Sakala la kashfa ya benki ya Standard na aibu kwa nchi

10Feb 2016
Nipashe
Sakala la kashfa ya benki ya Standard na aibu kwa nchi

WIKI iliyopita tulitoa sehemu ya kwanza ya makala ambayo tulijaribu kuonyesha sababu zilizoifanya Benki ya Standard kukubali makosa ya kushindwa kuzuia vitendo vya ufisadi.

Katika sehemu hii ya pili tunaangal;ia mkakati huo na jinsi mzigo ulivyotupwa kwetu, Tanzania na athari zake
Kuna mambo mengi ambayo yatabaki siri kubwa. Sababu ni kwamba Benki ya Standard imekimbilia Mahakamani Uingereza kukiri kosa ili kutafuta kinga na kuitupia mzigo wa ufisadi Tanzania.

Na kwa upande wetu Tanzania kama itaamua kukimbilia kutumbua majipu bila kutafakari juu ya uzito wa ufisadi uliofanyika katika mradi huu juu ya Benki ya Standard ilifaidika kiasi gani na Tanzania inafidiwa kiasi gani, kutakuwa hakuna cha maana kitakachokuwa kimefanyika.

Madhumuni ya kutunga sheria ya mtu au taasisi kukiri makosa na kuwa tayari kushirikiana na Mashirika ya Uchunguzi wa makosa makubwa (SFO) ni kutoa nafasi kwa mashirika hasa makuwa kujirekebisha tabia ili yaendelee kutoa huduma kwa mujibu wa sheria.

Njia ya kushtakiwa kwa makosa makubwa inaweza kupelekea shirika kufutwa, wawekezaji kuuza hisa zao na viongozi wa Shirika kunyanganywa leseni za kuendeshea shughuli za Kitaaluma katika biashara ya fedha.

Baadhi ya viongozi wa taasisi za Kiserekali wamesifia njia hii ya kutanzua migogoro na mashauri, lakini Shirika la kuchuguza na kuraghibisha dhidi ya vitendo vya Rushwa (Corruption Watch) lina mawazo tofauti na kwa muhtasi kulenga kwenye sehemu kuu tatu.

Kwanza, hakuna Mkurugenzi au msimamizi yeyote katika Makao Makuu ya Benki ya Standard ambaye ameonekana anahusika na kufikishwa mbele ya sheria, kutokana na ukweli kwamba habari zote zilikuwa zinatoka kwenye matawi Tanzania, kuingizwa kwenye mchakato, kwa madhumuni ya uthibiti na uamuzi.

Wanaotupiwa mzigo na kutuhumiwa ni Mameneja wa matawi na maofsa wa Idara za serikali walioko Tanzania.
Ni wazi taswira inayojengwa ni kwamba masuala ya ufisadi yanafanywa na baadhi ya nchi ambazo hazijaimalika kidemokrasia na pia watu ambao wanatangazwa kuwa vinara wa kutoa rushwa kwa maofsa wa serikali ni watu watokao nchi za aina hiyo.

Pili uchunguzi uliofanywa na Shirika la SFO ni uchunguzi wa nini kilichokuwa kinaendelea ndani ya benki. Habari zimetolewa na Maafsa wa benki hizo. Ni siri ya SFO na Benki ya Standard, kwani wao ndiyo walisaini Mkataba wa kukiri kosa na hivyo Benki kupewa adhabu.

Kuna hoja kwamba habari habari zozote zinazohusu Benki ys Standard ilipata mapato kiasi gani na Tanzania ilipata hasara ipi ili Fidia kwa Tanzania itathimininiwe kwa kigezo cha faida na hasara, ni siri.

Mkakati wa mashirika ya Kimataifa ya kibiashara, madini na mafuta mara nyingi hupenda kuweka kipaumbele kisemwacho kwamba wakati kukitokea matatizo katika utekelezaji mradi au mahusiano na serikali ambapo vitega uchumi vimewekeza, njia za usuluhishi au shauri linaweza kufunguliwa katika mahakama za kimataifa au mahakama za nchi nyingine hasa zile za Ulaya na Marekani.

Mashauri ya kutoelewana au kukubaliana kati ya wawekezaji na serikali zimewahi kufunguliwa kati ya serikali ya Tanzania na mashirika ya uwekezaji kama IPTL na Shirika la Uingereza la mradi wa maji.

Kwa nini mashirika yanapendelea kufungua mashauri nje ya Tanzania; ni wazi kwamba mashirika hayo yamejenga picha kwamba Mahakama za Tanzania ni changa pengine zinapata ugumu wa kusimamia mashauri mazito kama hayo.

Wasiwasi mwingine huenda wanahofu majaji na wanasheria wa Tanzania labda hawana uzoefu na taaluma katika masuala ya uwekezaji na sheria za Kimataifa za kulinda Vitega Uchumi.

