Rekodi, takwimu Ligi Kuu katika namba

17Jun 2019
Adam Fungamwango
DAR
Nipashe
Rekodi, takwimu Ligi Kuu katika namba

738- Hii ni idadi ya mabao yaliyofungwa kwenye Ligi Kuu msimu huu. Ni ongezeko la mabao 173 kwani msimu uliopita 2017/18, jumla ya mabao 600 yalifungwa kwenye Ligi msimu huo.

Wachezaji wa Simba wakipongezana kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union ambayo imetengeneza takwimu na rekodi kwa kuzaa hat-trick mbili kwenye mechi moja msimu wa 2018/19.

Hata hivyo, msimu huu kuna ongezeko la timu nne, zaidi kutoka 16 za msimu uliopita hadi 20.

243- Namba hii inasimama kama ni idadi ya wafungaji wote waliofunga mabao kwenye Ligi Kuu msimu uliomalizika. Idadi hii imeongezeka zaidi kwani msimu uliopita 2017/18 ilikuwa ni wachezaji 156.

52- Ni idadi ya penalti zilizotolewa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara iliyomalizika 2018/19. Msimu uliopita kulikuwa na jumla ya penalti 38, hivyo msimu huu kumekuwa na ongezeko la penalti 12 zaidi.

 

44- Namba hii inasimama kama idadi ya penalti zilizofungwa au kuwekwa nyavuni na wachezaji mbalimbali za Ligi Kuu msimu uliomalizika. Penalti 32 zilifungwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita kwa hivyo zimeongezeka penalti 12 msimu huu zilizotiwa kwenye kamba.

 

17- Hii ni idadi ya mabao yaliyofungwa kwenye raundi ya mwisho ya Ligi Kuu, jumla ya timu zote 20 zikishuka dimbani kwenye viwanja mbalimbali nchini kumalizia mechi zao, kila timu ikicheza mechi ya 38.

 

15- Haya ni mabao yaliyofungwa kwenye raundi ya ufunguzi wa Ligi Kuu msimu huu. Baada ya timu zote 20 kucheza mechi za kwanza kulikuwa na idadi hii ya mabao, ambayo yalikuwa ni pungufu ya mawili ya idadi ya mabao ya mechi za mwisho.

10- Hii ni idadi ya mabao ya kujifunga kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu mzima. Mashabiki wa soka katika hili wanawakumbuka zaidi wachezaji wawili ambao ni Ally Ally wa KMC aliyejifunga mwenyewe kwenye mechi dhidi ya Yanga na timu yake kuchapwa mabao 2-1, mwingine ni Mohamed Hussein 'Tshabalala' aliyejifunga kwenye mechi ambayo timu yake ya Simba ilicheza dhidi ya Kagera Sugar na kuwa bao pekee kwenye mechi hiyo, Simba ikilala bao 1-0.

9- Ni rekodi ya idadi kubwa zaidi ya mabao yaliyofungwa kwenye mechi moja msimu huu. Hii ilikuwa ni mechi kati ya Simba dhidi ya Coastal Union. Mechi hiyo ilichezwa Mei 8, mwaka huu na Simba iliibugiza bila huruma Coastal Union mabao 8-1 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

8- Hii ni namba inayosimama kwenye idadi ya penalti zilizokoshwa au kuota mbawa kwenye Ligi Kuu msimu huu uliomalizika. Msimu uliopita ni penalti sita tu ziliota mbawa na kuwa na ongezeko la penalti mbili. Lakini pia namba hii inasimama kama ni idadi ya wachezaji waliokosa penalti kwenye Ligi Kuu msimu uliomalizika. Ina maana kuwa wachezaji wote wamekosa penalti moja moja na hakuna aliyekosa mara mbili kwenye mechi moja, au tofauti.

5- Hat-trick tano zimefungwa msimu huu uliomalizika. Ni idadi ya hat-trick sawa na ya msimu uliopita  iliyomalizika kukiwa na jumla ya hat-trick tano.

Namba hii pia inasimama kuwa ni idadi ya penalti zilizofungwa na straika wa Simba John Bocco ambaye ndiye anayeongoza kwa kufunga penalti nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu msimu huu.

3- Ni idadi ya wachezaji wa kigeni waliofunga mabao matatu kwenye mechi moja, maarufu kama 'hat-trick' msimu huu. Hawa ni Mganda Emmanuel Okwi na Mnyarwanda Meddie Kagere, wote wa Simba ambao kila mmoja alifunga kwenye mechi dhidi ya Coastal Union. Mwingine ni Alex Kitenge raia wa Burundi akiichezea timu ya Stand United alifanya hivyo kwenye mechi dhidi ya Yanga, lakini timu yake ikifungwa mabao 4-3.

1- Inasimama kwa straika Salum Aiyee ambaye ni Mtanzania pekee amefunga mabao mengi zaidi kwenye ligi msimu huu. Mchezaji huyo wa Mwadui amemaliza ligi akiwa amecheka na nyavu mara 18 nyuma ya kinara Mnyarwanda Kagere. Namba hii pia inasimama kwake ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliomalizika. Alifanya hivyo kwenye mechi ya ufunguzi Agosti 22, mwaka jana kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Kagera, alipoifungia timu yake bao dakika ya tisa tu ya mchezo, mechi iliyoisha kwa timu yake ya Mwadui kuchapwa mabao 2-1. Mabao yote ya mechi zote 10 za ufunguzi yalifungwa baada ya dakika hiyo kupita.

Pia namba hii inasimama kwa Aiyee  kama mchezaji pekee wa Kibongo nchini kufunga 'hat-trick' msimu huu. Alifanya hivyo kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa Uwanja wa Mwadui Complex, timu yake ikishinda mabao 4-0.

Habari Kubwa