Sakata la akina Lipumba CUF, maoni tofauti yatolewa

31Aug 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Sakata la akina Lipumba CUF, maoni tofauti yatolewa

“Tumbili akimaliza miti anakuja mwilini.”

Profesa Ibrahim Lipumba.

Hiyo ni kauli ya Mwanasiasa Mkongwe Hamad Rashid Mohammed, akimaanisha kuwa, wale wote wanaowafukuza viongozi na wafuasi ndani ya vyama vya siasa, zamu zao zinakaribia.”

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa makala haya, kufuatia hatua ya Chama cha Wananchi (CUF), kuwasimamisha na kuwafukuza baadhi ya viongozi wa chama hicho akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.

Hamad alisema, itafika wakati viongozi wakuu wa chama hicho nao watafukuzwa, kwa sababu tayari baadhi ya wafuasi wa CUF wameshadai kuwa Katibu Mkuu wao ambaye ni Maalim Seif Sharif Hamad, hafai.

Alisema mtu yeyote, taasisi au chama chochote kinachofanya jambo, kinatakiwa kujifunza na kujitathmini, lakini kwa CUF hawajifunzi hilo la namna ya kuongoza matatizo yanapotokea.
Hamad alisema, uongozi wao wa juu unategemea utashi wa mtu na sio utashi wa taasisi, na ndio maana imefikia hatua hiyo ya kutimuana.

Alisema walipaswa kujitathmini hao wanaowafukuza wenzao, kama wao hawana makosa, kwa kuwa nao wana makosa makubwa ndani ya chama hicho.

Mwanasiasa huyo alisema, chama hicho kimeundwa kwa mfumo wa umoja wa kitaifa, hivyo siyo busara kikaegemea upande mmoja tu wa nchi, ambao ni Zanzibar na kuitenga Tanzania Bara.

Alisema, madhumuni ya kuanzishwa chama ni kushika dola, lakini chama cha CUF, kimeshindwa kujidhibiti na hakiko makini na kwa hali hiyo kitaendelea kuwayumbisha wanachama wake.

“Wakati mimi nilipokuwa CUF, mfumo tuliokubaliana katika chama ni kuambiana makosa, sasa kama mnakataa kuambiana na unamuona mwezio mbaya huwezi kuendesha chama,”alisema kiongozi huyo ambaye na yeye ni miongoni mwa viongozi waliowahi kufukuzwa katika chama hicho.

Mkongwe huyo wa siasa za Zanzibar, na Tanzania kwa ujumla, alisema ni aibu chama kama hicho kikongwe kuwa na vurugu na kwamba hata hizo jumuiya za kimataifa walizoziomba kuwasaidia kupata demokrasia, zitawasaidiaje wakati wenyewe ndani ya chama wana migogoro kibao.

“Wewe mwenyewe una madhambi mangapi tukisema tunaanza kuhesabiana madhambi, pale hakuna anayeweza kubaki katika CUF,” alisema.

Aliwashauri viongozi hao waliosimamishwa uanachama wao wasiyumbe na akawakaribisha kujiunga na ADC, ili waweze kupanga utaratibu wa kuanzisha demokrasia ya kweli, ndani ya chama.

Naye Naibu katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema kuwa chama chochote cha siasa kinawajibu wa kuangalia anayekiuka miiko na taratibu za chama na kumwajibisha, lakini akasema chama kinapaswa kutoa nafasi kwa wanachama ya kuweza kujitetea, kabla ya kusimamishwa au kusitishwa uanachama.

Alisema, CUF kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad amekuwa na utaratibu na mtiririko wa kuwafukuza viongozi wenzake, bila ya sababu za msingi.

“Tumeshuhudia amemfukuza (James) Mapalala, Masoud Mageni, Hamad Rashid na hao akina profesa na wenzake, ambao wote hao walikibeba chama hicho kwa hali na mali, lakini tumeona pia ni jinsi gani Maalim anavyowaandama wenzake,” alisema Vuai.

