Rushwa inavyokwamisha wanawake Zanzibar kuwania nafasi za uongozi

23Oct 2019
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Rushwa inavyokwamisha wanawake Zanzibar kuwania nafasi za uongozi

INAPOFIKIA kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, wanawake wengi hujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika majimbo ya uchaguzi kupitia vyama vyao vya siasa.

Wananchi Zanzibar wakipiga kura kwenye uchaguzi wa mwaka 2015. PICHA: MTANDAO

Hata hivyo, wengi wao hushindwa kupata nafasi hizo kutokana na jamii kutawaliwa na rushwa.

Kutokana na uwezo mdogo wa kipato walionao wanawake, rushwa imekuwa ni kikwazo kwao kupata nafasi za uongozi katika majimbo ya uchaguzi.

Ili kuwa kiongozi kupitia jimbo lazima kwanza uteuliwe na chama cha siasa kuwa mgombea na wananchi wakupigie kura ndipo uwe mbunge, mwakilishi au diwani kwa upande wa kata/shahia kwa Zanzibar.

MGOMBEA

Khuzaima Bakari ni mwanamke ambaye alishagombea nafasi ya uwakilishi kwa vipindi vitatu mfululizo kwenye chaguzi zilizopita lakini anasema amekosa nafasi hiyo kutokana na rushwa inavyotawala hasa katika kipindi cha uchaguzi.

“Rushwa inaanzia kwenye vyama vya siasa hadi katika jamii, maana wanawake tumekuwa tukidaiwa rushwa aidha ya fedha au ngono ili chama kiweze kukusimamisha kuwa mgombea na jamii iweze kukuchagua,” anasema.

Anabainisha wanawake hawana uwezo wa kifedha, hivyo wanapojitokeza kugombea majimboni kuna mfumo umewekwa, kwamba ukitaka kupita katika kura za maoni, ni kutoa rushwa na wanawake hawana fedha za kutosha.

Anabainisha kwamba wanawake wanakabiliwa na rushwa za aina mbili ambazo ni rushwa ya fedha ama ya ngono na kwa kuwa hawana uwezo wa kutosha wa kifedha wa kutoa rushwa na hawapo tayari kutoa rushwa ya ngono, ndiyo sababu wanashindwa kupata nafasi za uongozi majimboni.

“Wakati mwingine hata hufikii hatua ya kuwa mgombea, jina linakatwa katika mchakato wa kura za maoni ndani ya vyama vya siasa...hali hii haipo kwangu tu, bali inawakabili wanawake wengi Zanzibar," anasema.

WANANCHI MJINI NA VIJIJINI

Bahati Issa ni mkazi wa Kikungwi Kusini Unguja, anasema wanawake wanakosa nafasi za uongozi kutokana na rushwa na hivi sasa wamekuwa na hofu ya kugombea kwa sababu ya kushamiri kwa vitendo hivyo.

Anabainisha wapo wanawake wenye uwezo wa kuwa viongozi, lakini wanakosa nafasi kutokana na kudaiwa rushwa na kwa kuwa hawako tayari kuitoa, ndoto zao huishia hapo.

“Chaguzi zilizopita rushwa ilitawala, sasa tukiwa tunaelekea kwenye chaguzi zijazo, tunaviomba vyama vyote vya siasa na serikali kulisimamia hili, kwani sisi wanawake tuna hamu ya kugombea,” anasema.

TATU OTHMAN

Tatu Othman ambaye ni mkazi wa Magomeni, Mjini Unguja, ambaye ana ulemavu wa uoni anasema wanawake wanashindwa kugombea nafasi za uongozi kwa sababu hawana fedha.

“Tunashindwa kusonga mbele katika harakati za kugombea si kama hatutaki…tunataka na tunapenda, lakini hatuna fedha na unapoenda kuomba nafasi na kuulizwa kama una fedha, unaanza kuvunjika moyo,” anasema.

Kwa upande wake, Zaituni Bahorera, mkazi wa Kijiji cha Makunduchi, anasema kikwazo kikubwa cha wanawake kushindwa kugombea nafasi za uongozi ni rushwa kwani wapo wanawake wenye elimu nzuri ambao wakipewa nafasi wanaweza kuleta maendeleo, lakini rushwa ndiyo inawafanya washindwe kufikia ndoto zao katika uongozi.

