Safari ya ajabu angani yenye mafanikio

19Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Safari ya ajabu angani yenye mafanikio

KATIKA mpango wa kuanzisha safari za kibiashara kwenda anga za mbali, Shirika la Nasa, limejaribu chombo chake kitakachotumika kwa safari hizo kwa mafanikio.

Chombo kinachosafiri kwenda katika anga nyingine. PICHA: MTANDAO.

‘Crew Dragon’ chombo cha kubeba watu kwenda anga za mbali kilichotengenezwa na Shirika la Kimarekani la ‘SpaceX’ kwa ajili ya Shirika la ‘Nasa’ kimerudi duniani kutoka kituo cha kimataifa cha anga.

Katika taarifa iliyotolewa na Nasa kuwa ni ya jaribio, chombo hicho kilichorushwa kwenda kituo cha kimataifa cha anga, kimerejea duniani na kutua katika bahari ya Atlantiki kilomita 450 kutoka jimbo la Florida.

Chombo hicho kiligusa anga la dunia saa moja na dakika 52 na kugusa uso wa bahari saa mbili na dakika 45 katika eneo hilo.

Nasa katika mpango wake wa kuanzisha safari za kibiashara, mnamo Machi 2 mwaka huu, ilirusha chombo kilichobuniwa kwa ajili ya kubeba watu kwenda kituo cha kimataifa cha anga.

Siku inayofauta, Machi 3, chombo hicho kiliwasili kituoni hapo na kukaa katika kituo hicho cha angani kwa muda wa siku sita.

Baada ya mafanikio hayo ya jaribio la safari iliyofanyika bila kuwa na watu jaribio la safari itakayokuwa na watu wawili, wanajimu wa Nasa kwenda kituo cha kimataifa cha anga, litafanyika mwezi Julai, mwaka huu.

Katika taarifa nyingine chombo cha shirika la Boeing kijulikanacho ‘Starliner’ kinatarajiwa kujaribu safari ya bila watu mwezi ujao na iwapo litafanikiwa katika jaribio hilo, itafanya jaribio litakalokuwa na watu, mwezi Agosti mwaka huu.

•Kwa mujibu wa TRT.

Habari Kubwa