Rita yaanika mapinduzi yake toka utendaji hadi makusanyo

14Feb 2020
Maneno Selanyika
Dar es Salaam
Nipashe
Rita yaanika mapinduzi yake toka utendaji hadi makusanyo
  • *Uandikaji wosia sasa ni foleni
  • *Vyeti watoto; kata, shule, kliniki
  • *Elekroniki yaibua mageuzi mapato

KATIKA kuboresha utumishi wa umma chini ya Programu ya Kuboresha Utumishi wa Umma (Public Service Reform Program), serikali ilifikia uamuzi wa kuiboresha Idara ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali, ambayo ndani yake ilikuwa na Kitengo cha Msajili Mkuu.

Shughuli ya usajili wa vizazi ilipofanyika mkoani Mara hivi karibuni. PICHA: MAKTABA

Lengo lilikuwa kuboresha huduma zitolewazo na idara tajwa, ili thamani ya fedha inayotolewa na serikali, ilingane na huduma zinazotolewa.

Mchakato wa kuanzisha wakala ulianza Februari 2003 na ilipotimu Juni 23, 2006 wakala ulizinduliwa rasmi ukipewa jina la Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson, anasema uanzishwaji wa Rita imefanyika chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Sura ya 245 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Desemba 12, 2005.

Anasema kazi zote zilizokuwa zikifanywa na Idara ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali, zikiwamo za usajili wa vizazi na vifo chini ya Msajili Mkuu, sasa zinafanywa na wakala huo.

Anazitaja huduma zinazotolewa na wakala Rita kuwa ni pamoja na kusajili vizazi na vifo na kutoa vyeti vya vizazi na vifo, kutayarisha takwimu za vizazi na vifo, ndoa na talaka, kutoa leseni za kufungisha ndoa kwa viongozi wa dini na kutoa vibali maalum vya kufunga ndoa bila kutangaza siku 21.

Nyingine ni kutoa vibali ili kuruhusu ndoa ifungwe mahali maalum mfano katika hoteli, hospitali, na hata kama watahitaji kufunga ndoa mahali pengine popote zaidi ya hizo zilizotajwa.

“Wakala pia unasajili ndoa na talaka na kutoa nakala za shahada za ndoa na talaka, kutoa shahada ya kutokuwapo na pingamizi la kufunga ndoa kwa raia wa Tanzania anayetaka kufunga ndoa nje ya nchi," anasema.

Kwa upande wa huduma za udhamini, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu huyo anazitaja huduma hizo kuwa ni kusajili na kutoa hati ya usajili kwa wadhamini wa vyama vya siasa, vikundi, makanisa, misikiti na mali.

Huduma nyingine ni kusimamia mali isiyokuwa na mwenyewe au ya watu walio chini ya umri wa utu uzima (miaka 18), kusimamia mirathi na kuendesha mashauri ya mirathi, ufilisi na udhamini mahakamani, na kutayarisha na kuhifadhi wosia.

Anabainisha kuwa huduma za usajili wa vizazi, vifo na ndoa zinapatikana katika ofisi zote za wakuu wa wilaya nchini zikisimamiwa na Katibu Tawala wa Wilaya.

Anasema huduma nyingine zote zilizobaki, zinapatikana Ofisi ya makao makuu ya Rita jijini Dar es Salaam na ofisi ya Kanda ya Kati Dodoma huku wakiendelea na maandalizi ya kufungua ofisi nyingine katika kanda za kusini, kaskazini na nyanda za juu kusini.

MAFANIKIO MIAKA 4 YA JPM

Hudson anasema katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano, Rita imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kutoa huduma tajwa hapo juu kwa wananchi na wadau mbalimbali.

Anasema kuwa ili kuboresha huduma, wakala umekuwa na programu na mikakati mbalimbali kwa lengo la kupanua wigo wa wananchi kupata huduma.

Anasema katika uongozi wa Rais John Magufuli, wamekuwa na mkakati wa Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu (CRVS), uliobuniwa kwa lengo la kuongeza kasi ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu nchini ambayo ni vizazi, vifo, ndoa, talaka, watoto wa kuasili.

Anasema mkakati huo umesaidia kutoa vyeti vya kuzaliwa watoto wa umri chini ya miaka mitano, usajili ukifanywa katika ofisi za watendaji wa kata na vituo vya tiba vinavyotoa huduma za mama na mtoto, na huduma hizo zinapatikana bila malipo.

Anabainisha kuwa mikoa 12 imefikiwa kati ya 15 ambayo mpango huu unatekelezwa nchi nzima na kwa kipindi cha miaka minne, watoto 3,244,034 wamepata vyeti vya kuzaliwa, kulinganisha na watoto 800,460 waliopata vyeti katika kipindi hicho wakati wa uongozi wa serikali ya awamu ya nne.

