Sababu 5 sare Simba, Yanga Ligi ya Mabingwa

12Aug 2019
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Sababu 5 sare Simba, Yanga Ligi ya Mabingwa

SARE tatu za mechi za kimataifa kwa timu za Tanzania zilipatikana siku ya Jumamosi kwenye viwanja na nchi mbalimbali.

Beki wa Yanga, Paul Godfrey akipiga hesabu ya kuwazuia wachezaji watatu wa Township Rollers kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopigwa Uwanja wa Taifa Jumamosi.

Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba wakiwa nchini Msumbiji kwenye mji wa Beira, walitoka suluhu ya bila kufungana na UD Songo katika pambano kali la aina yake la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga ikiwa mbele ya mashabiki wake, ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Township Rollers ya nchini Botswana kwenye mechi nyingine ya Ligi ya Mabingwa.

Timu mpya kabisa iliyopanda daraja na kuanza kucheza Ligi Kuu msimu uliopita, KMC, ilifanya maajabu baada ya kutoka sare dhidi ya AS Kigali,  si tu ikicheza kwa mara ya kwanza michuano ya kimataifa, lakini pia ikicheza ugenini.

Kwa matokeo hayo ni kwamba timu hizo tatu zinahitaji matokeo chanya kwenye mechi za marudiano zitakazofanyika wiki mbili zijazo.

Yanga ndiyo itakuwa na kazi kubwa kwa sababu italazimika kwenda kupambana ugenini nchini Botswana, wakati Simba itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, ambao mara nyingi si salama kwa timu ngeni zinapofika hapo.

KMC pia ina nafasi kubwa ya kusonga mbele kwani suluhu iliyoipata ugenini imeipa moyo na kiburi cha kupambana ikiwa kwenye ardhi ya nyumbani.

"Tumefanya kitu kizuri kutoruhusu bao. Pamoja na juhudi kubwa za wapinzani, lakini wachezaji wangu walikaa imara, tutajiandaa kwa ajili ya mchezo wa marudiano. Mchezo wetu wa marudiano tuna nafasi ya kufanya vizuri, tunaomba mashabiki wetu watupe sapoti," alisema Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems.

"Kwa sasa hesabu ni kwamba tutakuwa na kikosi imara ambacho kitapata matokeo kwenye mchezo wetu wa marudiano, mashabiki waendelee kutupa sapoti katika hili, nami nitafanyia kazi makosa yote," Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera naye anaongeza maneno hayo.

Kwa jicho la mchambuzi wa makala haya, hizi ndizo sababu zilizofanya timu hizo kupata sare kwenye mechi hizo za mkondo wa kwanza.

1. Simba, Yanga hazina muunganiko

Bado timu za Simba na Yanga hazina muunganiko kutokana na kuwa na baadhi ya wachezaji wageni.

Yanga ndiyo iliyoongoza kwa kuchezesha wachezaji wengi wageni, tofauti na wale waliokuwa kwenye kikosi hicho msimu uliopita. Ni wachezaji wawili wa zamani tu ambao walianza mechi hiyo ambao ni Paul Godfrey na Papy Tshishimbi pekee, huku Mrisho Ngassa akiingia kipindi cha pili.

Hata Kocha Mkuu wa Yanga, Zahera amekiri hilo na kusema kuwa wachezaji wake bado wana tatizo la kushindwa kuelewana wakiwa ndani ya uwanja jambo ambalo linaleta ugumu kupata matokeo uwanjani.

Simba nayo iliathiriwa na hali hiyo, ingawa si sana kwa sababu Aussems alijitahidi sana kutopanga wachezaji wengi wageni na badala yake akaziba mapengo ya wachezaji ambao wameondoka.

Wachezaji wapya ambao Simba iliwapanga kwenye mechi hiyo ni Benno Kakolanya na hii ni kwa sababu Aishi Manula ni majeruhi, wengine wakiwa na Gadiel Michael, Sharaf Eldin Shiboub, Francis Kahata, na baadaye aliingia Deo Kanda.

 

2. Michuano kuanza kabla ya Ligi Kuu

Michuano ya Ligi ya Mabingwa pamoja na Shirikisho barani Afrika kuanza kabla ya Ligi Kuu Tanzania Bara haijaanza nayo imekuwa ni majanga, kwani imesababisha timu za Simba na Yanga kutokuwa kwenye muunganiko na wachezaji kuwa bado hawajaelewana.

Kocha wa Simba alishawahi kulalamika kuwa walishtukizwa na ratiba hiyo kwani walitegemea kuwa wangeanzia kwenye raundi ya kwanza na si ya awali.

Hii ina maana kuwa bado alikuwa hawajajiandaa na michuano hiyo, lakini kwa sababu imekuja kwa kushtukiza, akabadili aina ya mazoezi ili mradi kuendana na matakwa ya mechi za awali.

Kwa jinsi timu hizo zilivyo, kama zingeanza na mechi za Ligi Kuu angalau tatu ama nne, halafu ziende kwenye mechi za kimataifa, tungeweza kushuhudia timu zote mbili zikitinga hatua inayofuata kirahisi.

3. Zahera kuchelewa kurudi

Yanga pamoja na kuonekana ina baadhi ya wachezaji wapya wenye uwezo mkubwa, lakini bado inaathiriwa na vitu vingi vya kiufundi na hii inasababishwa na Kocha Mkuu, Zahera kuchelewa kurejea kutoka kwenye mapumziko.

Zahera alirejea wiki moja tu kabla ya Yanga kuanza michuano hiyo, na ingawa si viongozi wa Yanga wala mashabiki wao waliokemea jambo hilo, lakini hili limeigharimu sana timu hiyo kwenye mechi hiyo. Na hata kama itatolewa kwenye michuano hiyo, Zahera ni lazima abebe lawama hiyo na wala si wachezaji wake.

4. Simba kuanza kuheshimu wapinzani

Simba imepata sare kwa mara ya kwanza ugenini na hii ni tofauti na msimu uliopita. Kwenye Ligi ya Mabingwa msimu uliopita ilipata ushindi kwenye mechi moja tu dhidi ya Mbabane Swallow ya Eswatini zamani ikiitwa Swaziland, huku ikipokea vichapo kwenye mechi zingine zote za ugenini.

Kocha wa Simba anaonekana safari hii amebadilisha mbinu na kucheza mfumo wa kujilinda zaidi timu inapokuwa ugenini kuliko kushambulia zaidi ambapo huwapa mwanya wapinzani.

Kwenye mechi dhidi ya UD Songo, Simba ilionekana kutafuta zaidi sare kwani ilishambulia mara chache na kujilinda zaidi.

5. KMC ilicheza sehemu ilipopazoea

Mwezi mmoja tu uliopita, timu ya KMC ilikuwa nchini Rwanda kwenye michuano ya Kombe la Kagame. Michuano hiyo iliyoanza Julai 6 hadi 19, si tu kwamba iliifanya KMC inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni kupata angalau uzoefu kidogo, lakini pia kuizoea nchi ya Rwanda, hasa Kigali kiasi kwamba hata ilipopangiwa dhidi ya AS Kigali haikuhofu sana kwa sababu ni sehemu ambayo wanaifahamu.

Ndiyo maana hata mechi yenyewe KMC ilicheza soka safi bila hofu kwa sababu tayari walikuwa wameshaizoea nchi hiyo kwa kila kitu kiasi cha kuwapa tabu wapinzani wao.

Habari Kubwa