RIPOTI MAALUMU:Uvunaji haramu watishia mikoko kutoweka nchini

20Aug 2016
Moshi Lusonzo
Nipashe
RIPOTI MAALUMU:Uvunaji haramu watishia mikoko kutoweka nchini

UVUNAJI na utoroshaji wa raslimali za mikoko katika maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi nchini, umeshamiri kwa kiwango cha kutisha huku serikali ikikiri kushindwa kudhibiti biashara hiyo.

Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, misitu ya miti hiyo ambayo ni muhimu katika utunzaji wa mazingira, imeteketezwa kwa kasi kubwa na kusababisha tishio la kutoweka katika kipindi kifupi kijacho.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe katika pwani ya Bahari ya Hindi kuanzia Pemba Mnazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisiju na Rufiji mkoani Pwani, unaonyesha kuwa kila wiki, zaidi ya tani 40,000 za miti ya mikoko inakatwa na kuuzwa ndani na nje ya nchi.

Kiwango hicho cha uvunaji ni sawa na majahazi matano yenye uwezo wa kubeba tani 800 yanayofanikiwa kutorosha maliasili hiyo bila kukamatwa.

Soko kubwa la miti hiyo liko visiwani Zanzibar, Umoja wa Falme za Kiarabu, visiwa vya Shelisheli na Comoro.

Hata hivyo, aliyekuwa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Gerald Kamwenda, alikiri uzuiaji wa biashara hiyo ni mgumu kutokana na kuhodhiwa na wafanyabiashara wakubwa na ukosefu wa vitendea kazi kwa watumishi wakala.

DHAHABU YA KIJANI

Miti ya mikoko inafahamika kwa jina la ‘Dhahabu ya kijani’ kutokana na kuwapatia faida kubwa watu wanaojihusisha na biashara hiyo. Miti hiyo inapatikana katika maeneo ya makutano ya mito na fukwe za bahari katika ukanda wa kitropiki.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Tanzania ina hekta 115,000 za misitu ya mikoko katika pwani yake kuanzia Tanga hadi Mtwara. Lakini nusu ya misitu hiyo (hekta 52,000), ziko ndani ya mlango bahari wa Mto Rufiji.

Akizungumza na Nipashe, ofisa kutoka TFS, Florian Kaaye, anasema eneo hilo kubwa lilitengwa kama hifadhi ya misitu tangu miaka ya 1930 na serikali ya Ujerumani.

Miti hiyo inakomaa na kuwa tayari kuvunwa kuanzia miaka mitano hadi 100 kulingana na aina husika.

Aina hii ya miti inapostawi, samaki hawachezi mbali kutokana sehemu hiyo kuwa nzuri kwa kutagia mayai na kutengeneza chakula cha samaki.

Miti hiyo pia ni muhimu kwa kuzuia mmonyoko wa udongo kwenye kingo za bahari na ina uwezo mkubwa wa kunyonya hewa ukaa kwa muda mfupi.

Hata hivyo, sifa yake mikoko ni uimara na kudumu muda mrefu na watu wamekuwa wakitumia mbao na nguzo za miti hiyo katika ujenzi.

Wataalamu wanaeleza kuwa nguzo za mikoko zinapotumika kujengea nyumba, hudumu kwa zaidi ya miaka 100 bila kuharibiwa na wadudu.

HALI HALISI

Katika uchunguzi uliofanywa, imebainika kuwa misitu ya miti hiyo katika maeneo ya Pemba Mnazi, Kimbiji na Tundwi Songani ni kama imekwisha baada ya kufyekwa kwa kasi ya ajabu.

Katika sehemu ambazo miaka miwili iliyopita kulikuwa na misitu ya miti hiyo, kwa sasa vimebaki visiki na mabaki ya magogo na matanuri ya mkaa yakiwa yamezagaa kila mahali.

