani angetwaa.

Wachezaji hao ni Bocco aliyemaliza na mabao 16, Mugalu aliyeshika nafasi ya pili kwa mabao 15, pamoja na Meddie Kagere aliyekamata nafasi ya nne kwa mabao 13. Aliyechafua gazeti ni Prince Dube wa Azam FC aliyeshika nafasi ya tatu kwa kumaliza na mabao 14.

#6 'Kiatu' mara ya nne mfululizo

Timu hiyo imeweka rekodi nyingine ya mastraika wake kuwa wafungaji bora kwa misimu minne mfululizo.

Tangu msimu wa 2017/18, Simba imekuwa ikitoa mfungaji bora hadi msimu huu.

Msimu wa 2017/18, Mganda Emmanuel Okwi alitwaa kiatu cha dhahabu akipachika mabao 20, na msimu wa 2018/19, Mnyarwanda, Meddie Kagere alikuwa mfungaji bora, akipachika mabao 23, akatetea tena nafasi yake msimu uliofuata wa 2019/20 akikwamisha mabao 22, na msimu huu Bocco ameifanya Simba kutetea tena nafasi hiyo kwa mabao 16.

#7 Kipa wake aongoza kwa 'clean sheet'

Kipa wa Simba, Aishi Manula ameiongezea tena timu yake rekodi, kwa kuongoza kucheza mechi nyingi
Manula amemaliza ligi akiwa na 'clean sheet' 18, akifuatiwa na kipa wa Mbeya City Haroun Mandanda ambaye amesimama golini mara 15 bila kuruhusu wavu wake kutikiswa.

Metacha Mnata wa Yanga na Abutwalib Mshery wa Mtibwa Sugar, wana 'clean sheet' 13 kila mmoja, huku Jeremiah Kisubi wa Prisons.

Kipa mkongwe Juma Kaseja yeye amesimama langoni mara 11 bila kuruhusu bao pamoja na Aron Kalambo wa Dodoma Jiji, huku Daniel Mgore wa Biashara United akiwa na 'clean sheet' 10.

#8 Mastaa wake waliongoza 'assist'

Kwa mara nyingine tena, Simba imeweka rekodi kwa mchezaji wake Clatous Chama kutoa pasi nyingi za mabao maarufu kama 'assist'.

Hadi Ligi Kuu Tanzania Bara inamalizika, Chama ametoa 'assist' 15, akifuatiwa na mchezaji wengine wa Simba, Luis Miquissone ambaye ametoa pasi za mwisho kumi.