Serikali, EU sasa kuwaonyesha Watanzania ulipo mlo wenye lishe

10May 2022
Gerald Kitabu
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali, EU sasa kuwaonyesha Watanzania ulipo mlo wenye lishe
  • *Kujenga vituo vya misosi asilia Dar, Z’bar

SERIKALI na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) wamezindua kampeni ya kitaifa ya lishe inayolenga kuwaelimisha, kuwahamasisha na kuwajengea wananchi tabia zinazofaa za kula vyakula bora vinavyopatikana nchini.

Wadau mbalimbali wakishiriki katika uzinduzi wa kampeni ya lishe bora: PICHA: GERALD KITABU

Kampeni hiyo ya kitaifa italeta mambo mapya ikiwamo kuanzisha maeneo ya vyakula asilia ‘ msosi asilia’ Dar es Salaam, Mbeya na Zanzibar ili kuimarisha mifumo ya chakula na lishe kwa kutumia vyakula vinavyopatikana katika maeneo watu wanayoishi.

Kampeni hiyo ya kitaifa inalenga kuwafikia Watanzania takribani milioni 32 inafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia programu ya AGRI-CONNECT, inayowahimiza watu kushiriki kikamilifu.

Uzinduzi wa kampeni hiyo ambao pia ulifanyika pia Zanzibar, ulifanyika katika soko la Kisutu jijini Dar es Salaam ukianza na kuhamasisha, kutoa elimu na kupanua wigo wa mazingira bora na wezeshi ili Watanzania wabadili tabia na kuanza kula mlo wenye lishe unaopatikana sehemu wanazoishi.

Viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wanasema inalenga kuimarisha lishe bora na kupunguza utapiamlo nchini, watu wakihimizwa kutumia vyakula vinavyopatikana kwenye mazingira yao.

Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula katika wizara hiyo, Dk. Honest Kessy, anazindua kampeni hiyo akisema kipaumbele cha serikali ni kupunguza utapiamlo kwa kiwango kikubwa kadri inavyowezekana.

Anawaambia washiriki kuwa kampeni hiyo imekuja katika kipindi ambacho dunia inahangaika kukabiliana na kumaliza janga la UVIKO-19.

“Tumeimarisha usimamizi wa masuala ya chakula na lishe kwa kuhimiza uwekezaji zaidi katika kilimo, uzalishaji wa chakula na elimu ya lishe ili kuongeza upatikanaji na ufikiwaji wa milo iliyo bora kupitia uzalishaji katika kilimo na uelewa bora zaidi wa umuhimu wa milo bora katika kuzuia matatizo ya afya kwa sababu ya ukosefu wa lishe na kuimarisha kinga ya mwili,” anasema Kessy na kuwataka wananchi kushiriki kikamilifu.

YATAKAYOFANYIKA

Kauli mbiu ya programu hiyo ni lishe bora ni mtaji, kampeni hii ya kitaifa itajumuisha shughuli mbalimbali kama vile programu za mapishi, ziara za elimu ya lishe katika daladala, mafunzo kwa vijana wasichana na kuanzishwa kwa maeneo ya chakula au msosi asilia itakayoandaa vyakula vya Kitanzania Dar es Salaam, Mbeya na Zanzibar.

Ndani ya kipindi cha miaka miwili kampeni inatarajia kuwafikia watu milioni 32 kupitia majukwaa mbalimbali likiwamo la mitandaoni.

TIJA YA PROGRAMU

Mwakilishi wa FAO nchini, Dk. Nyabenyi Tipo, anasistiza kwamba wakati janga la dunia likiendelea, umuhimu wa milo bora katika kukabili madhara yake ni wa muhimu zaidi.

Anaongeza kuwa mabadiliko katika tabia za jamii kuhusiana na uzalishaji wa chakula, ulaji, na ufikiwaji wa masoko utaongeza upatikanaji wa chakula, kuimarisha kinga ya mwili na kuwapa wakulima wadogo kipato.

Katika tukio hilo watu 100 wa kwanza kuwasili katika soko la Kisutu ulipofanyika uzinduzi huo walipewa kikapu cha chakula kilichojaa vyakula anuai vilivyoonyeshwa katika sahani ya mfano ya milo bora. Vyakula walivyopatiwa bure ni pamoja na nyama, samaki, mafuta, mbogamboga, matunda, viazi lishe, viazi mviringo, unga na maharage lishe.

Programu hiyo inayoongozwa na FAO inayoitwa kujenga uhimilivu wa mifumo ya kilimo na chakula na lishe bora katika muktadha wa janga la dunia ni nguzo ya nne ya mradi wa AGRI-CONNECT kusaidia minyororo ya thamani kuleta ustawi wa pamoja unaokazia zaidi lishe na kuanzisha mifumo ya kusaidia kupunguza makali ya janga katika upatikanaji wa chakula na masoko.

UDUMAVU UNATISHA

Akizungumzia hali ya afya kwa watoto chini ya miaka mitano, mtaalamu wa lishe ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mafunzo na Elimu ya Lishe, Dk. Esther Nkuba, anasema asilimia 34 ya watoto wa umri huo nchini wamedumaa.

Anaongeza kuwa hali ya lishe kwa watoto chini ya miaka mitano ni kiashiria muhimu kwa afya ya mtoto.

Anaeleza kuwa kulingana na takwimu za 2015-16 za Tanzania Demographic Health Survey (TDHS-MIS), asilimia 34 ya watoto chini ya miaka mitano wamedumaa, hali inayoashiria uwepo wa utapiamlo nchini. Asilimia tano ya watoto chini ya miaka mitano wana unyamavu hali inayoonyesha uwepo wa utapiamlo mkali.

Anawashauri wazazi kuwanyonyesha watoto wao kwa muda wa miezi sita bila kuwapa chochote kama inavyoshauriwa na watalaam ili kuwapa kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Mradi wa AGRI-CoNNECT unaonyesha juhudi mbalimbali za serikali kwa kushirikiana na wadau wa EU na FAO wanaopambana kupunguza tatizo hili na kuweka mikakati na mipango mbalimbali ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata mlo wenye lishe bora.

Tanzania ni moja ya nchi zilizo na ardhi yenye rutuba, mabonde na mito tena taifa linalima vyakula na matunda ya kila aina katika maeneo mbalimbali na hivyo kujitosheleza kwa chakula cha mwaka mzima.

Pamoja na kujitosheleza kwa chakula uzingatiaji wa lishe bora imekuwa tatizo kubwa. Mfano Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ya Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa na Katavi pamoja na kwamba ndiyo inayoongoza kwa kuwa na chakula kingi lakini inayoongoza kwa matatizo ya ukosefu wa lishe bora. Udumavu wa watoto chini ya miaka mitano kwa sababu ya kula aina moja ya mlo ni mtindo uliyozoeleka kwa kaya nyingi kwenye mikoa hiyo.

Ukitembelea miji mbalimbali mikubwa na midogo kuna ongezeko kubwa la watu wenye unene na uzito uliopitiliza na udumavu miongoni mwa watoto chini ya miaka mitano, yote yakiashiria ulaji duni.

Unene uliopitiliza wa mfano ni kihatarishi kimojawapo kinachoweza kusababisha magonjwa kadhaa ikiwamo magonjwa ya moyo, kiharusi, kisukari na kama vile saratani.

Habari Kubwa