Samia alivyosawazisha tatizo lililokwaza uwekezaji nchini

26Nov 2021
Sanula Athanas
Arusha
Nipashe
Samia alivyosawazisha tatizo lililokwaza uwekezaji nchini
  • *Ajivunia mafanikio ndani ya muda mfupi
  • *Profesa uchumi aibuka na angalizo lake

JUNI 15, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alipozungumza na vijana jijini Mwanza, aliweka wazi kuwapo upungufu mkubwa wa ajira zao nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan, alipokutana na Mhandisi Ahmed El Sewedy, Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Elsewedy Electric ya nchini Misri, baada ya kuwasili Ikulu Chamwino jijini Dodoma, Agosti mwaka huu. PICHA: MAKTABA

Kimsingi, ni wimbo unaosikika nchini na kwingineko duniani, ingawa uhalisia wake unatofautiana kati ya taifa moja na lingine.

Wakati wa mkutano uliopita wa Bunge la Bajeti, wabunge pia waliibua suala hilo wakianika kinachowasibu vijana waliohitimu masomo, ni kukosekana fursa za ajira kwao.

Alipokuwa mkutanoni jijini Mwanza, Rais Samia alibainisha Tanzania ina jumla ya vijana milioni 20.7 wenye umri kati ya miaka 15 na 35, lakini kati yao asilimia 11.4 ya wenye sifa za kuajiriwa, hawako kazini.

Vilevile, akihutubia kinamama jijini Dodoma Juni, mwaka huu, Rais Samia alitaja idadi ya Watanzania wenye ajira rasmi kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2017 ni wastani wa milioni tatu (takwimu halisi 3,014,106).

Huo ni wastani wa asilimia tano ya Watanzania kwa mujibu wa takwimu za sasa, ndiyo wako kwenye ajira rasmi.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeripoti Agosti 14, 2019 kiwango cha ajira kilipungua kwenye sekta binafsi kutoka waajiriwa 239,019 mwaka 2016/17 hadi ajira 137,054 mwaka uliofuata, yaani 2017/18.

Rais Samia katika ufafanuzi wake kwa vijana, siku hiyo, aliangukia mtazamo wa wataalamu uchumi, akiwamo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Dar es Salaam, Prof. Honest Ngowi, kwamba fursa za ajira serikalini ni finyu na mtazamo mpana uko sekta binafsi.

Pia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inataja tathmini ya uhaba wa ajira kitaifa na kiini cha tatizo.

CAG, Charles Kichere, kupitia ripoti ya mwaka 2019/20 iliyowalishwa bungeni Aprili mwaka huu, anasema uwekezaji umepungua na kukwaza ajira.

Anabainisha miradi mipya kwenye Kituo cha Uwekezaji (TIC), ilipungua kwa wastani wa nusu na ndiyo ulikuwa uhalisia wa mwenendo wa ajira nchini miaka mitano iliyopita.

CAG anasema kwa kipindi hicho ajira zilipungua kutoka waajiriwa 63,223 mwaka 2015/16 hadi waajiriwa 32,115 mwaka 2019/20, sawa na asilimia 48.

Takwimu hizo zinatoa taswira inayokinzana na maelekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17- 2020/21) unaoielekeza serikali kuhamasisha, kuwezesha na kuratibu uwekezaji, mabadiliko ya teknolojia, viwanda na biashara nchini.

Ripoti ya CAG inasema kupungua miradi hiyo kumechangiwa na kuwapo mazingira hasi kwenye uwekezaji. Inabainisha Tanzania kuwa ya 141 kati ya 190 kwa vigezo vya mazingira rafiki, kwa uwekezaji na inatajwa kuporomoka kwa asilimia nane katika utengenezaji mazingira rafiki ya uwekezaji kwa miaka mitano iliyopita (2015-2020).

CAG anasema, ni hali inayosababishwa na TIC kutotoa huduma zote stahiki za uwekezaji (one stop centre), ikitoa huduma nne kati ya 11 zinazotakiwa kuwapo.

"Kuna ucheleweshaji wa mrejesho wa maombi ya uwekezaji katika mamlaka husika. Vigezo vya kimataifa vinataka iwe ndani ya siku 14, lakini uhalisia uliopo nchini ni siku 182 hadi 675," anabainisha.

Ni hali inayotoa tafsiri kitaalamu kwamba, hitaji la wiki mbili, linahitimishwa ndani ya wiki 26 au miezi sita.

CAG anadokeza Tathmini ya Athari za Mazingira inayotekelezwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), inachukua muda mrefu kukamilika, wastani wa siku 95.

