Sababu 5 Simba, Yanga kupishana na mil. 70/-

28Jan 2019
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Sababu 5 Simba, Yanga kupishana na mil. 70/-

KWA mara ya tatu mfululizo timu za Tanzania zimekuwa wasindikizaji kwenye michuano ya SportPesa.

Kipa wa Simba, Aishi Manula, akidaka mpira wakati wa mechi ya nusu fainali dhidi ya Bandari FC ya Kenya, ambayo walichapwa 2-1

Michuano hiyo huzishikirisha timu za Tanzania na Kenya, lakini inaonekana Kenya imeendelea kutawala michuano hiyo, baada ya timu za Simba, Yanga, Mbao FC na Singida United kusukumizwa nje ya michuano hiyo.

Tangu mwaka 2017, michuano hiyo ilipoanzishwa, hakuna timu yoyote ya Bongo iliyotwaa ubingwa na hata mwaka huu kombe hilo limerudi tena nchini Kenya kufuatia Bandari na Kariobangi Sharks kupepetana fainali jana.

Timu za Bongo zimeshindwa kabisa kutwaa kiasi cha Dola za Marekani 30,000 sawa na Sh, milioni 69.2 za Tanzania kwa mechi tatu tu, huku Ligi Kuu ya Tanzania inayokadiriwa kuwa na kiasi hicho cha pesa kwa bingwa ikicheza mechi 38, pia mpaka sasa kukiwa hakuna uhakika wa kupata pesa hizo kwa kukosekana mdhamini.

Mwaka 2017 michuano hiyo ilifanyika nchini Tanzania na Gor Mahia ikatwaa kombe hilo kwa kuwachapa mahasimu wao wa jadi AFC Leopards mabao 3-0 kwenye mechi ya fainali.

Kwenye michuano hiyo Simba ilitolewa hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya Nakuru All Stars ya Kenya, huku Yanga ikitolewa nusu fainali pia kwa mikwaju ya penalti 4-2, habari ikaishia hapo.

Mwaka uliofuata 2018 ilifanyika nchini Kenya na kwa mara nyingine tena Gor Mahia ilitwaa ubingwa kwa kuichapa Simba mabao 2-0 yaliyofungwa na Meddie Kagere ambaye kwa sasa anaichezea timu hiyo aliyoifunga na Jacques Tuyisenge.

Yanga iliyaaga mashindano hayo mapema ilipopigwa mabao 3-1 na Kakamega Home Boyz, Singida ikapigwa na Gor Mahia mabao 2-0.

Mwaka huu mambo ni yale yale. Safari ya Simba iliishia kwa Bandari hatua ya nusu fainali ikapigwa mabao 2-1, wakati huo Yanga ilishaondolewa mapema tu kwa mabao 3-2 dhidi ya Kariobangi Sharks, Singida United nayo ikitoka mapema, Mbao FC baada ya kuweka rekodi ya kuwatoa mabingwa mara mbili Gor Mahia, ikaondolewa kwa mikwaju ya penalti nusu fainali dhidi ya Kariobangi.

Cha kujiuliza ni mkosi gani kwa timu za Tanzania kushindwa kutwaa kombe hilo kwa miaka mitatu mfululizo?

Hizi ni sababu tano zinazosababisha timu za Bongo kuwa nyanya kwenye michuano hiyo...

 

Ligi dhaifu ya Tanzania.

Ligi ya Tanzania ina kelele nyingi za vyombo vya habari na pesa, huku ikiwa na mashabiki wengi wanaoifuatilia, lakini haina mvuto na wala si bora. Ni dhaifu kwa maana halisi ya udhaifu.

Ratiba mbovu isiyoeleweka. Kuna baadhi ya timu hazina kabisa wazo la kuusaka ubingwa, badala yake zinatafuta pointi kwa ajili ya kubaki Ligi Kuu tu. Timu zinazoonekana kuusaka ubingwa kwa maneno na vitendo ni Simba, Yanga na Azam tu, zingine zote ni wasindikizaji. Hapa huwezi kupata ligi bora.

Kuwapo kwa waamuzi wabovu, waamuzi wenye maamuzi yanayotia shaka, upendeleo, rushwa, kuwapo kwa tetesi za baadhi ya viongozi kununua mechi, baadhi ya wachezaji wa timu kupokea pesa kwa ajili ya kuziachia timu zingine ushindi, haya yote yanasababisha timu za Tanzania zishindwe kupata ushindi zinapokwenda kucheza mechi halisi, zenye waamuzi bora na timu bora zenye wachezaji wanaojitambua.

 

Wachezaji kuchagua mechi

Sifa zilizopitiliza za kwenye magazeti ya michezo, mitandao ya kijamii na kwenye vijiwe wanazopewa wachezaji wa Kibongo mara nyingi zinawavimbisha kichwa na kuona wao ni zaidi kuliko wachezaji wa timu nyingine.

Matokeo yake wachezaji wanacheza wanapojisikia. Wanaamua ni mechi gani ya kucheza kwa bidii na nyingine wanacheza kama wako kwenye mazoezi. Wanachagua michuano ya kucheza, mingine wanaiona kama vile haina maana. Hawaitilii maanani. Kisa wao ni mastaa. Hii inawafanya washindwe kucheza vema wanapokutana na timu zenye wachezaji wanaojitambua na kujituma kisawasawa kama tunavyozishuhudia kwenye SportPesa Cup.

 

Kukosa nguvu

Ukiondoa timu ya Mbao FC, timu zilizobaki za Tanzania pia zinatatizwa na wachezaji wao kutokuwa na nguvu au stamina za kutosha wanapopambana na timu za Kenya ambazo msingi wao namba moja wa soka ni nguvu.

Wachezaji wa Tanzania wanapata tabu sana wanapokutana na timu ambazo hutumia zaidi nguvu.

Ukiangalia ni wachezaji wachache sana hasa wanaotoka nje ya nchi ndiyo utaona wana stamina, lakini wengi wao hutegemea vipaji vyao tu, hivyo timu za Kenya hutumia udhaifu huo kuziadhibu timu za Tanzania ambazo huwaambukiza hata wachezaji wa kigeni aina yao ya uchezaji.

Ni Mbao pekee inayoonekana kuwa na wachezaji wanaotumia nguvu na ndiyo maana waliwatoa Gor Mahia na hata kutolewa wametoka kwa mikwaju ya penalti kwa sababu walifanana na timu za Kenya.

 

Wachezaji hawajitumi, hawapambani

Ukiangalia timu za Tanzania utakuta kuna baadhi ya wachezaji hawatekelezi majukumu yao.

Ukiziangalia timu za Kenya na hata Mbao FC, utakutana na aina fulani ya soka la upambanaji na kujituma. Kila mchezaji anamsaidia mwenzake na kufika kwenye eneo kwa wakati husika. Yaani wanacheza kitimu zaidi.

 

Soka lisilo na malengo

Timu za Kenya pamoja na kwamba wachezaji wake wanaonekana hawana vipaji vikubwa, lakini wanacheza kwa malengo.

Wanapocheza unaona kuna kitu wanatafuta. Kuna wakati wanacheza pasi fupi fupi na wakati mwingine pasi ndefu kutokana na mechi jinsi inavyoendelea. Timu za Tanzania zinaonekana kama vile zinafanya shoo ya kucheza soka uwanjani na si kutafuta ushindi kwa hali na mali, tofauti na wenzake Wakenya ambao pamoja na kwamba wanaonekana kupata nafasi chache, lakini wanakuwa nazo makini na kuzitumia.

 

 

 

 

 

Habari Kubwa