Anabainisha idadi ya wanawake walio katika katika vyombo vya kutunga sheria wanaotoka majimboni ni ndogo, ikilinganishwa na wanaume.

“Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) katika uchaguzi wa mwaka 2015, kilitoa elimu kwa wanawake kugombea nafasi za uongozi, elimu ambayo ilitufikia hadi sisi vijijini, cha kushangaza ni wanawake watano tu ndio waliopata nafasi ya uwakilishi kupitia majimboni,” anasema.

Anabainisha baada ya kutolewa elimu hiyo, wanawake zaidi ya 50 walijitokeza kugombea nafasi za uongozi kupitia vyama mbalimbali vya siasa, lakini ni wanawake watano tu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndio waliopata nafasi hizo.

OMAR

Hassan Omar, Mkazi wa Kijiji cha Kizimkazi, anasema kuwa wapo wanawake wenye uwezo mzuri wa kuwa viongozi lakini wanakosa nafasi hizo kutokana na uwepo wa rushwa katika jamii.

“Asilimia kubwa ya watu wanaoingia katika uongozi hasa wanaume, wako kwa ajili ya maslahi yao binafsi na ndio maana, wanawake wanakosa nafasi za uongozi,” anasema.

Kingine anachotaja kukosesha wanawake nafasi za uongozi ni kitendo cha wanaume walio wengi kupeana nafasi za uongozi ili maovu yao yasiweze kutambulika.

Anawaasa wanawake kutovunjika moyo, bali wapambane ili kutimiza ndoto zao za kuwa viongozi na kuiletea nchi maendeleo.

"Naamini unapompa nafasi ya uongozi mwanamke ni rahisi zaidi kuleta maendeleo kwa sababu wanawake si watu wa kupokea rushwa kirahisi kama tulivyo sisi wanaume," anaongeza.

TAMWA

Hawra Shamte, Meneja wa Sera na Utetezi kutoka TAMWA Zanzibar anaitaka jamii ifahamu kuwa rushwa ni adui wa haki na wanawake wana haki ya kugombea nafasi za uongozi.

Anasema wanawake kugombea nafasi za uongozi iwe urais, ubunge, uwakilishi au udiwani ni haki yao ya kikatiba na wala hawastahili kutoa rushwa.

“Rushwa ni vita ngumu mno kweli kwa wanawake na hasa wanapotaka nafasi za uongozi, hukabiliwa na rushwa ama ya fedha au ya ngono na ni ngumu kwao kutoa rushwa,” anasema.

Anaitaka jamii kuwapa fursa wanawake ya kugombea nafasi za uongozi na kuachana na masuala ya rushwa kwa sababu kiongozi anayetokana na rushwa hataweza kuwaletea maendeleo.

Aidha, anazishauri mamlaka za kuzuia rushwa kuweka mitego, kuwafuata wanasiasa kuzungumza nao kuhusiana na rushwa kwa sababu wengine wanaona ni jambo la kawaida kuombwa pesa, wakatoa.

Aliitaka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa Zanzibar (ZAECA) kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na rushwa hasa wakati huu wa kuelekea chaguzi, kwani rushwa inaanzia ndani ya vyama katika vikao vya uteuzi wa wagombea.

NAIBU SPIKA

Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma, anasema ni kweli kilio kikubwa cha wanawake katika kugombea nafasi ya uongozi ni rushwa ya fedha na ngono.

Anabainisha ni lazima wanawake kupaza sauti kukemea rushwa kuanzia ndani ya vyama vya siasa hadi katika jamii, kwani zimekuwa zikiwarudisha nyuma.

Mgeni anasema, wanawake si kwamba wanataka uongozi kwa kujionyesha bali kuna mambo wanataka kuyasema na kuyasimamia.

“Tumekaa kimya muda mrefu na mambo mengi tumekosa...tunafahamu nyumba nyingi maskini zinazoendeshwa na wanawake...sisi ndio tunaotupiwa watoto, tunaoingia leba...sasa nani ataiambia serikali kwamba tunataka hospitali zenye huduma bora, vifaa ili kupunguza vifo vya mama na watoto?” Anahoji na kuongeza:

“Hayo yote hayataweza kupatikana kama wanawake hatutapaza sauti zetu na kama hatutogombea nafasi za uongozi."

