Sanga Aaga...

27Jan 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Sanga Aaga...
  • Aonya ukatili kijinsia ni kama janga la taifa

“UKATILI wa kijinsia ni tatizo kubwa katika jamii. Kuna matukio mengi yanayoendelea. Changamoto kubwa ni ule utayari wa wale tunaowatarajia kutoa vidhibiti na ushirikiano hawako tayari kufanya hivyo,”ndivyo anavyosema Edda Sanga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa), aliyemaliza muda wa uongozi wake Edda Sanga

Sanga Mkurugenzi Mtendaji  wa Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa),  aliyemaliza muda wa uongozi wake Januari 11, mwaka huu, anayasema hayo , anapomkabidhi kijiti na kumtambulisha kwa wanahabari Mkurugenzi mpya, Rose Reuben.

 

Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe ili kupata ufafanuzi zaidi,  anasema watu wanaotarajiwa kukomesha unyanyasaji wa kijinsia ni polisi, madaktari, waathirika, wazazi, walezi, ndugu, marafiki pamoja na majirani.

 

“Inaonekana ukatili mkubwa unafanyika ndani ya familia. Na huko ndiko kuna matatizo makubwa, lakini  familia zinaona raha zaidi kuhakikisha zinabakia kuwa  na  muonekana wa wastaarabu, hazitaki masuala hayo yatoke nje . Aidha,   hazijali kuhusu  kilichompata aliyefanyiwa ukatili,” anaonya Sanga.

 

Kadhalika, anasema kwa kipindi alichotumikia chama hicho kwa nafasi ya utendaji amebaini kuwa pamoja na hali hiyo uelewa wa masuala ya ukatili wa kijinsia  miongoni mwa Watanzania ni mkubwa na kwamba amebaini wako majasiri walio tayari kutoa taarifa na ushuhuda.

 

“Tatizo kubwa ni vyombo ambavyo vinatakiwa visaidie ili waliofanya matukio wachukuliwe hatua, taarifa za matukio haziwafikii kwasababu watu hawatoi ushirikiano. Tamwa imefanya vizuri lakini utayari umekuwa kikwazo sana ili haki itendeke,” anasema mkurugenzi mstaafu.

 

UFUMBUZI

Sanga anaeleza kuwa  suluhisho ni elimu na kuendelea kupeleka uhamasishaji kwa jamii kwa kutafuta mbinu nyingine zaidi ikiwamo uchechemuzi, kutumia sanaa, simulizi, ushuhuda kwa waliotendewa ukatili lakini hayo yafanyike baada ya kupata msaada wa kisaikolojia.

 

“Wapo ambao wamebakwa wakiwa watoto wadogo mpaka wanapokuwa wakubwa wanapata  msongo wa mawazo na wanaathirika kisaikolojia,” anasema Sanga.

 

Anaeleza zaidi: “Tunaofanyakazi ya uchechemuzi imefanyika kwa miongo mingi, wapo wanaohoji kuna haja ya kuendelea na uchechemuzi au zitafutwe njia mbadala za kuleta utofauti na mabadiliko ambayo ni chanya zaidi?”

 

Sanga ambaye ni miongoni mwa wanachama 12 waanzilishi wa Tamwa mwaka 1987, anasema uelewa, elimu, ubunifu na utayari wa jamii ni muhimu katika mapambano hayo na kwamba ni lazima kazi iendelee.

 

“Nikisema yote nina maana ya serikali, vyombo vya dola, mahakama, watunga sheria, raia wa wa kawaida, wazazi walezi, dini, walimu, wazee na viongozi wote wa kijamii, tukishirikiana na tukapata mkakati wa kutufanya tuweze kuzungumza haya masuala  bila kificho, wala kizuizi kwa mjadala wa kitaifa na kuona jambo linahitaji nguvu za watu wote,” anasema.

 

Aidha, anasema serikali imefanya jitihada nyingi ikiwamo mpango mkakati uliozinduliwa mwaka 2016, ambao umeleta usaidizi na kuzuia kwa kuwa kama inawezekana kutoa usaidizi wa aliyefanyiwa ukatili na kupunguza matukio ni jambo lenye manufaa na la kuungwa mkono na jamii.

 

Anasema jambo hilo likiachwa litaendelea kuleta madhara makubwa kwa jamii ya Watanzania na kuwa na watoto ambao wameathirika zaidi kisaikolojia.

 

“Mfano mimba za utotoni, siku hizi kuna matukio mengi na idadi inatolewa kila wakati ya watoto walioachishwa shule kwa mimba hizo ni kubwa na inaonyesha kwa jinsi gani tatizo linachangua kudumaza maendeleo ya taifa,” anabainisha.

