Serikali za Kiafrika na intaneti

16Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali za Kiafrika na intaneti
  • Si Facebook, Twitter wala WHATSAPP

NI jambo linalozidi kuwa la kawaida katika baadhi ya mataifa ya Afrika, ambako serikali zimezima mara kwa mara intaneti au kuzuia mitandao ya kijamii.

Watu wengi hutumia huduma za intaneti kama anavyoonekana raia huyu.PICHA: MTANDAO

Mwaka mmoja umepita tangu Chad ilipobana mitandao maarufu ya kijamii na miezi kadhaa baada ya mawasiliano ya intaneti kufungwa katika miji muhimu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) baada ya uchaguzi mkuu.

Sudan ilibana nafasi ya raia kuingia katika mitandao wakati wa maandamano dhidi ya serikali kama ilivyokuwa nchini Zimbabwe.

Wanaharakati wa dijitali wanasema hilo ni kubana taarifa, lakini serikali zinadai inasaidia kuimarisha usalama.

Basi serikali inafanikiwa vipi kufunga au kubana mitandao?

Serikali inaweza kubana matumizi ya intaneti kwa kuagiza kampuni zinazotoa huduma za intaneti (ISPs) kudhibiti au kubana uwezo wa wateja kuingia katika mitandao.

Mara nyingi huwa kuna kizuizi kinachowekwa kwa wateja kutofika katika mitandao ya kijamii inayotumika sana.

Kama hatua kali zaidi, serikali inaweza kuagiza kufungwa kabisa huduma nzima ya intaneti.

Mnamo mwaka 2018, kulikuwa na visa 21 ambapo intaneti ilifungwa kwa kiwango fulani au kabisa, ikilinganishwa na visa 13 mnamo mwaka 2017 na visa 4 mwaka 2016, kwa mujibu wa kundi la uangalizi la kujitegemea Access Now.

Ivory Coast, DRC, Chad, Cameroon, Sudan, Ethiopia, Mali, Nigeria na Sierra Leone zilibana intaneti mwaka jana.

Ni mtindo unaodhihirika duniani kote. Mnamo 2018, kulikuwa na visa 188 vya intaneti kubanwa ikilinganishwa na 108 mwaka 2017 na 75 mwaka 2016.

Katika kila nchi, ni uamuzi wa kampuni zinazotoa huduma hiyo ya intaneti kutekeleza maagizo ya serikali kubana intaneti.

Mfumo mmoja unaotumika unafahamika kama URL-based blocking. Huu ni mfumo unaohusisha kuweka kizuizi kinachozuia wateja kuingia katika mitandao iliyopigwa marufuku.

Mteja anayejaribu kuingia katika mitandao hiyo hupata ujumbe “server not found” au mtandao haupatikani, umezuiwa na msimamizi wa mtandao.

Mfumo mwingine unafahamika kama 'throttling'.

Mbinu hii huzuia kwa kiwango kikubwa idadi ya wateja wanaotembelea mtandao maalum, na kutoa hisia kwamba kasi ya huduma ni ndogo na kuwafanya wateja waelekee kwingine.

Hili ni la afueni, kwasababu ni vigumu kutambua iwapo mitandao inazuia wazi au ni kutokana na upungufu wa miundombinu duni.

Kama hatua ya mwisho, kampuni za mawasiliano zinaweza kutakiwa kufunga kabisa huduma kwa ujumla na kuzuia wateja kupokea data yoyote.

JE KAMPUNI ZINAWEZA KUSEMA ‘HAPANA?

Uwezo wa serikali kubana intaneti unategemea uwezo wao kudhibiti kampuni za mawasiliano nchini.

Kampuni za kutoa huduma ya mawasiliano zinapewa vibali na serikali, jambo linalomaanisha kwamba huenda wakatozwa faini au wakapoteza mikataba.

Huenda wateja wakawa na haki ya kukata rufaa mahakamani, lakini kiuhalisi ni aghalabu kuona hilo likifanyika.

Mapema mwaka huu Mahakama nchini Zimbabwe, iliamua kurudishwa huduma ya intaneti baada ya serikali kuagiza ibanwe.

Kwa upande wake serikali ya Zimbabwe imeidhinisha sheria mpya zinazoipa udhibiti mkubwa katika matumizi ya intaneti.

Waziri wa Habari Zimbabwe, Monica Mutsvangwa anasema hili “litahakikisha kwamba intaneti na teknolojia zinazohusika zinatumika kwa manufaa ya jamii, na sio kukiuka usalama wa kitaifa.”

Lakini kuna mifano pia ambapo serikali zinazotaka kufunga intaneti zinakuwa na urahisi wa kulitekeleza hilo.

“Kuna mataifa kama Ethiopia ambapo sekta ya mawasiliano ya simu bado iko chini ya serikali,” anasema Dawit Bekele, Mkurugenzi wa Ofisi za Afrika za Jamii ya Intaneti.

“Kama intaneti imefungwa kabisa kuna namna ambazo wateja wanaweza kutumia kuepuka vizuizi vilivyopo na kuingia katika mitandao,” anaongeza.

Mbinu inayofahamika sana ni ya kutumia mitandao inayoruhusu kuruka vizuizi (VPNs).

Mitandao hii huwa kama njia, inayofanya kuwa vigumu kwa kampuni ya kutoa huduma za intaneti kuweka vizuizi kwa mitandao iliyopigwa marufuku.

Serikali zinaweza pia kuzuia VPNs, lakini si sana kushuhudiwa kufanya hivyo kwasababu hutatiza shughuli za wanadiplomasia na kampuni kubwa zinazotegemea intaneti kwa shughuli zao.

Baadhi ya mataifa yametaja sababu ya kusambaa kwa ‘habari za uongo’ katika mitandao kama sababu ya kuidhinisha vikwazo hivyo.

Lakini wachambuzi na viongozi wa upinzani wanataja hii kuwa sababu ya kukandamiza makundi yanayozikosoa serikali, ambayo hutumia mitanda kama Facebook na WhatsApp kujipanga.

BBC

Habari Kubwa