RTO alipofunga safari kufurahia ‘birthday’ na yatima wa Kibaha

15Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
RTO alipofunga safari kufurahia ‘birthday’ na yatima wa Kibaha
  • Mwenye kituo afunguka alivyokianzisha, wanavyoishi

KATIKA kutetea usalama barabarani ni jambo la ushirikiano, kati ya taasisi zinazotoa elimu ya usalama barabarani na Jeshi la Polisi Tanzania Kitengo cha Usalama Barabarani na wadau wao huchukua hatua za kufanya ushirikiano.

* Watoto wanaoishi katika Kituo cha Yatima, Fadhillah, kilichopo Misugusugu, Kibaha.

Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani na mabalozi wengine, asasi ya Road Safety Ambassodor (RSA), waliungana kula chakula pamoja na watoto yatima wa kituo cha Fadhillah kilichopo Misugusugu, Wilaya ya Kibaha.

 

 

Ilikuwa na tafsiri pana, kwamba ilikuwa sehemu ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa Kamanda wa Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani (RTO) Mossi Ndozero.

 

Ni uamuzi aliyoupendekeza kufanya sherehe ndogo ya kuzaliwa kwa kujumuika na watoto hao, kwa lengo la kuwafariji watoto waliopoteza wazazi wao na sasa wako katika vituo vinavyowalea.

Hafla hiyo iliendana na kutoa zawadi aina mbalimbali kama vyakula na mafuta, pia akawapa semina elekezi kuhusu usalama wao wawapo barabarani au kwenye magari pindi wanaposafiri.

Kamanda Mossi, aliambatana na wasaidizi wake

aliwaomba wazingatie sheria na kanuni za usalama barabarani na inapotokea tatizo lolote kuhusu usalama wako wakiwa barabarani, hatua gani za kuzifuata kupata haki yako.

Alichokifanya RTO wa Pwani, ni jambo lililofufua tafsiri pana ya wazazi, kwamba haishii kwa watoto aliowazaa au anaowalea, bali hata mtu wa mbali, ambaye anaweza kujumuika naye kufurahi pamoja.

Kujumuika pamoja na watoto yatima na kuwapa semina elekezi ya usalama barabarani, ni jambo jema ambalo wengi wao suala la usalama barabarani bado hawajalifahamu vizuri.

Msingi wa neno yatima, inamwangukia mtoto aliyewapoteza wazazi wake wote wawili na vituo vya kulea watoto vinajitoa kwa hali na mali, kwa ajili ya malezi ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, huku kila siku vikiongeza idadi ya wakazi wake kutokana na uhalisia ulioko katika maisha.

VITUO VS YATIMA

Imekuwa kawaida hivi sasa takriban kila mkoa au wilaya ina idadi kubwa ya vituo vinavyotoa huduma kwa watoto wasiopata malezi ya kifamilia.

Mbali na serikali, yapo mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyoanzishwa na yanaendelea kuanzishwa kwa minajili ya kuwasaidia watoto wasiopata huduma za msingi kimalezi katika mazingira yao.

Tafsiri rasmi ya kituo cha malezi imeainishwa na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, kwamba ni nyumba, shule au taasisi inayoendeshwa na mtu au kikundi cha watu, kwa minajili ya kuwatunza watoto wanaohitaji malezi.

Sheria imebainisha sifa za mtoto anayeweza kuishi kwenye vituo hivyo. Kwanza, ni asiyekuwa na familia na asiyeweza kupata malezi sahihi katika familia yake. Kwa idhini ya Ofisa Ustawi wa Jamii, mtoto huyo anaweza kuishi kwenye vituo vya malezi.

Pili, mtoto mwenye wazazi na familia, lakini ambaye kwa maoni ya Ofisa Ustawi wa Jamii, kuishi kwenye kituo cha malezi, ni salama zaidi kuliko nyumbani kwao.