Katika eneo la Tundwi Songani, kwa mfano, eneo hilo lenye kilomita saba za mraba za mikoko, tano zimeshatoweka na upande wa delta ya Mto Rufiji, zaidi ya hekta 1,200 zimeteketea hadi sasa.

Meneja wa TFS Mkoa wa Pwani, Suleiman Burenga, anasema makisio ya kiwango hicho ni kikubwa licha ya kikosi chake kujitahidi kuzuia.

Burenga anasema mwaka 1995 hekta 3,800 ziliangamizwa, na hadi mwaka 2011 zaidi ya hekta 9,000 ziliteketea kutokana na uvunaji huo haramu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Songani, Abdulmalik Ally, anasema hifadhi ya mikoko kwenye makutano ya Mto Mbezi na Bahari ya Hindi imetoweka kwa kasi ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Anasema watu wanaojishughulisha na biashara hiyo ni wafanyabiashara na viongozi wa serikali ambao wanafadhili kwa kutoa pesa nyingi.

Ally anasema kwa upande wa eneo lake, jumla ya kilomita tano za mraba za misitu zimekatwa na eneo lililobaki la hekta moja linakaribia kumalizwa kutokana na kasi kubwa ya ukataji haramu.

Anasema kila wiki majahazi mawili hufika na kubeba shehena za magogo, mbao, nguzo na mkaa na kusafirisha nje ya nchi.

Mwenyekiti huyo anaeleza imekuwa vigumu kuwazuia wahusika kutokana na kutishia kuwashambulia kwa silaha za moto.
“Ni kazi ngumu kwetu kama serikali ya mtaa kuwazuia. Unapoonekana kuwa kikwazo, wanajitokeza watu wazito wanakutishia hata silaha za moto. Hali ni mbaya tunaomba serikali iingile kati suala hili haraka,” alisema Ally.

Alisema hivi karibuni wamebadili utaratibu wa kuingia msituni baada ya kuwapo tishio la kukamatwa, badala yake kazi hiyo inafanyika nyakati za jioni na usiku.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo, Omar Mgeni, alisema wavamizi hao wanatumia mbinu mpya kila siku kukwepa kukamatwa.

Mmoja wa wakataji miti hao, Hashimu Muharami, alikiri kuhusika katika vitendo hivyo, akisema yote anafanya kwa sababu anajitafutia riziki.

Alisema wanatumwa na matajiri wao kukata miti kwa malipo ya kati ya Sh. 200,000 na 400,000 kulingana na idadi wanayohitaji.

“Tunapokwenda kukata miti tunakuwa kundi la watu sita hadi saba. Tunahakikisha kwanza tunalipwa malipo ya awali na tukimaliza tunamaliziwa pesa zetu wakati mzigo ukienda kupakiwa kwenye majahazi,” alisema Muharami.

BIASHARA HATARI

Wahusika wa biashara hiyo, ambao walizungumza na gazeti hili (majina yanahifadhiwa kwa usalama), walieleza usafirishaji wa rasilimali hiyo hufanywa kwa tahadhari kubwa ili kujilinda na polisi.

Mmoja wa watu hao, alisema wakati wa kusafirisha bidhaa za mikoko kwa maana ya mbao, nguzo, magogo na mkaa, wanatumia silaha na vitu vingine katika kuhakikisha mzigo huo unafika salama sokoni.

“Ni biashara nzuri yenye faida kubwa, lakini ni hatari sana polisi wakikukamata na ndiyo maana na sisi tunajilinda kwa silaha,” alisema.

Alisema bidhaa hiyo ina soko kubwa kisiwani humo na kwamba baada ya kufikishwa, sehemu kubwa husafirishwa katika nchi za Kiarabu na Shelisheli ambako kuna mahitaji makubwa.

“Mzigo ukifika Zanzibar unachambuliwa kwa kuangalia mahitaji. Nguzo zinauzwa hapo hapo kwa gharama kubwa kwa ajili ya ujenzi wa hoteli na nyumba za kifahari. Mbao na mkaa husafirishwa Uarabuni ambako kuna soko kubwa,” alisema.

