Sajili kubwa za kishindo zilizozingua EPL 2018-19

18Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Sajili kubwa za kishindo zilizozingua EPL 2018-19

INAWEZEKANA wanatumia fedha kubwa au la, lakini klabu zinakuwa kwenye hatari kubwa wakati wanaposajili wachezaji wapya. Wanaweza kuwa wachezaji wenye majina makubwa, lakini kwa sababu mbalimbali wanajikuta wanakuwa hawapo kwenye kiwango.

Fred

Mifano ya hii ni mingi, kuanzia kwa Alvaro Morata na Michy Batshuayi (Chelsea), Alexis Sanchez (Manchester United), Eliaquim Mangala (Manchester City), na wengineo.

Wakati mwingine, sio kwamba mchezaji kiwango chake hushuka ghafla mara moja, lakini mazingira ya klabu yanaweza kutokuwa rafiki kwa mchezaji. Fikiria kesi ya Diego Forlan.

Nyota huyo wa Uruguay hakufanya vizuri wakati akiwa pale Manchester United, lakini alikuwa mnyama kabisa katika klabu za Villarreal na Atletico Madrid baada ya kuondoka Old Trafford.

Dirisha la uhamisho la majira ya baridi la 2018-19 liliona klabu zilivyojitokeza kwa ajili ya kusaka vipaji ili kufanikisha malengo yao. Cristiano Ronaldo (Juventus), Richarlison (Everton), na Alisson Becker (Liverpool) wamekuwa na mafanikio makubwa tangu watue kwenye klabu hizo.

Kwa upande mwingine, wachezaji waliosajiliwa kwa fedha nyingi wameonyesha matunda yao, lakini wengine hola.

Hapa tunaangalia nyota watano ambao pamoja na kusajiliwa kwa fedha nyingi, wamezikatisha tamaa klabu zao...

 

5. Jean Micheal Seri (Fulham)

Raia huyu wa Ivory Coast akiwa anacheza nafasi ya kiungo alionekana kuvuta hisia za klabu nyingi wakati anakipiga pale katika klabu ya Ufaransa, OGC Nice.

Klabu ya FC Barcelona ilitajwa kuwa miongozi mwa timu zilizokuwa zinamwania, huku kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Xavi Hernandez, akinukuliwa akisema Seri alikuwa na DNA ya Barca.

Uhamisho haukutokea, na mwaka mmoja baadaye, alijiunga na Fulham kwa pauni milioni 25. Lakini tofauti na matarajio ya wengi, Seri ameshindwa kutamba hadi sasa.

 

 4. Riyad Mahrez (Man City)

Inaweza kuonekana kuwa vigumu kumuhukumu winga huyu wa Algeria, kwa sababu yupo katika timu ambayo huduma yake inatolewa na wachezaji wengine watatu (Raheem Sterling, Bernardo Silva, na Leroy Sane).

Hata hivyo, kiwango chake anapopata nafasi ya kucheza sio cha kuvutia, anaonekana wazi kama si yule aliyekuwa akitamba kule Leicester. Mchango wake kwa Leicester wa kutwaa taji la Ligi Kuu England ulimvutia kocha wa Manchester City, Pep Guardiola.

Klabu ikaingia mfukoni na kuchomoka na pauni milioni 60, lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 ameshindwa kufanya lolote. Sterling na Sane wamefanya kazi bora kwa upande wao, kwa kuwa miguu yao inafanya kazi nzuri.

Mahrez alikuwa akionekana kama mmoja wa mawinga bora zaidi duniani, lakini sasa mambo yamekuwa tofauti kabisa.

Licha ya kufunga mabao 11 na kutoa pasi za mwisho saba katika michezo 37 hadi sasa, kiwango chake sio cha kuridhisha.

 

 3. Jorginho (Chelsea)

Mchezaji mwingine ambaye hajawahi kuonyesha ubora wake katika msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu ya England. Muitaliano huyo alinunuliwa sambamba na kocha, Maurizio Sarri kutoka Napoli, kwa pauni milioni 57 na kulikuwa na matarajio mengi juu yake, hasa kwamba angeweza kucheza vizuri katika staili ya kocha Sarri.

Lakini kiwango cha Jorginho wa Chelsea ni tofauti kabisa na kile alichokuwa nacho kule Napoli.

 

2. Naby Keita (Liverpool)

Mengi yalitarajiwa kutoka kwa mchezaji huyu wa kimataifa wa Guinea baada ya kuondoka kule Bundesliga katika timu ya RB Leipzig.

Kiungo huyo mwenye ujasiri alikuwa kwenye rada ya Jurgen Klopp na hatimaye akafanikiwa kumsajili Januari mwaka jana kwa pauni milioni 53 na mchezaji akijiunga na timu hiyo majira ya joto.

Haukuwa msimu wa kwanza wa furaha kwenye Ligi Kuu kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24.

Mambo hayajakwenda kama yalivyopangwa, kwa kuwa majeraha na kushuka kiwango limekuwa tatizo kubwa kwake, huku ujio wa Fabinho ukimfanya kukosa kabisa nafasi.

Amecheza mechi 25 katika mashindano yote (14 akianza). Hajafunga bao lolote au kutoa pasi ya mwisho.

 

1. Fred (Man United)

Wakati nyota huyo wa Brazil alipoitosa Manchester City, mashabiki wa United walikuwa wakipiga kelele za furaha baada ya kuwazidi kete katika usajili huo (ikiwa ni mara ya pili baada ya kuwadizi pia kwa Alexis Sanchez).

Fred aliwasili kwa usajili wa pauni milioni 52 kutoka Shakhtar, huku kukiwa na kipengele cha bonasi ya pauni milioni 61.

Ujuzi wake, ujasiri wake, na akili zilikuwa zina maana ya kumtuma kama ‘mpishi’ wa Paulo Pogba ili aweze kucheza kwa uhuru zaidi pale mbele. Lakini matokeo yake ameshindwa kabisa kuthibitisha thamani yake, kuanzia akiwa chini ya Jose Mourinho hadi sasa chini ya Ole Gunnar Solskjaer.

Yale matarajio ya mashabiki wa Man United yametoweka kabisa, hajawa na mchango wowote kwa timu hadi sasa.

Habari Kubwa