RIPOTI MAALUM: Ajali za bodaboda zafilisi damu Hospitali Mkuranga

01Sep 2016
Yasmine Protace
Mkuranga
Nipashe
RIPOTI MAALUM: Ajali za bodaboda zafilisi damu Hospitali Mkuranga

MKURANGA ni moja ya wilaya za mkoa wa Pwani iliyoko katika barabara kuu iendayo mikoa ya Kusini; Lindi na Mtwara. Pia imepakana na wilaya ya Rufiji katika mkoa huo, ambao ndio umepakana na Lindi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Mkuranga, Awadh Myilulu.

Wilayani hapo kuna wakazi 200,000 wanaohudumiwa na hospitali ya wilaya ambayo kwa mujibu wa muundo wa huduma zas tiba kitaifa, ndio kuu kiwilaya na kwa mkoa, hospitali kuu ni ya Tumbi- Kihaba, ambayo ni ya rufaa.

Licha ya hadhi iliyo nayo, sehemu kubwa ya huduma zitolewazo na Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga kwa wenye magonjwa makubwa ni huduma ya kwanza.

Kutokana na jiografia ya mahali iliko Hospitali ya Mkuranga, iko umbali wa kilomita 91 kutoka Hospitali ya Tumbi. Ni safari ambayo lazima ipitie jijini Dar es Salaam.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkuranga, Dk. Annuar Mnyilulu, anasema idadi hiyo kubwa ya wakazi wanaotegemewa wanahudumiwa na hospitali yenye jukumu moja tu kwa wagonjwa wenye hali mbaya, kwamba wanapewa huduma ya kwanza pekee.

Dk. Mnyilulu anasema hospitali anayoiongoza haina vifaa muhimu kama vile mashine za X-ray na madaktari bingwa wa kutoa huduma muhimu, ikiwamo mtaalam wa mifupa, ambaye ni miongoni mwa wanaohitajika sana, kulingana na aina ya wagonjwa anaowapokea kwa wingi .

Pia, inaelezwa kuwapo gari moja tu ya wagonjwa, wanaolazumika kukimbizwa kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambako ni umbali wa kilomita 47.

Mganga huyo mfawidhi, anasema upungufu huo hulazimisha kuomba gari kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya, kwa ajili ya kusafirisha mgonjwa kwenda Muhimbili, pindi mahitaji yanapotokea, hali amabyo ni ya kawida kwea kujitokeza kila mara.

UPUNGUFU WA WODI

DK. Mnyilulu anasema eneo la Mkuranga mara nyingi kunakabiliwa na tatizo la kuwapo majeruhi wengi watokanao na uendeshaji mbaya wa pikikipiki za biashara, maarufu kama bodaboda.

Anasema mara nyingi wanalazimika kuwachanganya wagonjwa wa matatizo mengine na majeruhi wa ajali katika wodi moja, jambo ambalo si sahihi kitaaluma na kibinadamu.

“Kwa kweli tunapokea waathirika wengi wa ajali. Kwa mfano, mwezi Julai mwaka huu, tulipokea majeruhi 19, lakini tunalazimika kuwachanganya na wagonjwa wa matatizo mengine, kwa sababu hatuna jengo maalum kwa ajili ya majeruhi.

“Si jambo zuri, unampatia huduma ya kwanza majeruhi, huku mgonjwa mwingine anaangalia. Hivyo tunaiomba serikali itupatie jengo maalumu kwa ajili ya majeruhi wa ajali, ili tuweze kuwatenganisha wakati wa kuwahudumia,” anasema.

Dk. Mnyilulu anafafanua kuhusu wagonjwa majeruhi hasa wa ajali zas pikipiki, wengi ni wenye umri kati ya miaka 18 na 38.

OFISA USTAWI JAMII

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Mkuranga, Peter Nambanga, anasema hospitali ya wilaya hiyo, hivi sasa ndiyo tegemezi kuu kiwilaya, lakini inakabiliwa na uhaba mkubwa wa damu kutokana na kuwapo ajali nyingi za bodaboda.

Nambanga anaeleza masiktiko yake namna ajali zilivyoongeza matumizi ya damu, jambo linalohitaji ufumbuzi wa haraka, katika azma ya kuokoa maisha ya jamii ya Mkuranga.

Ombi lake kwa umma ni kwamba, kufanyike uhamasishaji wa
wananchi wajitolee kuchangia damu, ili kunusuru mahitaji ya matumizi ya damu hospitalini Mkuranga.

''Kila siku, lazima watafikishwa majeruhi watatu wa bodaboda, hivyo kabla ya kuhudumiwa lazima waongezewe damu,'' anasema Nambanga.

Malalamiko ya Ofisa Ustawi Jamii huyo, ni kwamba ajali zitokanazo na bodaboda zinaongezeka kutokana na kasi ya kushamiri biashara ya bodabda.

Kwa mujibu wa Ripoti ua Utafiti uliofanyika katika kata tisa, kati ya 25 wilayani hapo, ambako kuna vijana 900 wa Mkuranga wanaojishughulisha na biashara ya bodaboda.

Nambanga analalamika kuwa, sehemu kubwa ya waendesha bodaboda hawana elimu ya sheria za barabarani, hali inayochangia kuwapo ajali za kila mara.