Alisema kuwa hao wote waliofukuzwa walithubutu kumkosoa Maalim Seif, lakini hayupo tayari kukosolewa na kwamba ukimkosoa umekwenda kinyume, na dawa yake ni kukufukuza katika chama.

Vuai alisema, tofauti iliyopo kati ya CCM na CUF ni kwamba, CCM huwapa fursa viongozi wake waliofanya makosa fursa ya kuweza kujitetea katika vikao vya chama, lakini kwa upande wa CUF, inaonyesha hawana utaratibu huo.

Naibu katibu Mkuu huyo wa CCM, alimlaumu Maalim Seif na kumtupia lawama kuwa amepandikiza mbegu ya ubaguzi katika chama chake, kati ya Tanzania Bara na Uzanzibari, jambo ambalo ni baya sana.

Alisema hao wote waliosimamishwa uanachama ndani ya CUF ni watu makini wanaosimamia hoja, na watu ambao hawakubali kuburuzwa na kutokubali kwao kuburuzwa ndio kumesababisha uanachama wao kusimamishwa.

Alisema kuwa, vyama vyote vya upinzani vikipata ajali za kisiasa, mchawi wao huwa wanadai ni CCM jambo ambalo halipendezi, halijengi umoja na wala halileti tija.

Kiongozi huyo alisema, CUF sasa inaelekea kubaya, hivyo kinapaswa kujifunza ili kiimarike na kuweza kupambana katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Mwanaharakati wa mambo ya kisiasa Dadi Omar Maalim, alisema kuna namna ya usimamiaji bora wa demokrasia ndani ya vyama vya siasa inayohitajika, kwa sababu watu wengi waliingia katika vyama kwa lengo la kujipatia umaarufu na maslahi binafsi.

Alisema, inapotokea kiongozi amekiuka utaratibu na katiba za chama, ni sahihi kutolewa madarakani au kufukuzwa uanachama kwa sababu inaonekana hakubaliani na maamuzi na mwenendo wa chama, kwa hivyo kuendelea kubakia ni kuleta migogoro ya makusudi.

“Kwanza niipongeze CUF, kwa sababu ni wazoefu wa migogoro ya kisiasa kwa kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumika kukivuruga chama hicho,”alisema.

Alisema kuwa, viongozi hao walisimamishwa ama kufukuzwa uanachama inaonekana walikuwa wakitumika, kwa lengo la kuweza kuivuruga CUF.

Alisema sio chama cha CUF pekee ambacho kimechukua uamuzi huo wa kuwafukuza viongozi wake, kutokana na kwenda kinyume na utaratibu wa chama, kwani hata chama tawala kimeshawahi kuwafukuza viongozi wake.

Wakili wa kujitegemea, ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema kuwa, uhuru wa wananchi kujiunga na vyama vya siasa na chama kufukuza wanachama ndio hasa malengo ya kuondoa vikwazo vya kivyama na uhuru wa vyama.

Alisema, hivi sasa vyama vipo katika soko la kisiasa na wananchi ndio kama wateja, hivyo chama kisiporidhika na mteja kina uhuru wa kumfukuza na mwanachama asiporidhika na uongozi wa chama ana uhuru wa kukiacha.

Alisema kuwa, chama chochote cha siasa pamoja na viongozi na wanachama huwa wana misingi wanayoisimamia, kwa mujibu wa katiba na kanuni za vyama vya siasa, hivyo ikitokea wanachama wakaonekana kuwa wanakwenda kinyume, chama kina fursa ya kuwaacha.

Alisema, ndani ya CUF kuna viongozi waasi na ndio maana CUF imeshindwa kuwavumilia viongozi hao, hasa ikizingatiwa vurugu zilizotokea katika mkutano mkuu na ndio maana imefika pahala ikaamua kusimamisha uanachama wa baadhi ya viongozi wake.