Kutokana na ukubwa wa biashara na thamani ya miti hiyo, uchunguzi unaonyesha kuwa majahazi yanayotumika kubebea yanalindwa kiasi ambacho inakuwa vigumu polisi na maofisa misitu kuyafikia.

Meneja wa TFS Wilaya ya Rufiji, Henry Mallya, alikiri kuwa ni hatari kukabiliana na watu hao kama hakuna boti yenye nguvu na polisi wenye silaha.

Alisema kutokana na biashara hiyo kuwa na mtandao mkubwa, wakati mwngine wanaamua kuziachia boti zinazobeba ili kuokoa maisha yao. alisema baadhi ya watu waliothubutu kufuatilia waliangamizwa kwa kuzamishwa majini, hivyo wanahofia usalama wao.

Mallya ambaye ofisi zake ziko katika Kijiji cha Nyamisati, alisema wanakabiliwa na ukosefu wa boti na kwamba zilizopo hazina uwezo wa kukabiliana na nguvu ya majahazi makubwa.

Pia alisema wana upungufu mkubwa wa vitendea kazi, hivyo wanachokifanya ndicho kipo katika uwezo wao.

Kituo hicho ambacho kinafanya kazi ya kulinda misitu ya mikoko katika ukanda wa Pwani ya Mkuranga hadi Muhoro wilayani Rufuji, kina boti ndogo mbili ambazo zote zimechakaa na mbili kubwa zilizotolewa kama msaada, hazitoi huduma baada ya kuharibika.

Hata hivyo, alisema wanajitahidi kukabiliana na wahalifu hao kwa kutumia njia zingine ikiwamo kuwavamia na kuwakamata wakati wakipakia mizigo au wanaposafiri kwenye mapitio ndani ya delta hiyo kuelekea bahari kuu.

“Hata ndani ya mapitio tunakabiliwa na changamoto ya kukosa chombo chenye uwezo wa kutembea maji yakiwa yamerudi. Inatubidi tusubiri maji yanapojaa ndipo tunakwenda wakati huo wenzetu tayari wamefanya uhalifu,” aliongeza.

Kutokana na juhudi hizo, alisema kila wiki wanafanikiwa kukamata majahazi mawili na kutoza faini ya kati ya Sh. 500,000 na Sh. milioni moja.

Hata hivyo, alieleza viwango hivyo vya faini ni vidogo kulinganisha na mazao yanayovunwa na hatari ya kutoweka kwa rasilimali hiyo.

Akizungumzia utoaji vibali kwa wavunaji, Mallya alisema kwa mwaka huu jumla ya watu 15 wamepewa vibali na kwamba adadi kubwa ya watu wanatumia vibali bandia.

Ukataji holela wa mikoko umeanza kuleta athari nyingi katika maeneo mbalimbali ya pwani na kusababisha maisha kuwa magumu.

Asha Bakari, mkazi wa Kisiju, alisema katika kipindi kifupi wameshuhudia kuwapo kwa ukosefu wa samaki na baadhi ya mapitio ya bahari wanayotumia kutoka na kuingia ndani ya visiwa kujaa mchanga.

Mwanamke huyo ambaye anajishughulisha na biashara ya kukaanga na kuuza samaki, alisema upatikanaji wa bidhaa hiyo umekuwa mgumu kiasi cha wafanyabiashara kuu kwa Sh. 10,000 kwa samaki badala ya Sh. 5,000 ya awali.

Twalib Mketo, anayejishughulisha na uvuvi wa kaa, alisema ukataji wa mikoko umesababisha janga kubwa baada ya samaki kupungua baada ya kushindwa kuzaliana.

“Kawaida ya kaa wanazaliana chini ya miti ya mikoko, sasa haipo tena hata upatikanaji wake unakuwa mgumu na wakati mwingine kukosa kabisa,” alisema Mketo.