ZAECA

Kwa upande wake Makame Khamis Hassan ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi na Operesheni wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa Zanzibar (ZAECA), anasema matukio ya rushwa katika maandalizi ya uchaguzi yamekuwa yakitokea katika hali tofauti, hasa ikizingatiwa kuwa uchaguzi unapita katika hatua mbalimbali.

Anasema hatua ambayo ZAECA inapokea malalamiko mengi ya tuhuma za vitendo vya rushwa ni ya kampeni za wagombea ndani ya vyama.

Anabainisha kuwa malalamiko ya tuhuma za vitendo vya rushwa waliyopokea katika uchaguzi wa mwaka 2015 pamoja na ule wa marudio wa mwaka 2016 yalihusisha wagombea wa kiume kutoka vyama mbalimbali vya siasa.

“Hatuna malalamiko ya tuhuma za rushwa zilizowahusisha wagombea wanawake, sijui labda kwa sababu ya uchache wa wagombea wanawake ikilinganishwa na wanaume,” anasema.

Anawataka wanawake ambao wanakumbana na vikwazo vya rushwa katika kugombea nafasi za uongozi kuripoti katika mamlaka hiyo ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Kaimu mkurugenzi huyo aliitaka jamii kufahamu kuwa inapochagua kiongozi ambaye ametoa rushwa isitarajie manufaa au maendeleo kutoka kwake kwa sababu atataka fedha alizowapa anazirejesha.

Anasema kuelekea katika uchaguzi mkuu mwakani, ZAECA imejiandaa kuhakikisha vitendo vya rushwa vinapungua na viongozi wanaingia madarakani kihalali.

MSEMAJI MKUU WA SMZ

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, anasema vitendo vinayoambatana na masuala ya rushwa na uhujumu uchumi, kamwe haviwezi kuvumilika mahali popote pale iwe ndani na hata katika uga wa kimataifa.

Anabainisha wapo baadhi ya watendaji na watumishi wa umma wasio waaminifu wanaendelea kuhujumu uchumi kwa kupokea rushwa na kuisababishia serikali hasara au wananchi wake kuwaweka katika mazingira magumu pale wanapohitaji huduma za kijamii.

Balozi Iddi anasema zipo tuhuma za uhujumu uchumi na upokeaji rushwa zipatazo 108, ambapo upelelezi wake haujakamilika zilizoripotiwa katika ZAECA kufikia mwaka 2018.

Anazitaka taasisi zinazohusika na ufuatiliaji wa masuala ya rushwa na uhujumu uchumi kisheria kuondoa muhali na kuharakisha upelelezi wake ili wahusika wafikishwe katika vyombo vya sheria ili haki ichukuwe mkondo wake.

HISTORIA

Hivi sasa idadi ya wanawake wanaowania nafasi mbalimbali wakati wa uchaguzi duniani imechochea uwepo wa usawa wa jinsia katika mabunge.

Rwanda ni miongoni mwa nchi 10 zenye zaidi ya asilimia 40 ya wabunge wanawake, jambo ambalo linawezekana kabisa kwa Zanzibar, kuwa na viongozi wanawake kwenye Baraza la Wawakilishi ambapo hivi kati ya majimbo 54, ni majimbo matano tu ndiyo yanayoshikiliwa na wanawake kwa uwakilishi na majimbo matatu kwa ubunge kwenye Bunge la Taifa.

Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2003 nchini Rwanda, yameruhusu asilimia 30 ya viti kuwa vya wanawake bungeni, na tangu wakati huo wanawake wamekuwa wakijitokeza katika chaguzi mbalimbali.

Mabadiliko hayo yalikuja baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ambapo watu 800,000 walipoteza maisha, hali iliyosababisha wanawake kulazimika kufanya majukumu mbalimbali ili kuijenga upya nchi yao.

Rwanda hivi sasa ni moja kati ya nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi barani Afrika.

Habari Kubwa