Serikali inavyolea, kuibua wanasayansi wa ndani

26Jan 2021
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali inavyolea, kuibua wanasayansi wa ndani

SAYANSI, teknolojia na ubunifu vinatajwa kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu, ya kiuchumi na kijamii na kutokana na umuhimu wake, serikali hushindanisha wabunifu kwa lengo la kupata wabunifu na kazi zinazoweza kuendelezwa kwa tija kukuza utaalamu.

Helikopta iliyobuniwa na Adam Kinyekire wa Tunduma mkoani Songwe. PICHA: MTANDAO

Mashindano hayo hufanyika kila mwaka yakihusisha makundi ya wabunifu na wadau wa sayansi na teknolojia katika nyanja mbalimbali nchini, ili kuhamasisha na kuleta mwamko wa kuibua na kuendeleza teknolojia na ubunifu miongoni mwa Watanzania.

Baadhi ya yale ambayo wabunifu wamewahi kushindanishwa, ni kutengeneza vitu na kutoa mawazo yanayolenga kutatua matatizo mbalimbali katika sekta za afya, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na elimu, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Maulilio Kipanyula.

Anaongeza kuwa hadi kufikia mwaka juzi, serikali imetumia Sh. bilioni 50.55, kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu na kufadhili watafiti na wahadhiri katika mafunzo ya shahada ya uzamili na uzamivu.

Anasema hayo katika warsha ya siku moja kwa waandishi wa habari, inayofanyika jijini Dar es Salaam na kuongeza kwamba, serikali inawatambua wabunifu kuanzia ngazi ya chini ili kazi zao zinufaishe taifa na wao wenyewe wajikwamue kiuchumi.

Aidha, anawahimiza Watanzania kubuni na kugundua teknolojia ambazo zitasaidia nchi kupiga hatua kimaendeleo, ili kufikia uchumi wa viwanda na pia kuhamasisha watafiti wasiishie kusambaza matokeo ya utafiti bali pia wauweke kwa namna ambayo utawafikia walengwa kwa lugha rahisi.

Miongoni mwa wabunifu walionufaika na Sh. bilioni 50 ni Adam Kinyekire, aliyepata Sh. milioni 99 kwa ajili ya kuendeleza utafiti wa kutengeneza helikopta, uwekezaji unaohusisha kuimarisha karakana.

Aidha, fedha hizo zimelenga kuongeza ubunifu, utafiti na kuibua teknolojia zaidi na pia ili kumsaidia serikali imemuunganisha na Shirika la Nyumbu la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) la Automotive Technology Centre (TATC), lililoko Kibaha kama njia ya kuendeleza ubunifu wake, anasema Profesa Kipanyula.

Mtaalamu wa Fizikia Edwin Konzo, anasema wabunifu wengi zaidi wanatakiwa kujitokeza kila mashindano yanapofanyika ili kazi zao ziweze kutambuliwa na kuendelezwa kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla na kwamba teknolojia na ubunifu ndilo eneo muhimu zama hizi za sayansi na teknolojia.

Anasema kupitia mashindano, serikali inaibua kutambua na kuendeleza ubunifu na ugunduzi unaofanywa na Watanzania hususani wale wa ngazi za chini na inatoa nafasi kwa wahusika hao kujitangaza na kujulikana na wadau wa ubunifu wa ndani na nje ya nchi.

Mkuu wa Mawasiliano serikalini, Sylivia Lupembe, anasema, kushindanisha ubunifu ni mkakati wa serikali ambao unalenga kuwaibua na kuwafikia watu wengi zaidi wanaoshiriki katika mashindano kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo vya ufundi stadi, vyuo vya ufundi wa kati, vyuo vikuu, taasisi za utafiti na maendeleo na mfumo usio rasmi.

“Mashindano haya ni chachu ya ubunifu wa teknolojia, hivyo Watanzania zaidi wanatakiwa kutumia teknolojia, kwa kuwa ni kichocheo cha maendeleo ya haraka katika sekta ya huduma.” Anasema Sylvia.

Anaongeza kuwa kupitia mashindano ya ubunifu, washindi wanapata kipato kutokana na kiwango cha fedha ambacho kinatolewa na kwamba serikali itazidi kuendeleza ubunifu ili uwe bidhaa na uchangie katika kukuza uchumi na maendeleo ya taifa.

Anasema, kwa utaratibu huo, ana uhakika wabunifu wengi zaidi wanaweza kuwa wanajitokeza kila mashindano yanapofanyika, kwa kuwa mbali na kuongeza ubunifu wananuifaka kwa kazi zao.

Suala la ubunifu, ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele katika ilani ya CCM ni pamoja na kukuza sayansi, teknoloja na ubunifu ili vitumike kikamilifu kuendesha sekta za kukuza uchumi na kuleta maendeleo.

Katika ilani hiyo serikali imeahidi kuimarisha mfumo wa uratibu wa shughuli za sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchangia kwenye ujenzi wa uchumi imara na endelevu na kutenga fedha ili kusomesha Watanzania nje na ndani ya nchi katika vyuo bora duniani kwenye sayansi, teknolojia na tiba ili kupata maarifa bora na ujuzi utakaochochea maendeleo nchini.

Ilani inasema kuwa serikali itaweka mazingira wezeshi kwa wataalamu wabobezi kutoka nje kuja kufanya kazi nchini, ili kuhawilisha (kuhamisha) maarifa na teknolojia kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Ahadi nyingine ni kuweka kipaumbele katika kujenga na kuendeleza uwezo wa Watanzania na kuimarisha matumizi salama ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika maeneo ya kimkakati, ikiwamo matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia na maendeleo ya teknolojia ya kidijitali.

Maelekezo mengine ya CCM kwa serikali, ni kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kusimamia na kuendeleza masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa kuratibu uwekezaji utafiti unaochochea ugunduzi na utakaowezesha nchi kupunguza utegemezi wa teknolojia zinazotoka nje.

Habari Kubwa