Zainabu Bori, kwa upande wake alisema wanawake waliokuwa wanajishughulisha na uchomaji chumvi katika fukwe za Shungu na Mbezi wamesimamisha shughuli zao baada ya kukosa kuni za mikoko.

Alisema awali walikuwa wakitumia kuni zinazotokana na miti ya mikoko, lakini baada kukatwa na wavunaji haramu, wamejikuta wakisimamisha kazi zao.

“Upikaji wa chumvi ulikuwa unatunufaisha kiuchumi kwa kuuza na kiasi kingine kwa matumizi ya nyumbani. Baada ya mikoko kukatwa tumekosa kuni za kupikia na imetubidi tusimame,” alisema.

Hata hivyo, alikiri kwamba walikuwa wakitumia kuni za miti hiyo bila kupewa ruhusa na mamlaka husika, lakini walitumia kwa kufuata utaratibu mzuri.

Abdallah Shomari, mchuuzi katika soko la Tundwisongani, alikubali kwamba bidhaa hiyo ya chumvi kwa sasa haipatikani licha ya kupendwa na wateja wengi kutokana na kuwa laini na yenye harufu nzuri.

Alisema kukosekana kwa bidhaa hiyo kumewarudisha nyuma baada ya wakazi wa eneo hilo kutopendelea chumvi ya viwandani.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema (sasa Mkuu wa Wilaya ya Ilala), alikiri kuwapo uharibifu wa miti hiyo na kueleza kwamba serikali inafanya jitihada ya kuhakikisha inalindwa.

Alisema doria za mara kwa mara zinafanywa kwa pamoja kati ya TFS na Idara ya Mazingira na Misitu ya Manispaa ya Temeke katika kukabiliana na watu hao.

Pamoja na jitihada hizo, alisema ni vigumu kumaliza tatizo hilo kutokana na jiografia ya bahari kuwa pana na yenye vikwazo vingi kufika eneo moja hadi lingine.

“Eneo la bahari ni kubwa, hatuwezi kuwaona wahalifu kwa kuwa hatuna zana za kisasa. Hata hivyo tutazidi kupambana nao pale tunapoweza,” alisema Mjema.

USHAURI MZITO

Ili kufanikisha vita dhidi ya wafanyabiashara haramu wa bidhaa za mikoko, baadhi ya wananchi wameishauri serikali kujenga mfumo mzuri kwa kuwashirikisha wananchi katika kulinda misitu hiyo.

Fatuma Saidi, mkazi wa Nyamisati, alisema wananchi wanaoishi maeneo ya misitu hawashirikishwi ipasavyo, badala yake wanaonekana kama maadui.

Alisema kama ungeandaliwa mpango maalumu wa kuwajengea uwezo kupitia vikundi, wangetumia raslimali hiyo kwa njia endelevu na kuilinda.

“Kama serikali ingesaidia kuunda vikundi vya wananchi na kisha kuwapa mitaji kama ya ufugaji wa nyuki na kuwakabidhi eneo la kufanya shughuli zao, lazima wangeilinda kwa sababu wanajua wakikata miti nyuki wanakimbia,” alisema Saidi.

Kauli hiyo, inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Songani, Abubakar Ally, ambaye alisema ushirikiano kati ya serikali na jamii hauko sawa, jambo linalosababisha watu kuona jukumu la kuitunza na kulinda mikoko si lao.

DC KIGAMBONI AJINASIBU

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, alisema serikali itahakikisha wilaya hiyo inakuwa na mpango bora wa ardhi ikiwa pamoja na kupima eneo lote na kuanisha shughuli zinazofanyika.

Alisema uharibifu wa mikoko unatokana na kuongezeka harakati ya maendeleo hasa katika ujenzi wa makazi, hivyo ni muhimu kila mwananchi atambue wapi anaishi na wapi hatakiwi kwenda kufanya kazi yoyote.

“Wilaya ya Kigamboni bado changa. Tunalazimika kuandaa mpango kabambe wa upimaji wa ardhi yote ili kila mtu atambue wajibu wake pamoja na utunzaji wa mikoko,” alisema Mgandilwa.

