Serikali inavyokosa mabilioni hoteli za kitalii

04Dec 2017
Sanula Athanas
Nipashe
Serikali inavyokosa mabilioni hoteli za kitalii

SERIKALI imepandisha makusanyo yake kutoka wastani wa Sh. bilioni 800 kwa mwezi kabla ya Novemba mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa Sh. trilioni moja kwa mwezi, kwa mujibu wa taarifa za kila baada ya miezi mitatu zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Hata hivyo, licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato, bado inakosa mabilioni ya shilingi kutokana na ufanisi duni wa ukusanyaji kwenye sekta ya utalii.

Hali hiyo inakinzana na dhamira ya uimarishaji uchumi ya Rais John Magufuli ambaye tangu aingie madarakani Novemba 5, 2015, amekuwa akitilia mkazo ulipaji kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya nchi.

Novemba 20, 2015, wakati akilizindua Bunge la 11 bungeni mjini hapa, Rais Magufuli alisema: "Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ukusanyaji wa mapato umekuwa chini ya makadirio kwa sababu mbalimbali. Serikali ya awamu ya tano itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

"Tutahakikisha kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki. Hatutasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayekwepa kulipa kodi. Kodi ni kitu muhimu, lazima kila mtu anayestahili kulipa kodi alipe."

Wakati Rais akihimiza wananchi walipe kodi na mamlaka ziongeze ufanisi katika ukusanyaji mapato, Nipashe imebaini serikali inapoteza mabilioni ya shilingi katika sekta ya utalii kutokana na udhaifu wa kimfumo kudhibiti mapato ya sekta hiyo muhimu.

Huku Wizara ya Maliasili na Utalii ikikiri kuwapo kwa changamoto hiyo, Nipashe imebaini azma ya serikali kuwa na watalii milioni nane na fedha za kigeni Dola za Marekani bilioni 20 (Sh. trilioni 43.7) kwa mwaka kufikia mwaka 2025, iko hatarini kutotimia kwa sababu ya kukosa mfumo madhubuti katika kufuatilia idadi ya watalii wanaolala kwenye hoteli na mabanda ya watalii nchini.

Nipashe imebaini walakini huo kutokana na ripoti mbalimbali za wizara hiyo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuonesha udhaifu katika udhibiti wa mapato ya sekta hiyo inayochangia asilimia 25 ya fedha zote za kigeni nchini.

Azma ya kufikia watalii milioni nane na kuingiza Dola bilioni 20 kufikia takriban miaka saba ijayo, ilibainishwa Novemba 10, mwaka huu kwenye ofisi ndogo za Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam wakati wa hafla fupi ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi - Maendeleo ya Utalii wizarani hapo, Uzeeli Kiangi, aliyestaafu mwanzoni mwa Julai mwaka huu baada ya kutumikia kwa miaka 33.

Mstaafu huyo alisema serikali ina azma ya kufikia watalii milioni nane na kupata fedha za kigeni Dola za Marekani bilioni 20 kila mwaka kufikia mwaka 2025, lakini azma hiyo huenda isitimie kutokana na mfumo duni wa utendaji katika sekta hiyo.

Bila kuzungumzia kwa kina kuhusu kasoro zilizomo kwenye mfumo wa utendaji wa sekta ya utalii, Kiangi alidokeza kuwa miongoni mwa mambo muhimu katika kufanikisha azma hiyo ya serikali ambako wao wanawajibika, ni watendaji wa sekta hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano, kuepuka rushwa na kuzingatia miiko ya kazi.

Wakati serikali ikiweka azma hiyo, takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonesha sekta ya utalii bado iko chini katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

Kitabu cha hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18 kilichosomwa bungeni mjini hapa Mei 23, mwaka huu na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, kinaonesha (ukurasa wa tisa) kuwa sekta ya utalii nchini inachangia asilimia 17.5 ya Pato la Taifa na inaipatia nchi asilimia 25 ya fedha zote za kigeni.

Huku malengo ya serikali yakiwa kufikia watalii milioni nane kwa mwaka kufikia mwaka 2025, kwenye ukurasa wa 136 wa kitabu hicho inaelezwa kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai Mosi, 2012 hadi Machi 31, mwaka huu (2017), jumla ya watalii waliotembelea hifadhi za taifa ni milioni 4.3. Kati yao, milioni 2.4 ni watalii wa nje na milioni 1.9 ni watalii wa ndani.  