Hudson pia anasema katika utekelezaji wa mpango wa Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri wa Miaka 5-17, utekelezaji umefanyika katika wilaya 13 katika mikoa ya Mara, Simiyu, Singida, Njombe, Shinyanga na Ruvuma na zaidi ya wanafunzi 335,583 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.

Kiongozi huyo wa Rita pia anasema wakala katika kipindi hicho cha miaka minne umeboresha mfumo wa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watu wazima kwa kuongeza matumizi ya teknolojia na uhamasishaji kwa wananchi na kwamba wananchi 433,850 wamepata huduma kupitia kampeni za uhamishaji.

"Pia kumefanyika maboresho katika sheria iliyoanzisha wakala. Hatua za kuipitia sheria zilifanyika mnano Septemba 2019, Bunge lilipopitisha marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo ambayo tayari imetiwa saini na Mheshimiwa Rais na sasa kanuni zinaandaliwa kwa ajili ya utekelezaji wa maboresho hayo.

"Maboresho yaliyofanyika yanatoa nguvu ya kisheria kwa ugatuzi wa majukumu ya usajili kwenda karibu na wananchi, waliko katika ofisi za watendaji wa kata na vituo vya tiba pamoja na matumizi ya Tehama," anasema.

Hudson anasema mafanikio mengine ni kuzinduliwa kwa Mfumo wa Usajili wa Njia ya Kielekroniki (BRS4G), kulikofanyika Juni 23, 2018.

Anasema mfumo huo umefanya mabadiliko katika miundombinu ya mifumo ya Tehama kwenye nyanja mbalimbali za utoaji huduma ikiwa ni pamoja na kuweka vifaa vya kisasa vilivyo na uwezo mkubwa zaidi wa kutunza kumbukumbu na kubadilishana taarifa na mifumo ya taasisi nyingine.

“Kwa sasa huu ndiyo mfumo mama unaotumika katika taasisi na unatumika katika ofisi zote za wilaya Tanzania Bara na ofisi ya makao makuu," anasema.

Anabainisha kuwa tayari mfumo huo umeunganishwa na mifumo ya Vitambulisho vya Taifa, Idara ya Huduma za Uhamiaji, Daftari la Mpigakura na taasisi nyingine kama Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Baraza Mitihani (Necta), Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) na wako mbioni kuunganisha na mfumo wa Tasaf.

Anasema mafanikio mengine ni kuwezesha ofisi za wilaya kutumia kompyuta, akibainisha kuwa wakati serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani ni ofisi 24 tu za wilaya 24 (asilimia 17) zilizolikuwa zinatumia kompyuta katika kuingiza taarifa na kuzalisha vyeti.

Anasema ofisi katika wilaya nyingine zote zilizobaki, zilikuwa zinatumia mashine ya 'type writer' ambayo ufanisi wake ni mdogo na haina uwezo wa kutunza kumbukumbu, lakini sasa wamesimika mifumo ya kompyuta katika wilaya zote 142.

Hudson anasema Rita pia imejiunga katika mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato ya serikali (GePG) tangu Novemba 2017, na umeiwezesha kuongeza makusanyo yake kutoka wastani wa Sh. bilioni 3.8 mwaka 2014/2015 hadi Sh. bilioni 6.8 mwaka 2018/2019, sawa na ongezeko la asilimia 178.9.

MWAMKO WOSIA

Anasema katika kipindi hicho cha miaka minne, kumekuwa na mwamko wa kuandika wosia. Anasema Rita inatoa huduma ya kuandika na kutunza wosia na kusimamia mirathi na mpaka sasa, wosia mpya zipatazo 337 zimeandikwa na kuhifadhiwa na wakala.

"Tunawashukuru wadau na taasisi na mashirika ya ndani ya nchi na ya kimataifa ambayo tunashirikiana nao katika utoaji wa huduma. Baadhi yao ni Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na Idara ya Uhamiaji. Wengine ni Unicef, Benki ya Dunia (WB), Serikali ya Canada na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu ya Tigo," anasema.

Hudson anasema Rita katika miaka minne ya serikali ya awamu ya tano imepata mafanikio makubwa katika maeneo ya kuongeza ufanisi kutoa huduma, kuunda mifumo mipya inayoondoa urasimu, matumizi ya Tehama na kuongeza makusanyo na mapato ya wakala.

“Mafanikio yaliyopatikana yameongeza imani kwa wadau wa maendeleo ambayo wameendelea kujitokeza kushirikiana na Rita katika utekelezaji wa mipango mbalimbali," anasema.

Habari Kubwa