 

Sanga anasema ikumbukwe  mabinti hao ndiyo walimu, walezi, wakulima wa baadaye na kwamba watakuwa wasio na elimu, wenye msogo wa mawazo na matatizo ya kiafya na kwamba hawatachangia kikamilifu kwenye maendeleo ya nchi.

 

“Napenda kuona taifa letu linatafakari katika mtazamo kuwa hawa ni jamii ambayo inangoja kuingia maeneo mbalimbali, kama  wazazi na walezi  wa  nguvu kazi.Lazima mipango yetu iangalie ukatili huu wa kubakwa, kulawitiwa na kuukomesha,” anasema.

 

KUENEZA UELEWA

Sanga anazungumzia uelewe wa masuala ya ukatili wa kijinsia, akisema moja ya mradi uliofanywa na Tamwa ni masuala ya kupinga ukatili katika wilaya 10, saba za  Bara na tatu za Zanzibar.

 

“Mfano kata za Kitunda na Kivule jijini Dar es Salaam kwenye Wilaya ya Ilala kuna jamii kubwa ya watu kutoka mkoani Mara. Tulipokuwa tunakwenda kuzungumza nao tulipata wanaume ambao waliitikia kikamilifu kupinga ukatili  lakini kwenye utekelezaji imekuwa ni tatizo kubwa,”anasema Sanga.

 

Walibaini kuwa kuna ushirikiano mkubwa wa wauguzi na madaktari katika kuendeleza ukeketaji watoto wachanga, na wahusika wanafanya hivyo kuogopa mkono wa sheria, anaongeza.

 

“Imani yao ni kwamba asiyekeketwa hajatimia, si mwanamke ambaye unaweza kukakabidhiwa majukumu, ukamwamini au akawa raia mwema na timilifu katika kabila lake,” anasema.

 

“Jingine ni suala la kiuchumi kwa kuwa mangariba wanapewa fedha nyingi kadri wanavyokeketa. Hivyo  wanahitaji kupata shughuli mbadala za kiuchumi na kuachana na  wanachokifanya. Mfano wazee wa kimila mkiongea nao wanakubali ni kitu kibaya lakini hawana uhakika wakiacha wataishije,”anasema Sanga.

 

 

“Haya ni masuala magumu kwa kuwa ni ya kimila, tamaduni na kiimani za kidini pamoja na ushirikina, si jambo la kwenda nalo kwa wepesi lazima tuendelee kuwaelimisha na kuchukua hatua maana bado wanatafuta njia mbadala ya kuendeleza mila zao,” anakumbusha Sanga.

JAMII ZA WAFUGAJI

Mkurugenzi mstaafu wa Tamwa anasema kwa upande wa jamii za wafugaji, tatizo ni kubwa lakini angalau kwa sasa utoaji wa elimu shirikishi unahusisha watoto imefanikisha kuwaeleza  kwanini ukeketaji ni mbaya hivyo waukimbie.

 

“Changamoto kubwa inakuwa  wanapokimbia kukeketwa jinsi ya kuwarudisha kwenye familia zao ili wakubalike na kuendelea na maisha inakuwa ngumu, lakini  jamii inaendelea kuelewa,” anasema.

 

NYAKATI NGUMU

 

Mkurugenzi huyo anasema wakati mgumu alioupata ni wa  kuwapata wanachama kushiriki kwenye uandishi wa habari hasa zinazohusu unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

 

“Ushiriki wao ulikuwa umelega sana, pamoja na kwamba niliingiza idadi kubwa ya wanachama lakini bado kazi haikuwa ya kuridhisha  katika shughuli mbalimbali za chama,” anasema na kuongeza:

 

“Niliingiza watu kwenye chama lakini hawakufanya kile kilichotarajiwa na niliingiza wengi ambao ni vijana na nilitarajia wangeleta mawazo mbadala na tofauti ambayo yanalingana na hali ambayo Tanzania, Afrika na dunia inakwenda.”

 

KUJITEGEMEA

 

Mkurugenzi huyo anayemaliza muda wake anasema ndani ya TAMWA amejifunza umuhimu wa  vyama vya kiraia kujitegemea kifedha na  kuwa na vyanzo vya ndani vya mapato na kuacha kutegemea wahisani.

 

“Unapotegemea wahisani chochote kinaweza kutokea, na kinapotokea mnakuwa hamjajiandaa hivyo kinawasambaratisha na kuwachanganya. Lakini mkiweza kuwa na vyanzo vya ndani mnasonga mbele …..,” anasema Sanga.

 

 

 

 

 

Habari Kubwa