SAIDI OMAR SAID: Fundi mekanika aliyeunda  helikopta ya abiria 5 Z’bar

12Jan 2018
Rahma Suleiman
Nipashe
SAIDI OMAR SAID: Fundi mekanika aliyeunda  helikopta ya abiria 5 Z’bar
  • Aiteka hadhira Maonyesho ya Biashara Maisara
  •  Chombo chake kinasafiri Unguja - Dar kwa nusu saa
  • Ajigamba kuwa mara ya 3 kuushangaza umma 

IJUMAA iliyopita katika gazeti hili ilikuwa na makala inayomhusu Mhindi Amol Yadav (41), aliyebuni na kuunda ndege yake, kazi iliyomchukua miaka saba.

Said Omar Said, maarufu kama Sugu.

 

Jamii yake ilimshangaa sana na inaendelea kumshangaa katika maonyesho yaliyofanyika mjini Mumbai anakoishi, akionekana kuweka historia kubwa. 

Ni kazi iliyomchukua miaka saba, akiunda  ndege ya abiria sita yenye uwezo wa kuruka kima cha kilomita nne na kusafiri  umbali wa kilomita nne kwa saa.

Kama ulivyo usemi “Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni” hilo katika kipindi hicho hicho cha mshangao wa Mumbai, limetokea kwa Mzanzibari, Said Omar Said, maarufu kama Sugu. 

Huyu naye, ambaye amemzidi   Yadav kwa miaka saba, kwa maana ya kuwa na umri wa miaka 51, katika

Maonyesho ya Viwanja vya Maisara, amewasilisha ubunifu wake wa kuunda helikopta, tena yake akitumia miaka mine, ikiwa ni pungufu kwa miaka mitatu kwa kazi ya Yadav.

Hii nayo ina uwezo wa kupakia abiria watano huku ikiwa ni hisitoria ya kwanza, kama ilivyo kwa Yadav.

Wengi nao wamemiminika kwa Saidi kushuhudia ubynifu wake unaoyapaisha Maadhimisho ya Miaka 54 ya Mapinduzi Zanzibar, kilele cha shamrashamra zake zikiwa ni leo.

Ni kawaida ya maonyesho ya biashara yanayowasilishwa katika kuadhimisha mapindizi kila mwaka.

Watu wakiwa wamezonga eneo hilo kushuhudia ubunifu huo wa Mzanzibari mwenye elimu ya kidatu cha tatu tu, Saidi anasema katumia jumla ya Sh. milioni nane kukamilisha kazi yake ya kibunifu.

Said au ‘Sugu’ anasema hicho ni kifaa chake cha tatu kubuni, ingawa anakiri kwamba kifaa cha safari hii - helikopta kimemgusa, pia kimewaacha watu katika mshangao mkubwa zaidi.

Anasema imemchukua miaka minne kubuni na kutengeneza usafiri huo wa anga hadi kukamilisha.Kilichomvutia 

Saidi anasimulia kuwa kilichomvutia kutengeneza usafiri huo ni ubunifu binfasi  aliokuwa nao na alijikuta akitengeneza usafiri huo ambao una uwezo wa kusafirisha abiria watano kwa wakati mmoja.

“Mimi ni mbunifu na nimeshabuni vitu vingi na hivi sasa akili yangu inavyoniongoza tu huamua kubuni na kutengeneza kitu ninachokikusudia,” anasema.

Saidi anasema usafiri huo una uwezo wa kuruka hewani kwa masafa kilomita 100 hadi 120 angani na inatumia mafuta ya ndege wastani wa lita 60.

Anasema, hadi kukamilika utengenezaji wa usafiri huo, imemgharimu Sh. milioni nane ya kununua vifaa mbalimbali, fedha ambazo ni zake mwenyewe na hakuna ama ufadhili au msaada wowote.

“Hivi sasa imemalizika na hapa ina uwezo wa kutembea, angani lakini hapa nasubiri kibali kutoka Mamlaka ya Anga Zanzibar,” anaeleza Saidi na anaongeza:

“Lakini leo natarajia kuiendesha kidogo ili wananchi waridhike, maana hapa toka jana wamekesha kutaka kuhakikisha inatembea,” anasimulia.

Ubunifu ulivyo 

Saidi anasema ameipa jina la ‘Sugu Air Force 0.1’ na ina uwezo wa kusafiri kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam kwa muda wa dakika 30.

Anasema alishawahi kutengeneza gari ya ilimuwezesha kushinda katika mashindano ya ubunifu yalioandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania na kuwa mshindi wa kwanza.

Mbunifu huyo anasema alishatengeneza puto lenye uwezo wa kuruka angani, lakini mamlaka ya anga ilimkataza kulirusha kwa sababu hakuwa na elimu ya urubani.

“Nilipewa tuzo katika mashindano ya Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania, kutokana na kubuni na kutengeneza gari, lakini kilichoniumiza kuwa niliahidiwa vifaa vyenye thamani ya Sh. milioni 12 nikabidhiwe, ili kuboresha ubunifu wangu wa gari niliyoitengeneza ili kuwa nzuri zaidi, lakini mpaka leo sijaletewa na nikavunjika moyo,” anasema.

Safari yake 

Analalamika kutoungwa mkono na serikali na taasisi mbalimbali, licha ya kuwa mbunifu wa vitu mbalimbali.

Sugu anasema alimaliza elimu yake ya kidato cha tatu mwaka 1982, katika shule ya Jang’ombe iliyopo mkoa wa Mjini Unguja, akiwa sasa mkazi wa Mpendae aliyejiajiri kwa ufundi magari na pikipiki.

Anaongeza kuwa:”Nimeunda gari mbili na baluni, watu na serikali imeona. Sasa sijui niiambie nini serikali, naona nitakufa na ubunifu wangu, kama muwa unavyokufa na utamu wake”.

Anawataka vijana wenye vipaji na ubunifu wajitokeza, akisema kuna uwezekano wakajitokeza watendaji wa kiserikali wenye mtazamo wa kuinua ubunifu na vipaji.

Mtazamo wake anasema, kutokana na umri mkubwa alio nao, anatamani kuwa mwalimu wa kuwafundisha vijana ufundi wa namna tofauti.

Maoni ya wananchi 

Ali Abdallah, ni miongoni mwa waliofika kwenye maonyesho ya viwanja vya Maisara kushuhudia ubunifu huo.

Anaomba serikali kutambua jitihada hizi za kibunifu, kwani katika nchi zilizoendelea, watu mfano wa mbunifu Saidi hutunzwa kutokana na mchango wanaoutoa kwa taifa.

“Inawaje sisi hatujafika katika maendeleo makubwa ya kuweza kutengneza usafiri wa anga, lakini ni muhimu akawekwa hata kutoa ushauri na kusadia vijana katika kufikia maendeleo ya usafiri wa anga,” ansema Abdallah.

”Mimi hapa nasubiri ipae hewani, maana inaonekana amechukua muda mrefu wa kutengeneza usafiri huu,”anasema Abdallah.

Ali Faki Hassan, mkazi wa Mkokoti Kaskazini Unguja, anasema alifika viwanjani hapo kwa shughuli nyingine, lakini baada ya kuona ubunifu huo, imebidi avunje safari zake ashuhudie usafiri huo wa anga, huku akikiri ishara alizoziona zina uwezo wa kuruka.

Anamsifu mbunifu huyo kuwa ni shujaa, hivyo anaielekezea ombi serikali imtazame na imuenzi mbunifu huyo, kwa sababu ameonyesha uwezo mkubwa ambao utaweza kuileta nchi maendeleo.

Hassan anaishauri serikali kufanya utaratibu wa kumuwezesha Saidi kuendeleza ubunifu wake huo, hata nchi kuwa na wataalamu.

“Tukiwa na wataalamu kama hawa, tutaweza kuwa na maendeleo ya viwanda kama Sera ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa ni nchi ya viwanda,” anasema Hassan.

Katibu Mkuu Viwanda

Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar, Dk. Juma Ali Juma, anaanza kwa kutoa mtazamo wake kuwa, iwapo wajasiriamali watahamasishwa, wana uwezo wa kutengeneza bidhaa nyingi zitakazoweza kuuzika katika soko la ndani na nje ya nchi.

Anaeleza kufurahishwa sana kuona mbunifu huyo ametengeneza usafiri huo, hivyo serikali inakusudia kuwahamasisha wajasiriamali kuwawezesha, ili kuweza kufikia mahitaji ya soko.

“Mimi nampongeza sana mbunifu huyu aliyetengeneza usafiri huu na wabunifu kama hawa tutawaendelea, ili kuweza kupata vifaa na kufanya kazi za ziada ili kuiletea nchi maendeleo,” anasema Dk. Juma.       

     

Habari Kubwa