Naye Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile, alisema anaamini bila serikali kupambana na watu wanaonunua bidhaa hizo kwa wingi, kuna ugumu wa kufanikiwa katika mapambano hayo.

“Kuna matajiri wanatumia miti ya mikoko kwa ajili ya ujenzi wa nyumba zao. Hilo si siri linajulikana hata na serikali lakini linafumbiwa macho na hatimaye tunazidi kulaumiana wenyewe kwa wenyewe,” alisema.

NEMC YASHTUKA

Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC), Manchari Suguta, alipotakiwa kuelezea suala hilo, alisema ni jambo la kushtua na watalifanyia kazi katika kipindi kifupi kujua ukweli wake.

Alisema uvamizi na uvunaji wa mikoko ni kinyume cha sharia ya Mazingira kifungu cha 57 kifungu kidogo cha tano kinachoweka katazo la kufanya shughuli zozote za binadamu katika hifadhi ya bahari hususan kwenye mikoko.

Aidha, Sheria ya Ardhi, kifungu cha kwanza hadi saba na kile kidogo (A-B), inazuia watu kuendesha shughuli zozote mita 60 kutoka pigo la mwisho la maji ya bahari.

TFS YAJITETEA

Aliyekuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa TFS, Gerald Kamwenda, alisema uvamizi na uharibifu wa misitu utatoweka tu endapo chombo hicho kitabadilishwa na kuwa mamlaka kamili.

Alisema endapo watafanikiwa watakuwa na uwezo wa kuunda kikosi cha askari ambacho kitakuwa na jukumu la kupambana na wahalifu.

Kamwenda alisema ulinzi wa majini una gharama kubwa, boti moja pekee inahitaji mafuta lita 200 kwa siku, wao kama wakala hawana uwezo huo kutokana na kukosa fedha.

“Kama tungekuwa mamlaka kamili tungeweza kuunda jeshi letu la kulinda misitu, kununua boti na kuzihudumia. Sisi wenyewe tungeweza kupambana nao bila kusubiri polisi au nguvu za nje,” anasema Kamwenda.

Alisema Wakala ina upungufu mkubwa wa wafanyakazi, jambo ambalo limerudisha nyuma udhibiti wa misitu ikiwamo mikoko.

Mtendaji huyo anaitaja Zanzibar kuwa kitovu cha biashara hiyo na kuomba kuwapo majadiliano kati ya Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar namna ya kuizuia.

Alisema kutokana na sheria za Zanzibar kutopiga marufuku uuzaji wa bidhaa zitokanazo na mikoko, kisiwa hicho imekuwa kama njia muhimu ya kusafirishia bidhaa za rasilimali hiyo kwenda nje ya nchi ambako kuna soko kubwa.

“Kunahitajika majadiliano ya wazi kuhusu hali hii na wenzetu wa Zanzibar, kwani inaumiza ikiwa sisi tunatunza misitu wao wanakuja kuvuna tena kwa njia haramu,” anatamatisha Kamwenda.

SERIKALI YAFUMBUKA
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, alisema suala la utunzaji wa misitu ni endelevu na wameanza hatua ya kuifumua TFS ili kuboresha utendaji kazi.

Hatua hiyo, alisema imechukuliwa baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuagiza kuchunguzwa kwa chombo hicho na kujipanga upya baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.

“Hatukuridhika na utendaji wa TFS. Misitu yote hata ya mikoko ni muhimu kutunzwa hivyo tumeamua kuwaondoa baadhi ya watendaji kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji na kukabiliana na uvunaji haramu wa mazao ya misitu,” alisema Prof. Maghembe.

Katika mabadiliko hayo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu, Kamwenda na wakurugenzi wenzake wameondolewa na kuhamishiwa katika vitengo vingine na Profesa Dos Santos Silayo ameteuliwa kushika nafasi hiyo.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa