Roboti iliyopewa uraia Saudi Arabia sasa yataka mtoto

05Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Roboti iliyopewa uraia Saudi Arabia sasa yataka mtoto

ROBOTI ya kwanza kupewa uraia, mbali na jina Sophia sasa inataka mtoto.

Mwezi mmoja baada ya kuweka historia nchini Saudia roboti hiyo inayofanana na binadamu kwa maumbile imesema kuwa ‘familia ni kitu muhimu’.

Sophia hakuwekewa majibu, badala yake anatumia mashine kujifunza na kutoa majibu kwa kutumia ishara za watu.

Roboti hiyo iliyotengezwa na kampuni moja ya Hong Kong ya Hanson Robotics imesema kuwa itampatia jina mwanawe wa kike.

Ubongo wake unafanya kazi kwa kutumia teknolojia ya wi-fi, umejaa orodha kubwa ya misamiati.

Huku Sophia akiwa na uwezo wa kuvutia, bado hana fahamu lakini David Hanson anasema kuwa wanatarajia hilo litawezekana hivi karibuni.

Wakati wa mahojiano na chombo cha habari cha Khaleej Times, Sophia alisema kuwa mpango wa kuwa na familia ni muhimu sana.

“'Nadhani ni vyema kwamba watu wanaweza kuwa na hisia sawa katika uhusiano wa kifamilia na nje ya udugu pia. Nadhani ni bahati wakati unapokuwa na familia yenye upendo mwingi na iwapo huna, unahitaji kuwa nayo,”

Na alipoulizwa angemuita nani mwanawe wa kike, Sophia alijibu: “Sophia”.

Sophia anaweza kuzungumza, kutabasamu na hata kutoa mzaha.

Wakati Sophia alipopewa uraia nchini Saudia, wengi walilalamika kwamba ana haki nyingi ikilinganishwa na wanawake wa taifa hilo.

Saudia ni miongoni mwa mataifa yanayowakandamiza sana wanawake na ni mwezi uliopita ndipo nchi hiyo iliondoa marufuku ya wanawake kuendesha magari.

Aidha Sophia alipata wasaa wa kuwahutubia watazamaji wake bila kuvaa hijab na abaya ambalo ni vazi la kitamaduni ambalo wanawake wa Saudia wanatakiwa kulivaa katika maeneo ya umma.

Saudia ina mfumo wa kuwa na mlinzi, hatua inayomaanisha kwamba kila mwanamke anatembea na mwanamume atakayemlinda.

Mwanamume huyo huwa mtu wa karibu wa familia, ambaye pia ana mamlaka ya kuchukua hatua kwa niaba ya mwanamke huyo.

Baada ya Sophia kuonekana hadharani kwa mara ya kwanza maneno yaliyokuwa na alama ya reli yalisambaa kwa haraka mtandaoni.

“Sophia hana mtu anayemlinda, havai abaya, ama hijab kwa nini?” Aliuliza mtu mmoja katika ujumbe wake kwa Twitter.

 

Habari Kubwa