Hapo, inafahamika kuna watoto walio na wazazi wenye matatizo kama ya akili, migogoro mikubwa inayomwathiri mtoto na hata wazazi wenyewe, ambao kwa namna moja au nyingine, wamekosa uwezo wa kumlea ipasavyo.

Tatu, ni mtoto anayelengwa na mgogoro wa kisheria kati ya wazazi wake na shauri linaendelea mahakamani. Mfano, ni mtoto ambaye wazazi wametengana na kila mmoja  anahitaji kukaa naye. Katika mazingira hayo, mtoto anaweza kupelekwa kwenye kituo cha malezi, wakati shauri likiendelea mahakamani.

ALIKOZURU RTO

Msimamizi na mmiliki wa kituo cha Fadhillah, Suraiya Mohamedi, anasema kuna jumla ya watoto yatima 120, wakigawanyika kila jinsi wako 60.

Anasema, kati yao 120 wana matatizo ya kiafya na umri anaowachukua ni kuanzia mtoto mchanga hadi miaka 12, ingawa wanaozidi umri huo anakuwa nao kwa lengo la kuwaendeleza kielimu na baadhi yao hivi sasa wapo ngazi ya vyuo, ikiwamo wanaosomea ualimu.

Suraiya anasema, sababu ya kuanzisha kituo hicho ni huruma aliyoipata, alipomshuhudia aliyeanguka na kuumia sana, ndio ikawa msukumo wa kuanzisha kituo mwaka 2013, ili kuwalea watoto wenye matatizo mbalimbali.

Anajivunia manufaa yake ni kuanzisha na kuwaunganisha watoto wenye matatizo mbalimbali, amefahamiana na watu mbalimbali, pia amekuwa kiungo katika jamii.

 

Mama Suraiya anasema, awali hakikuwepo kituo cha aina hiyo jirani na anakoishi, akiangukia imani yake kwamba ni ‘Ni thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu’.

 

Anaeleza njia anazotumia ni kupitia familia zenyewe anakohisi kuna shida ya malezi ya watoto, Idara ya Ustawi wa Jamii na Jeshi la Polisi.

HALI ZAO

Wakati hivi sasa asilimia kubwa ya watoto wananufaika na maisha ya nyumbani, lipo kundi kubwa la watoto yatima zaidi ya 700,000 nchini, wakikosa uhakika wa kupata huduma za msingi.

Takwimu za msingi za elimu nchini mwaka 2016 (Best 2016) ulionyesha Tanzania ina yatima 731,536 waliopoteza mzazi mmoja au wawili, sawa na wastani wa watoto tisa kwa kila 100.

Mikoa yenye viwango vikubwa vya yatima nchini ni Iringa, yenye watoto 14 kwa kila 100 (asilimia 14.4); Njombe watoto 13 (asilimia 12.7); Mbeya kuna watoto 11 na Pwani watoto 10.

Pia, kuna mikoa inayofuatia kwa kiwango kilicho chini ya wastani wa kitaifa wa watoto tisa, vikiwa wastani wa asilimia 8.5 ni mikoa ya Manyara, Kigoma, Singida, Mtwara na Lindi.

Katika kundi hilo la wanafunzi yatima, takribani robo au asilimia 23 wamepoteza wazazi wote wawili, hivyo kutegemea zaidi msaada wa walezi au wasamaria wema.

Mbali na yatima kwa mujibu wa takwimu hizo zilizotolewa kuna wanafunzi wa elimu ya awali 125,141 ambao wamepoteza mzazi mmoja au wote wawili, huku zaidi ya theluthi mbili wakiwa ni wale wenye mzazi mmoja.

Mwanza inaongoza kwa kuwa na yatima wengi katika elimu ya awali kwa kuwa na watoto 10,848 ikilinganishwa na Katavi yenye wanafunzi yatima 1,168.

Wadau wa malezi na haki za watoto, wanaeleza kuwa yatima ni miongoni mwa makundi ya watoto walio hatarini kutengwa katika jamii na kukosa fursa muhimu katika maisha zikiwamo za kielimu, kijamii na kiafya.