 

RIPOTI YA CAG

Ripoti ya CAG kuhusu Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha 2015/16, pia ilibainisha kuwa kukosekana kwa mfumo madhubuti wa kudhibiti malipo ya huduma za hoteli za kitalii ni moja ya changamoto zinazofifisha mchango wa sekta ya utalii kwenye uchumi wa nchi.

CAG Prof. Mussa Assad alikabidhi ripoti hiyo kwa Rais Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam Machi 27, mwaka huu na baadaye kuiwasilisha bungeni mjini hapa Aprili 13, mwaka huu.

Katika ripoti hiyo (ukurasa wa 23 na 24), Prof. Assad alibainisha kuwa serikali inapoteza mapato kwenye mikataba ya upangishaji hoteli, nyumba za kupangisha na kambi za kulala watalii kwa kukosa chombo cha kufuatilia malipo ya wageni katika hoteli hizo.

CAG alieleza katika ripoti hiyo kuwa kwenye hoteli, nyumba za kupangisha na kambi za kulala watalii, wanapaswa kuilipa serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) tozo ya kuendesha biashara ndani ya eneo la mamlaka hiyo.

Prof. Assad alibainisha kuwa mapato ya serikali kwenye eneo hilo yanatakiwa kukusanywa kwa kutoza asilimia 10 ya malipo ya kila mteja kwenye hoteli kwa siku au kiwango maalum kilichokubalika.

Hata hivyo, CAG Assad katika ripoti hiyo alibainisha kuwa ukaguzi wake ulibaini taarifa za wateja wanaolala ndani ya hifadhi zinahifadhiwa na kutolewa na wamiliki wa hoteli, nyumba za kupangisha na kambi zilizopo.

"Mamlaka (Tanapa) haina utaratibu wa kuhakiki usahihi wa taarifa husika wanazopata kutoka kwa wamiliki wa sehemu hizo za malazi. Hii inapelekea mamlaka kutegemea zaidi na kutumia taarifa kutoka kwa wamiliki wa hoteli hizo," Prof. Assad alibainisha.

Alisema hali hiyo inaashiria kupotea kwa mapato ya mamlaka kutokana na menejimenti ya hifadhi kutokuwa na uwezo wa kuhakiki usahihi na ukamilifu wa taarifa kutoka kwa wamiliki wa hoteli hizo.

Kutokana na changamoto hiyo, CAG alishauri menejimenti ya Tanapa kuwa na chombo cha kuiwezesha kuhakiki usahihi na ukamilifu wa taarifa za wageni kama zinavyotolewa na wamiliki wa hoteli hizo.  

Prof. Assad pia alishauri kuwe na kiwango maalum cha tozo hizo ili kuondokana na udanganyifu unaoweza kufanywa na wamiliki wa hoteli na mabanda ya kulaza watalii.

WIZARA YAKIRI TATIZOKatika mahojiano maalum na Nipashe mjini hapa Novemba 12, mwaka huu, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, mbali na mambo mengine, alikiri kuwapo kwa changamoto za kimfumo kudhibiti mapato ya serikali yatokanayo na malipo ya watalii wanaolala kwenye hoteli na kambi za watalii nchini.  

Hasunga ambaye aliteuliwa na Rais Magufuli Oktoba 7, mwaka huu kushika nafasi hiyo, alibainisha kuwa katika kipindi kifupi cha uongozi wake wizarani hapo, ametembelea maeneo mengi na kupewa taarifa kuwa Tanapa wana mfumo wa kufuatilia malipo ya watalii lakini unatofautiana na unaotumika kwenye mamlaka nyingine ikiwamo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA).

"Tulifikiri kwamba ni muhimu kwanza kujua ubora wa mfumo walio nao ambao wao wanadai ni mzuri," Hasunga alisema, "wanasema wanao mfumo mzuri kabisa wa kuweza kujua kwamba ni mtalii gani kaingia nchini na yuko wapi na amelala hoteli gani.