Jambo kuu ambalo limejitokeza katika siku za hivi karibuni ni lile lisemwalo, kwamba Mahakama za Tanzania ni vichaka vya rushwa kama ilivyoenezwa kwa suala la Akaunti ya Tegeta Escrow.

Madai ya Mahakama kuwa vichaka vya rushwa yapo mahala pote ulimwenguni.

Madai kwamba mfumo wa Mahakama za nchi za Ulaya Magharibi ni wa kibaguzi dhidi ya watu wasio wazungu umewahi kusikika ulimwenguni kote.

Au kwamba mahakama za Marekani na Italia zimetekwa na kuthibitiwa na makundi ya Mafia ni madai ambayo vilevile yamesikika.

Hata hivyo jambo la msingi la kuzingatia ni kwamba kila mfumo wa utoaji haki una historia, muktadha na falsafa ya jamii fulani.

Hivyo mfumo wa Mahakama wan chi za kibepari ni wazi utazingatia na kulinda maslahi ya ubepari, ikiwa ni pamoja na kulinda maslahi ya mashirika ya Kimataifa ya kibiashara, uchumi na uwekezaji ya nchi za Magharibi.
Kuna mambo ambayo kwa namna yoyote ile yanavunja sheria za kistaarabu na kama mambo hayo ni wazi, basi sheria hata katika nchi za Magharibi huchukua mkondo wake.

Lakini kuna mambo na njia ambazo hutumika kwamba utoaji haki kisiwe chanzo cha kuvunja mfumo wa kijamii na mfungamano wa utawala na taasisi za kiuchumi na biashara kitaifa na kimataifa.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa wakati Benki ya Standard ilipoamua kujishtaki na kukiri mbele ya taasisi ya Uchunguzi wa Makosa makubwa ya jinai (SFO).

Kama tulivyoeleza katika sehemu ya kwanza ya makala hii, Benki ya Standard, ambayo inamiliki na kusimamia mabenki ya Standard na Stanbic yaliyopo hapa Tanzania, ilitumia mbinu za kukiri kosa, kufanya uchunguzi wa ndani, kutoa habari za uchunguzi wake na kusaini mkataba wa Makubaliano na taasisi ya Mashtaka.

Benki ya Standard ilikubali kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za Uingereza za kukiri kutenda kosa na kupewa adhabu kwa misingi ya mshtakiwa kukubali kujirekebisha ili kusimamia vizuri uendeshaji wa shughuli zake, kwa madhumuni ya kuzuia vitendo vya rushwa na ufisadi.

Tatizo lote liko hapo. Kwa nini Benki ya Standard ilikubali kukiri kwamba ina makosa? Benki ya Standard ilifanya hivyo ili ielekeze uchunguzi, mashtaka na hukumu kuonyesha kwamba kilichofanyika ni kutokana na udhaifu wa mfumo ambao ulipelekea vitendo vya jinai kutokea.

Lengo kubwa likiwa kwa Benki ya Standard Kimataifa kujivua mzigo na kudai kwamba kule Tanzania; katika Benki zake za Stanbic na Standard na katika Idara za serikali ndiyo chanzo na mwisho wa ufisadi.

Kwa mara nyingine, Tanzania, ndani ya mashirika binafsi (benki) katika Idara za serikali (Hazina) na hata katika (Mahakama) zake, ambapo benki ya Standard haikwenda kukiri, ndipo kuna matatizo.

Kutokana kwamba wahusika ambao ni maofsa wanaotuhumiwa kutoka benki za Stanbic na Standard za Tanzania, maofsa wa serikali ambao inasemekana walihongwa na wengine wote wale ambao kwa namna moja au nyingine wanalijua suala hili kwa undani hawakuitwa kutoa ushahidi au kuwa marafiki wa mahakama, basi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lifanye uchunguzi wa kutaka kujua ukweli ili undani wa jambo hili ujulikane na kwa vipi Tanzania imepewa jina baya la kuwa kichaka cha ufisadi.

Vilevile Tanzania ifungue mashtaka dhidi ya Benki ya Standard kutokana na Benki hiyo kukiri huko Uingereza kwamba haikuzuia vitendo vya ufisadi vilivyofanyika ndani ya Benki hiyo.

Kama serikali itapeleka shauri hili mbele ya Mahakama, wakurugenzi wa benki ya Standard iliyoko Uingereza wataitwa shaurini na kutakiwa kujibu tuhuma na mashtaka, jambo ambalo halikutokea Uingereza na sasa wataalamu wa sheria wanabishania.

Ikumbukwe kwamba katika sheria ambayo benki ya Standard ilitumia kukiri makosa, kuna kipengele kisemacho kwamba ukitokea ushahidi mwingine ambao mhusika alificha kutoa habari, basi hukumu iliyotolewa itatenguliwa na mashtaka kuanza upya. Kwa madhumuni ya maslahi ya Taifa ni lazima Serikali ifungue mashtaka dhidi ya benki ya Standard yafunguliwe.

Habari Kubwa