Vilevile, ananyooshea kidole uhaba wa bajeti, akibainisha upungufu wa nusu ya hitaji halisi Sh. bilioni 45 (asilimia 49 ya mahitaji) na uhaba wa theluthi moja ya watumishi (asilimia 35 ya mahitaji ya watumishi 513) kwa mwaka huo wa ukaguzi.

Kupungua miradi mipya iliyosajiliwa TIC kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2020/21. CHANZO: Ripoti ya CAG 2019/20.

JICHO LA PROF. NGOWI

Katika wasilisho lake kuhusu uwazi na uwajibikaji wa kifedha wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Uwazi na Uwajibikaji (ITAC) jijini Arusha wiki iliyopita, Prof. Ngowi anashauri kuzitafutia ufumbuzi dosari zinazokwaza uwekezaji nchini.
Mkutano huo ulioshirikisha viongozi na wataalamu wa masuala mbalimbali yakiwamo ya kiuchumi, uliandaliwa na Taasisi ya WAJIBU.

Prof. Ngowi anasisitiza uwazi kwenye Utoaji vibali vya uwekezaji; ujenzi wa miradi; soko. Pia anasema kuwapo rushwa na kutotabilika kwa sera na sheria, kunasababisha uwekezaji nchini uendelee kuyumba.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya WAJIBU, Yona Killagane, anaunga mkono hoja ya serikali itafute majibu sahihi ya kukabiliana na kuyumba kwa uwekezaji nchini.

Killagane, pia aliishauri serikali kuondoa alichokiita ‘pengo la kibiashara’ kati yake na sekta binafsi. Anasema ni pengo hilo litakaloondolewa kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji miradi ya serikali.

Mwenyekiti huyo, anaishauri serikali iboreshe mazingira ya uwekezaji kutekeleza kikamilifu mpango mkakati wa kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini (Blueprint), ambao haujatekelezwa kikamilifu.

WAZIRI WA FEDHA

Akifungua mkutano, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, anakiri uwekezaji nchini umeyumba katika miaka ya karibuni na Rais Samia ameshaliona na kuweka mikakati ya kuimarisha eneo hilo.

Anasema, dhamira ni kuhakikisha uwazi na uwajibikaji unakuwapo katika usimamizi wa rasilimali za umma, kwa kuweka wazi takwimu na ripoti zinazohusu rasilimali za taifa.

Anasema mkuu huyo wa nchi anaendelea kuwawajibisha watendaji wa serikali wanaobainika kufuja mali ya umma na wanaoonekana kukwaza uwekezaji nchini.

Mkurugenzi wa Taasisi ya WAJIBU, Ludovick Utouh, katika hilo anampongeza Rais Samia kuanika matumizi ya Sh. trilioni 1.3 zilizokopwa na serikali kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kukabiliana na athari za UVIKO-19.

Utouh, aliyewahi kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), pia Mkurugenzi wa Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), anaendelea:

"Wananchi wana haki ya kujua matumizi ya fedha zao. Wakishajua matumizi ya fedha hizo, wanakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufanya ufuatiliaji ambao sasa utaimarisha zaidi uwajibikaji.”

MAFANIKIO YA SAMIA

Rais Samia alipohutubia mkutano wa Umoja wa Wanawake (UWT) visiwani Zanzibar, hivi karibuni, alisema katika kipindi kilichopita Tanzania ilipata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali zikiwamo za kimataifa, diplomasia ya Tanzania nje ya nchi imeimarika.

Anasema, kuimarika siasa za nje kumeyafanya mataifa kuishika mkono Tanzania kwa kuiunga mkono katika harakati zake za kuimarisha uchumi na maendeleo.

Rais Samia alisema katika uongozi wake atahakikisha unayafikia malengo ya maendeleo endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa (UN), huku akisisitiza mwanamke hataachwa nyuma katika safari hiyo.

Katika kuadhimisha Siku 100 za Rais Samia madarakani, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alibainisha kuongezeka miradi mipya ya uwekezaji inayosajiliwa nchini, baada ya mkuu wa nchi mpya kuimarisha uhusiano wa kimataifa.

Mnamo Juni 27, mwaka huu, kwenye ufunguzi wa kongamano la Siku 100 za Rais Samia jijini Dar es Salaam, Majaliwa alisema katika kipindi hicho cha miezi mitatu madarakani, ilisajiliwa miradi mipya 93 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.6 inayozalisha ajira 24,600 kwa vijana. 

Serikali iliyoko madarakani, kupitia ilani yake ya uchaguzi iliahidi kutengeneza ajira mpya milioni nane katika miaka hiyo mitano.