"Hilo wametuambia wao lakini sisi hatujathibitisha kwa sababu hatujaenda kuangalia ile mifumo tuthibitishe hayo wanayoyasema. Kwa hiyo kazi tutakayoifanya ni kwenda kuiangalia hiyo mifumo kwa sababu kama wizara tuna kazi mbili; kwanza kuhifadhi na ya pili kuhakikisha kwamba tunaongeza mapato ya serikali. Sasa mapato haya hayawezi kuongezeka bila kudhibiti mianya hii ya upotevu.

"Changamoto ya pili kwenye hoteli ni hoteli zenyewe kuwa chache, lakini hata hizo hoteli zilizopo hatuna mfumo mmoja. Tanapa wana mfumo wao, Ngorongoro wana mfumo wao, Tawa (Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori) wana mfumo wao, Uhamiaji wana mfumo wao na kila mahali kuna mfumo tofauti na kwingine."

Alisema serikali imeona kuna haja ya kuwa na mfumo mmoja ambao mtalii akiingia Uhamiaji, anaonekana mara moja kwa mamlaka zote zinazohusika na utalii, hivyo kuziwezesha kupeana taarifa na kujua hoteli anayolala na watahakikisha hoteli zote zinaunganishwa na mfumo huo.

"Na tunataka tuwe na mfumo mzuri utakaotuwezesha watalii hata kabla ya kufika nchini, alipie 'online' (mtandaoni) na afanye 'booking' (aombe hifadhi) ya vitanda hata akiwa hukohuko kwao. Tujue kabisa hata kabla ya kuja, watalii wamekuja au wamelipia vitanda kwa kutumia mfumo uliowekwa," Hasunga alisema.

Naibu Waziri huyo pia alibainisha kuna hoteli zipo ndani ya hifadhi na zinatoza gharama kubwa zinazofikia Dola 5,000 kwa mtalii kulala kwa siku, lakini serikali kupitia Tanapa inaambulia Dola 50 pekee.

"Tunafikiri hili inabidi tulikalie pamoja, tulifanyie kazi, tuone namna bora ya kutuwezesha kugawana mapato yanayotokana na hizi hoteli za kitalii kuliko ilivyo sasa," Hasunga alisema na kufafanua zaidi:

"Mtu 'ana-charge' (anatoza) Dola 5,000, hata kama kuna gharama kubwa za uendeshaji, lakini 'ame-charge' (ametoza) pale Dola 5,000 kwa siku kwa sababu ya mandhari na maliasili zilizopo pale.

"Sasa serikali haiwezi tu kuchukua Dola 50 ikasema basi iridhike. Tunafikiri ni lazima tukae chini tuangalie utaratibu mzima wa namna ya kugawana yale mapato yatokanayo na huu utalii na wawekezaji wa hoteli. Hili tutalifanya maana hii ni changamoto pia."

KIKOSI KAZI

Nipashe ilimtafuta Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi, ambaye alikiri shirika hilo kutokuwa na mfumo mzuri katika kudhibiti mapato ya utalii na kubainisha kuwa tayari kuna kikosi kazi kimeundwa na serikali kwa lengo la kusaka mbinu za kuitafutia ufumbuzi changamoto hiyo.

Alisema kikosi kazi hicho kinatakiwa kiwe kimeshakamilisha kazi kiliyopewa na serikali na kukabidhi taarifa yake kufikia mwezi ujao.

"Kimsingi, hiyo ni changamoto ya serikali kwa ujumla. Si changamoto ya Tanapa pekee kwa sababu wageni wanapokuja, huwa wanafikia maeneo mbalimbali. Kuna hoteli zilizopo ndani ya hifadhi na nyingine ziko nje ya hifadhi na hivyo ziko chini ya mamlaka nyingine," Kijazi alisema na kueleza zaidi:

"Ili kupata taarifa sahihi lazima kuwapo na mfumo wa kitaifa ili mgeni anapoingia tu nchini, atafahamika atakwenda kukaa kwenye maeneo gani atakayotembelea na atakaa siku ngapi kwenye kila 'facility'(hoteli/ mabanda) na 'movement' (matembezi) yake nzima kwa ujumla katika nchi.

"Hiyo itasaidia kutoa picha nzima ya kitaifa kwa ujumla kwa sababu tukifanya sisi tu Tanapa, nchi haitaweza kupata picha halisi ya 'movement' ya wageni katika maeneo yake.