Anaongeza:“Vijana wengi wanaoendesha bodaboda, hupatwa na mikasa ya ajali, kutokana na kuendesha kwa mwendo kasi, ili waweze kupata kiasi cha fedha na kutimiza malengo ya mmiliki wa chombo, hali ambayo huwafanya wakiuke sheria na taratibu zote za barabarani.”

Nambanga anasema kuwa, hivi sasa Halmashauriya Wilaya Mkuranga, inaandaa sheria ndogo wanayohisi itasaidia kupunguza ajali hizo.

“Sheria na adhabu zinazotaka kuletwa, hazitaweza kumaliza tatizo hilo. Lakini tunapaswa kutafiti na kugundua zaidi nini kinawafanya vijana hawa kuzidi kuwa sehemu kubwa ya ajali pamoja na kuwapatia elimu?” anahoji Nambanga.

NINI KIFANYIKE?

Mkuu wa Wilaya, Filberto Sanga, anaungana mkono na hoja za awali, kwamba kuwapo ajali nyingi kunafilisi akiba ya damu hospitalini Mkuranga. Anaeleza shaka yake, endapo itatokea mazingira ya damu kwisha, wakati kuna mahitaji ua dharura kutoka kwa wagonjwa.

Sanga ambaye ni mmoja wa wachangiaji damu katika hospitali hiyo, anasema kuna haja ya kutolewa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda, ili kupunguza kasi ya ajali.

“Mahitaji ya damu ni makubwa sana. Licha ya kutumika kwa majeruhi wa ajali, pia inahitajika kwa baadhi ya mama wajawazito. Natoa rai wananchi wenzangu wa Mkuranga, kila mmoja ajitahidi aje na watu 10 tuchangie damu kuokoa maisha ya wengine,” anasema.

Wakati huo anasema wameguswa na tatizo la ukosefu wa damu katika hosptali hiyo ambayo ni tegemezi katika masuala ya tiba na afya kwa wakazi wa wilaya nzima.

Mwenyekiti wa Muungano wa Asasi za Kiraia za Wilayani Mkuranga, Ally Ngalema, anasema kutokana na hali hiyo mbaya ya akiba ndogo ya damu inayochangiwa na mwenendo mbaya wa waendesha bodaboda, wamebuni programu maalum ya kuzunguka wilaya nzima kuhamasisha uchangiaji damu salama.

Ngalema anasema wanafanya hilo kuunga mkono jitihada za serikali wilayani hapo kuokoa maisha ya wahitaji damu, hasa wajawazito na watoto ambao ni wanahitaji wakuu.

Kwa mujibu wa Ngalema, mikakati huo utahakikisha unafika katika kata zote 25 za wilaya kuhamasisha wananchi wanashiriki katika kuchangi damu salama. Pia wananuia kujitolea kufanya usafi hospialini Mkuranga.

Ngalema anataja jingine katika mkakati wa muugano huo wa asai binafsi, ni kufanya kikao cha kuwashirikisha wadau wa bodaboda ambao ni waathirika wakuu wa ajali hizo kuona umuhimu wa kuchangia damu hospitalini.

Anasema wananuia kuwapa mafunzo ya usalama barabarani waendesha bodaboda na kuwahamasisha kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya, utakaowasaidia kukabili gharama katika dharura zote za kuumwa kwa namna mbalimbali.

“Katika kuhakikisha tunamaliza tatizo la ajali hizo katika wilaya yetu, tutatengeneza mfumo rahisi utakaomsaidia kila dereva wa bodaboda awe na chombo chake na kuhakikisha wanakuwa na mikataba, ili waweze kuzijua haki zao,” anasema Ngalema.

"Kutokana na utafiti tuliofanya, tumebaini kuwa bodaboda tisa kati ya 10, chombo si mali yake (dereva). Pia, hawana mikataba. Ajali inapotokea, si rahisi kupata haki yake. Kutokana na kuliona hilo, tutahakikisha wanaingia mikataba ili kuwarahisishia kujua na kupata stahiki zao,'' anasema.

Mratibu wa muugano wa asasi hizo, Faustin Onyango, anasema baada ya kupata taarifa kuhusu uhaba wa damu hospitalini, waliguswa na kuamua kulibeba tatizo hilo kwa ajili ya kuishirikisha jamii iweze kuchangia.

Onyango anadokeza kuwa bodaboda nyingi za Mkuranga hazijasajiliwa na madereva wake hawana leseni na ujuzi utokanao na mafunzo rasmi ya udereva wa pikipiki.

Onyango anazungumzia faini wanazotozwa waendesha bodaboda kutokana na ajali za barabarani, kwamba hazisaidii kupunguza ajali, hivyo kinachotakiwa ni kuhakikisha madereva wa pikipiki wanapatiwa elimu ya usalama barabarani, ndiyo nyenzo sahihi ya kupunguza matukio ya ajali.

Ushauri wa Onyango unaendana na hoja ya kuwashauri wazazi kuingilia kati kuwadhibiti watoto wao waache kuendesha bodaboda bila ya kuwa na sifa zinazotambulika kisheria.

"Kuna baadhi ya wazazi (na walezi) hufurahia kuletewa fedha na watoto wao ambao kiumri ni wadogo na hawana sifa mtambuka na anashauri wawe makini na kuachana na kasumba hiyo, ambayo inaweza kugharimu maisha ya watoto hao au kuwapatia ulemavu wa kudumu,'' anasema.

Habari Kubwa