Sare Yanga yazua kasheshe Mkwakwani

24Feb 2020
Isaac Kijoti
Tanga
Nipashe
Sare Yanga yazua kasheshe Mkwakwani
  • *** Polisi watuliza hali ya hewa, makocha, wachezaji wagoma kuzungumza baada ya...

BUNDI wa sare ameendelea kuganda mtaa wa Twiga na Jangwani baada ya jana kutoka sare ya nne mfululizo kwenye mwendelezo wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union.

Sare hiyo ilipokelewa kwa hisia tofauti kwa makocha na wachezaji wa Yanga kugoma kuzungumza na waandishi wa habari huku Ofisa Mhamasishaji, Antonio Nugaz, akimkunja shabiki mmoja aliyekuwa akiwarekodi.

Baada ya mechi hiyo, baadhi ya viongozi wa Yanga walionekana kujadili sare hiyo kwa hisia tofauti ndipo shabiki huyo alipoamua kuwarekodi kabla ya kunyang'anywa simu na kuwekwa mtu kati, lakini Polisi waliwahi na kuwatoa nje.

Kabla ya mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City, kisha suluhu na Tanzania Prisons mechi zote zikipigwa dimba la Taifa jijini Dar es Salaam. Baada ya hapo chupuchupu balaa la kupoteza liikumbe Yanga, lakini ikabahatika kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania katika Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Katika mchezo wa jana, Coastal ilizidiwa zaidi kipindi cha kwanza, lakini dakika 45 za mwisho Yanga ilionekana 'kukata pumzi' na wenyeji kuutawala mchezo.

Umakini wa kipa Metacha Mnata ulilinusuru jahazi la Yanga kuzama kutokana na mashuti makali yaliyokuwa yakirindimishwa langoni mwao na Ayoub Semtawa na Ayoub Lyanga.

Licha ya timu zote kufanya mabadiliko katika kipindi cha pili, hayakuweza kubadili matokeo ya mchezo huo ambayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 41 baada ya mechi 22.

Yanga iliwatoa Balama Mapinduzi, Tariq Seif na kuingia Mrisho Ngasa na Ally Mtoni huku Coastal ikiwapumzisha Mudathir na Semtawa na kuwapisha Hija Ugando na Kanduru.

Katika kipindi cha kwanza mpira ulichezwa zaidi langoni mwa Coastal Union na Yanga ilipata jumla ya kona sita dhidi ya moja ya wenyeji.

Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwenye mazoezi ya Yanga juzi, ndivyo ilivyotokea jana kwa kikosi hicho cha Mbelgiji Luc Eymael kushindwa kuzitendea haki kona hizo. Juzi katika mazoezi, Yanga ilikuwa ikifanyia kazi kona na hakuna hata moja waliyofanikiwa kuizamisha kimyani wakiwa mazoezini.

Yanga ilikuwa ya kwanza kufika langoni mwa Coastal, dakika ya kwanza tu, lakini haikuweza kuleta madhara kwa kipa Soudy Dondola wa Coastal. Jaribio la kwanza na hatari langoni mwa Yanga ilikuwa katika dakika ya 16, lakini kipa Mnata alikuwa makini kuzima mashambulizi ya Yanga.

Umakini wa kipa Dondola wa kulicheza shuti la Bernard Morrison katika dakika ya 32 uliinusuru Coastal kuwa nyuma kwa bao moja.

Shambulizi lingine hatari kwa Yanga ilikuwa dakika ya 45 baada ya Semtawa kuachia shuti kali kwa mguu wa kushoto, lakini Mtacha alikuwa makini kulicheza.

Habari Kubwa