"Kwa hiyo ni changamoto ambayo inafanyiwa kazi na serikali -- kuanzisha mfumo ambao utaunganishwa na watu wa Uhamiaji, TRA na mamlaka nyingine ili sasa wageni wanapoingia, matembezi yao yaweze kufahamika na maeneo wanakopitia yaliyopo ndani na nje ya nchi yawe yanafahamika."

Mkurugenzi Mkuu huyo alisema Tanapa itashirikiana na serikali kutekeleza azma hiyo lakini akasisitiza kuwa kiongozi wao katika utekelezaji huo ni Serikali Kuu kwa maana ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Uhamiaji.

"Taarifa nilizonazo ni kwamba mfumo huo tayari umeshaanza kufanyiwa kazi, kuna kikosi kazi kimeundwa katika ngazi ya wizara na kimepewa hadi Januari kiwe kimekamilisha taarifa yake juu ya mapendekezo jinsi ya kuutekeleza mfumo huo," Kijazi alisema.

UFUATILIAJI KWA KINA

Nipashe pia ilimtafuta Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAT), Nura-Lisa Karamagi, ambaye pia alikiri kuwapo kwa changamoto ya baadhi ya wenye hoteli na mabanda ya kulaza watalii kukwepa kulipa baadhi ya tozo lakini akasisitiza kwamba kwa sasa serikali inawafuatilia kwa kina watoaji wa huduma hiyo.

"Kwenye hoteli na mahema yaliyopo hifadhini si rahisi kwa sasa mtu kukwepa kodi au tozo za serikali maana lazima mgeni anapowasili tu getini asajiliwe vitambulisho, hati ya kusafiria na TRA huwa inachukua risiti za malipo, huwezi tena kufanya utapeli," alisema.

Nura-Lisa aliongeza: "Kwenye hoteli zetu pia TRA wanakuja kukagua na wanaomba orodha ya wageni, mgeni akiingia kuna kitabu cha orodha ya wageni. Uhamiaji wakija pia wanaangalia na kujiridhisha.

"Kama hoteli haina kitabu cha wageni wanafanya makosa, lazima mgeni akiingia uchukue kumbukumbu zake. Hoteli kubwa zote zinafanya hivyo, labda hali ni tofauti kwa upande wa hoteli ndogo."

Akifafanua zaidi kuhusu huduma hiyo, Nura-Lisa alisema yapo mahema ambayo yanakuwa kama chumba cha hoteli ambayo yapo kwenye hifadhi na zipo hoteli katika hifadhi na nyingine ambazo hazipo kwenye hifadhi na kwamba tozo za ndani ya hifadhi ni tofauti na zile za nje ya hifadhi.

Alibainisha kuwa mgeni anapoingia kwenye hoteli iliyopo ndani ya hifadhi, anatakiwa alipe ada ya kiingilio cha hifadhi inacholipwa kwa Tanapa ambayo alidai ni Dola saba (Sh. 15,397).

Vilevile Ofisa Mtendaji Mkuu huyo alisema wageni wakishaingia hotelini, uongozi wa hoteli husika unapaswa kuilipa Tanapa Dola 50 (Sh. 109,980) kwa kila mgeni kwa siku na kama atakuwa na gari atatozwa na serikali Dola 30 (Sh. 65,988) kwa siku.

"Kuna kitu kinaitwa ushuru wa kulala kwa watalii ni Dola 1.5 (Sh. 3,299) kwa kila mgeni," Nura-Lisa alisema, "hii inachukuliwa na TRA. Gharama kwa mgeni ndiyo hizo.

"Kwenye hoteli zilizo nje ya hifadhi, ushuru wa kulala ambao analipa mgeni ni VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) kwa chochote atakacholipia na kupatiwa risiti ikiwa ni pamoja na gharama za chumba kwa siku."

'Kigogo' huyo wa HAT alibainisha kuwa kwa ujumla, serikali kwa sasa inapata wastani wa Dola za Marekani 132 (Sh. 290,347) anazotozwa mtalii kwa siku kwa kulala kwenye hoteli ya kitalii iliyomo ndani ya hifadhi na kwamba kumewekwa sharti mgeni akifika getini haruhusiwi kuingia bila kutaja jina la hoteli au kambi ya watalii anayokwenda kulala siku hiyo.

 

Habari Kubwa