Sane alivyotua kibabe Bayern

06Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Sane alivyotua kibabe Bayern

KLABU ya Bayern Munich imekamilisha usajili wa winga, Leroy Sane kutoka Manchester City.

Sane mwenye umri wa miaka 24, amekubali kusaini mkataba wa miaka mitano na miamba hao wa Ligi Kuu Ujerumani, Bundesliga, ambao walithibitisha usajili wao Ijumaa iliyopita.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani kwa awali ameigharimu Bayern euro milioni 49, na itapanda hadi euro milioni 60, kwa mujibu wa Stats Perform News.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge, baada ya usajili huo alisema: "Tuna furaha kubwa kumkaribisha Leroy Sane hapa FC Bayern. Ni mmoja wa wachezaji ambaye tunamwelewa na ameshajithibitishia ubora wake mwenyewe kwa miaka michache iliyopita, hasa akiwa na timu ya taifa.

"Malengo yetu ni kuwaleta wachezaji bora wa Ujerumani hapa FC Bayern na usajili wa Leroy unahimiza malengo yetu. Ningependa kumshukuru Hasan Salihamidzic kwa kufanikisha uhamisho wake."

Salihamidzic, Mkurugenzi wa Michezo wa Bayern, aliongeza: "Tumefurahia ujio wa Leroy na kuwa mchezaji wetu wa Bayern. Leroy ni mtu wa kutengeneza tofauti na ataweza kuiimarisha timu yetu.

“Kwa uwapo wa Serge Gnabry, Kingsley Coman na Leroy, sasa tuko bora zaidi na tuna vifaa bora kuvitumia katika kila nafasi na ni watu muhimu sana kwenye kikosi chetu.

"Ningependa kuishukuru Manchester City kwa kuelewa na kufikia makubaliano mazuri. Ningependa pia kumshukuru rais na mwenyekiti kwa kuisimamia vizuri bodi ya wakurugenzi, Herbert Hainer, ambaye alikuwa mbele kwenye usajili huu tangu mwanzo na alielewa matatizo ya mlipuko wa virusi vya corona."

Akizungumza kabla ya mchezo wa Jumatano, Pep Guardiola alimtakia kila la heri mchezaji huyo kwa kile alichokifanya pale City na akasema ni mchezaji "sahihi" kwa Bayern.

Sane kujiunga na Bayern lilikuwa suala la muda tu, kwa sababu alikuwa akifuatiliwa tangu mwaka jana, ingawa awali miamba hao wa Ujerumani walibainisha kwamba wasingeweza kufikia bei waliyokuwa wakiitaka City.

Halafu akakumbwa na majeruhi makubwa ya goti wakati wa mchezo wa Ngao ya Jamii Agosti, mwaka jana na amerudi uwanjani mwezi uliopita.

Sane alijiunga na City akitokea Schalke mwaka 2016 katika dili ambalo lilitajwa kuwa thamani yake ni pauni milioni 37 na alikwenda kuonyesha kipaji cha kuvutia katika msimu wake wa kwanza.

Msimu wa 2017/18 alishinda tuzo ya mchezaji bora kijana wa mwaka wakati kikosi cha hicho cha Guardiola kikitwaa taji la Ligi Kuu England.

Sane aliisaidia City kutwaa taji hilo tena msimu uliofuata huku yeye mwenyewe akifunga mabao 16 katika mashindano yote, na hapo akaanza kuhusishwa na mpango wa kuwaniwa na Bayern.

Msimu huu kwa muda mwingine, Sane ameutumia akiwa majeruhi na kule Bayern ndio haswa sasa anakwenda kuonyesha kipaji chake kwa msimu unaokuja.

Guardiola amekubali kumuuza Sane kwa sababu angemwachia maana yake angeondoka kama mchezaji huru, kwani mkataba wake uliokuwa unamalizika Juni 2021.

Sasa Bayern, kwa ujio wa Sane maana yake ameongezeka baada ya ujio wa Tanguy Kouassi kutoka Paris Saint-Germain, ambaye mkataba wake na mabingwa hao wa Ufaransa ukiwa umemalizika.

Habari Kubwa