Alisema, chama chochote cha siasa kilicho makini hakiwezi kuvumilia ubinafsi wa mtu, na Profesa Lipumba alikiacha chama kikiwa kwenye mapambano wakati wa uchaguzi.

“Kipindi ambacho ni msimu wa mavuno, lakini alijitoa katika nafasi ya uenyekiti na ndio maana CUF ikakosa imani naye ya kumpa tena nafasi hiyo,” alisema na kuongeza:

“Chama cha siasa hakiwezi kumnusuru mtu kama huyo, hivyo CUF kimefanya jambo la busara kuwasimamisha uanachama viongozi hao.”

Aliwashauri wanachama wa CUF kujua kuwa chama hicho kina malengo na misingi, hivyo kushikamana na kuondokana na siasa tegemezi kwa kujenga chama kama taasisi, na sio kuyumbishwa na maslahi ya watu fulani.

“Pia naupongeza uongozi wa CUF kwa maamuzi yao ya kukisafisha chama na kukibakisha kionekane chama kilichopevuka na kilichokuwa makini, ambacho hakiwezi kuruhusu kuchezewa, kwani hatua hiyo itawawezesha kuvuka tafrani zilizopo ndani ya chama hicho,” alisema.

Naibu katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui, alisema kuwa uamuzi wa chama hicho kuwasimamisha viongozi wao wakuu, hautaleta athari yoyote katika chama.

Mazrui alisema kwamba, chama kimeona hakuna dosari yoyote itakayopatikana, bali kubakia kwao ndio kutaleta madhara makubwa ndani ya chama hicho na ndio maana kimeamua kuwatimua.

Alisema kuwa, Baraza Kuu la CUF limejiridhisha kwa ushahidi wa kwamba viongozi hao wanatumiwa na wameshiriki kikamilifu katika kuvuruga mkutano Mkuu wa CUF, uliofanyika Agosti 21 mwaka huu.

Alisema, vurugu hizo zilizofanyika katika uchaguzi huo zilisababisha kukiletea fedheha kubwa na pia kupata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 600.

Hivyo alisema, kwa vile viongozi hao wanahusika moja kwa moja na vurugu hizo, kuwabakisha kwao ndani ya chama ni kuendeleza uovu katika chama.

“Unapata ajali ukaambiwa kata mkono bora kata mkono, kuliko ukaja ukaoza kiwiliwili kizima, na sisi tunaamini kwamba hawa wanaondoka kwa sababu hawatufai tena ndani ya chama chetu,” alisema.

Hata hivyo alifafanua kwamba, chama chao cha CUF hakina mila za kulea wala kuleana na huo ndio msimamo wao katika chama, na mtu ambaye hawezi kufanya kazi aache mwenyewe chama, lakini si kuwaharibia.

“CUF haina mila ya kulea wala kuleana, na huu ndio msimamo wetu kama umeshindwa kufanya kazi ondoka mwenyewe, hukuondoka tutakuondosha, lakini hatutakuachia ukiharibu chama, kitendo hicho hakiwezi kuvumilika, lazima hatua za kinidhamu zichukuliwe”, alisema.

CUF mbali ya kuwasimamisha na kuwafukuza chama baadhi ya viongozi wao, lakini pia walitoa karipio kali kwa mujibu wa Katiba ya Chama, Ibara ya 83 (5) (b), kwa wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, ambao ni Rukia Kassim Ahmed na Athumani Henku.

Viongozi waliosimamishwa uanachama kwa mujibu wa Katiba ya CUF, Ibara ya 83 (5) (c), hadi hapo watakapopata fursa ya kujieleza mbele ya Baraza Kuu ni Prof Ibrahim Haruna Lipumba, Magdalena Sakaya, Abdul Kambaya, Ashura Mustafa, Omar Mhina Masoud, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha, Maftaha Nachumu, Mohamed Habib Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.

Habari Kubwa