Sababu 5 kwa nini Djuma haiwezi Simba

24Sep 2018
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Sababu 5 kwa nini Djuma haiwezi Simba

BAADA ya Simba kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Ndanda mjini Mtwara na pia kufungwa bao 1-0 dhidi ya Mbao FC, wanachama na mashabiki wa Simba wameonekana kucharuka.

Mrundi Masoud Djuma.

Wengi wanataka kocha Mbelgiji Patrick Aussems atimuliwe na nafasi yake ichukuliwa na Mrundi Masoud Djuma.

Wanachama na mashabiki wa Simba wanaamini kuwa Masoud ana uwezo mkubwa wa kuifundisha timu yao kutokana na kupenda kutumia mfumo wa 3-5-2 ambao ni wa kushambulia zaidi na aliwahi kufanya hivyo kwenye baadhi ya mechi za ligi msimu uliopita na ndiyo nyota anayotembelea nayo hadi leo.

Hata hivyo, wapo ambao wana maswali ambayo wanajiuliza ni kwa nini  makocha watatu wote waonekane hawafai na kumlalamikia yeye kuwa anawahujumu?

Ikumbuwe wakati Masoud akiwa msaidizi kwa muda mfupi tu Simba imefukuza makocha wawili ambao ni Mcameroon Joseph Omog na Mfaransa Pierre Lechatre walioonekana hawafai.

Muda mfupi tu tangu Aussems aanze kuifundisha, tayari ameshaanza kuonekana hafai, kitu ambacho baadhi wajiulize, inawezekana vipi makocha wote ambao Simba inawachukua wawe hawafai?

Kuna wanachama na mashabiki ambao wanataka apewe timu awe kocha mkuu na timu itafanya vizuri.

Hata hivyo, kuna sababu tano ambazo zinamfanya Masoud asiweze kuifanya Simba kuwika kama ambavyo wanadhani...

 

1. Umri mdogo, klabu kubwa

Kwa klabu kama ya Simba ambayo ni kubwa si kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati bali miongoni mwa kubwa Afrika, umri wa Masoud bado hauwezi kuwa mtu wa kukabidhiwa timu.

Ikumbukwe kuwa Simba ina wachezaji wengi maarufu, mastaa, wenye majina makubwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo inatakiwa iwe na kocha si mwenye umri mkubwa tu bali mwenye wasifu mkubwa na aliyefundisha klabu maarufu na kubwa na wachezaji wakubwa zaidi ili wamheshimu.

Ikumbukwe mchezaji akitoka mikoani na hana jina, akisajiliwa na klabu hiyo tu hata kama hakuna lolote aliloifanyia timu, tayari na yeye anajiona staa na anaweza kuwa jeuri, hivyo kocha kama Masoud hana uwezo wa kuwadhibiti na kumheshimu kama wakiamua.

Kumbuka kwenye Kombe la Mapinduzi mwanzoni mwa mwaka huu, wachezaji Shiza Kichuya na Jonas Mkude walivyomkasirikia baada ya kuwatoa kwenye mechi moja mjini Zanzibar kiasi cha kususa hata kukaa kwenye benchi, wasingeweza kufanya hivyo kwa kocha mwenye wasifu mkubwa.

 

2. Urafiki uliopitiliza na wachezaji

Kutokana na umri wake kuwa unakaribiana na wachezaji wengi wa Simba, amejenga urafiki na wachezaji wengi ambao si vibaya, lakini kama akiwa kocha mkuu unaweza kumletea matatizo pale atakapokuwa yeye ndiye mwamuzi wa mwisho.

Wachezaji hasa wa Kitanzania wanaeleweka kwa tabia ya kutopenda mazoezi magumu, na uchunguzi unaonyesha ukiona wachezaji wanampenda sana kocha basi ujue wanammudu, hivyo wana uwezo wa kumwambia mazoezi haya yanatosha na wakasikilizwa. Kocha hatakiwi kuwa na urafiki uliopitiliza na baadhi ya wachezaji kwa sababu kuna wakati hatofanya kazi yake vema, hilo tu linamnyima sifa.

 

3. Alishindwa Mapinduzi, SportPesa na Kagame Cup

Tayari Masoud ameiongoza Simba kwenye michuano mitatu mwaka huu na haikupata hata kombe moja.

Alikuwa peke yake kwenye mechi za Kombe la Mapinduzi na ndipo alipoanza kuufanyia kazi mfumo wake wa 3-5-2 uliowashinda wachezaji wengi wa Simba na kuanza kumnunia, huku wanachama na mashabiki hao hao wakimshutumu kwa mfumo mgumu ingawa baadaye ulizoeleka, lakini Simba ilitolewa na Azam.

Alikwenda nchini Kenya kwenye Kombe la SportPesa akiwa kaimu Kocha Mkuu, Simba haikuambulia kitu ikafungwa mabao 2-0 dhidi ya Gor Mahia na hata aliposimama kwenye Kombe la Kagame, bado Simba haikupata taji hata moja. Ikafungwa mabao 2-0 dhidi ya Azam.

 

4. Hana uzoefu mechi za Kimataifa

Bado wanachama na mashabiki wengi hawajui kwa nini viongozi wa klabu hiyo wanaleta makocha kutoka nje ya nchi kwa ajili ya klabu hiyo.  Akili yao inalenga zaidi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa zaidi na si Ligi Kuu Tanzania Bara.

Inawezekana Masoud akawa anaweza kuiongoza Simba kushinda baadhi ya mechi za ligi, lakini linapokuja suala la mechi za kimataifa inahitajika kocha ambaye ana uzoefu zaidi na michuano hiyo na amezifundisha timu kubwa zilizofanya vema kwenye michuano hiyo hiyo. Masoud yeye amezifundisha timu za Rayon Sport na APR za Rwanda ambazo hazikufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

 

5. Mfumo wake ni hatari kimataifa

Mfumo ambao unaonekana kupendwa na mashabiki wengi wa Simba wa 3-5-2 ni mzuri timu kama hiyo ikicheza na timu dhaifu kwa sababu itakuwa ikishambulia mfululizo, huku ikijibiwa na mashambulizi dhaifu kutoka kwa wapinzani.

Kwenye michuano ya kimataifa ni hatari kutumia mfumo huo kwa sababu timu inakutana na timu bora na zenye uwezo wa hali ya juu na kubadilisha mfumo kutokana na mpinzani, hivyo mabeki watatu nyuma hawawezi kuhimili mashambulizi, wataruhusu mabao kiurahisi.

Mfano nzuri mechi ya Kombe la Mapinduzi mjini Zanzibar, Simba ilikuwa ikiruhusu mabao kirahisi wakati wapinzani walipokuwa wakijibu mashambulizi na kukutana na ukuta dhaifu wa mabeki watatu, hivyo kutolewa kwenye michuano hiyo.

Kumbuka Simba ilivyocheza dhidi ya Asante Kotoko na kukutana na mastraika hatari na mawinga wasumbufu, lakini angalau mfumo wa Aussems ulisaidia ikatoka sare, laiti kama ule wa mabeki watatu nyuma ungetumika, ingekuwa hatari mno siku ile ya Simba Day.

Habari Kubwa