WASEMALO WADAU

Asasi ya kiraia ya Save the Children, inatoa ufafanuzi nje ya utafiti kwamba, vyanzo  vya baadhi ya mikoa kuwa na yatima wengi ni umaskini, magonjwa kama ukimwi, kifua kikuu na malaria, vifo vya kinamama wakati wa kujifungua na mifarakano katika ndoa.

Japo kuna sababu nyingi za mikoa tajwa kuwa na shida nyingi, moja ya sehemu ni ya matatizo ni kiwango kikubwa cha watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kwa mujibu wa Takwimu za Utafiti wa Viashiria vya Ukimwi na malaria (THMIS), mwaka 2011/12.

Tofauti na watoto wenye wazazi wote, yatima wanakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwamo kukosekana walezi imara na wenye mapenzi kwao, jambo linalowafanya watoto wakose haki  na fursa nyingi za kujiendeleza kimaisha.

"Tafiti zinaonyesha kuwa yatima huwa na changamoto za kifedha na vikwazo vingine vya kupata elimu, hivyo huwa katika hatihati ya kukosa elimu bora, ambayo ingewapa fursa ya kujikita kwenye taaluma zinazohitaji ujuzi wa juu na kupata ajira zinazolipa zaidi,” kwa mujibu wa utafiti wa Save the Children.

Mbali na kukosa elimu, yatima wapo hatarini kupata msongo wa mawazo na matatizo ya kisaikolojia, chanzo ni kukosa malezi kamilifu, hasa kutoka kwa wasio walezi wa uhakika, hali inayowazuia kufurahia utoto wao na kuishi kwa afya.

CHANGAMOTO

Yatima wanakumbana na changamoto za ulinzi katika familia na jamii, jambo linalowasogeza kuwa waathirika wakubwa wa mimba na ndoa za utoto, zinazowaengua kutoka kwenye fursa za kimasomo.

Hata hivyo, watoto hao wanaweza kulelewa katika mazingira mazuri ambayo yatawafanya wapate fursa nyingi kama wenye wazazi wote wawili.

Kuhusu kitua cha Fadhillah, Suraiya anataja changamoto zake ni usumbufu anaopata kupitia hao vijana kama vile tabia ya utundu.

Anakiri  jamii kumpatia misaada mingi ya kuwahudumia watoto hao, ingawa bado anaomba wafadhili wazidi kujitokeza kumsaidie kutimiza lengo aliloanzisha kuwasaidia yatima hao.

Inaelezwa kitaalamu, mafanikio dhidi ya madhila kwa yatima, yanaweza kupatikana kupitia utekelezaji wa sheria, sera na miongozo inayohusu maslahi na ustawi wa watoto kama vile Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009.

Ni mambo yanayoendana na maboresho ya sheria hasa zote zinazomkandamiza mtoto, ikidokezwa na wataalamu kuhusu maeneo kama Sheria ya Ndoa nchini, bado inachangia kuwapo yatima, hasa kwa jinsia ya kike kupitia ndoa na mimba za utotoni,

Hapo ndipo inapoingia haja ya nafasi ya serikali katika ngazi mbalimbali kuchukua hatua ya kuwatambua na kuwalinda yatima, inayosaidia kupatikana takwimu za wanafunzi yatima shuleni.

Lingine linaloingia katika mtazamo huo, ni hoja ya kuanzishwa mfuko wa elimu wa kila mkoa, unaolenga kuwawezesha wanafunzi wote wanaosoma katika mazingira magumu hususan yatima.

 

Pia, katika upande wa pili inabeba umuhimu wa uwezeshaji watoto wanaoishi mazingira magumu, kupitia chombo kama mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Malezi ya yatima ni mtambuka na yanahusisha taasisi na watu mbalimbali. Jambo linalosisitizwa ni kutimiza haki zao za msingi, ekimu ikiwa mojawapo.

 

Mwandishi ni mwalimu kitaaluma anapatikana kwa simu. (+255) 0717 314 100

Habari Kubwa