Sheria kuweka mazingira bora sekta huduma ndogo za fedha

14Feb 2020
Theodatus Muchunguzi
Dar es Salaam
Nipashe
Sheria kuweka mazingira bora sekta huduma ndogo za fedha
  • Itaweka nidhamu, uwazi katika Saccos, Vikoba
  • Riba tata, fedha kuibwa kwenye vibubu kukoma
  • Faini, vifungo watakaokiuka zawekwa bayana

KUKOSEKANA kwa sheria ya kusimamia, kuratibu na kuendelea sekta ndogo ya fedha kwa muda mrefu nchini, kumesababisha huduma kutolewa kiholela, huku watumiaji na watoa huduma wakiathirika.

Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha nchini, Dk Charles Mwamwaja.

Sekta hiyo inatajwa kuwa na umuhimu mkubwa kwa Watanzania wengi ambao wanaitumia kupata huduma za fedha. Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Huduma Ndogo za Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dionisia Mjema, takribani asilimia 80 ya Watanzania wanatumia huduma hizo.

Kutokuwapo kwa sheria hiyo tangu Uhuru, huduma zimekuwa zikitolewa katika mazingira yasiyo rafiki, huku watumiaji wa huduma hizo wakijikuta wametapeliwa. Kwa mfano, kuna waliopoteza mamilioni baada ya kushindwa kuvuma mbegu walizozipanda katika Deci na wengineo.

Pia kuna watoa huduma ambao wamekuwa wakiathirika kutokana na kuwakopesha watumiaji, lakini wateja hao hawarejeshi mikopo sababu ikiwa wakopeshaji kutokuwa na taarifa sahihi za wakopaji, hivyo wakati mwingine kuingia mitini.

Baada ya kubaini kasoro zote zilizokuwa zikiathiri sekta hiyo na kushindwa kuboreka na kuwa endelevu, serikali hatimaye ilianza kuchukua hatua kadhaa kwa ajili ya kuziba mapungufu hayo.

Lengo la serikali wakati wa kuanzisha mchakato huo mwaka 2007 lilikuwa ni kuitambua sekta hiyo, kuisimamia, kuiratibu, kuiendeleza na kuiwezesha ili iwasaidie wananchi katika kujikwamua na umaskini. Mchakato huo ulianza rasmi mwaka 2012 kwa utafiti na kukamilika mwaka 2018 ilipotungwa rasmi sheria hiyo kisha kufuatiwa na utungwaji wa kanuni zake mwaka 2019.

Kanuni hizo ambazo zilitungwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zimejikita katika maeneo mengi kwa kuweka masharti kuanzia usajili na utoaji wa leseni kwa madaraja yanayojuhusisha na utoaji wa huduma ndogo za fedha.

Zinaweka mazingira ya kuhakikisha kwamba watoa huduma wanatambulika, wanavyoendesha shughuli zao pamoja na kuwa na utaratibu wa kuwa na taarifa za wateja wanaowahudumia.

Sekta ndogo ya huduma za fedha inajumuisha watoa huduma katika madaraja manne. Daraja la kwanza linahusisha taasisi zinazopokea amana wakiwamo wakopeshaji binafsi wakati daraja la pili linahusisha taasisi za huduma ndogo za kifedha zisizopokea amana wakiwamo wakopeshaji binafsi, watoa huduma kwa njia za kielektroniki na kampuni za mikopo.

Madaraja haya mawili kwa mujibu wa Shanii Mayosa, Mwanasheria, ambaye ni mjumbe wa kikosi kazi cha utoaji elimu kwa umma kuhusiana na sheria hii ambayo inaelekeza kuwa muda wa mwisho kwa watoa huduma za kujisajili au kuwa na leseni ni Oktoba 31, mwaka huu, yanasimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Daraja la tatu ni vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (Saccos). Makundi haya matatu sheria hii inataka kukata leseni kwanza kabla ya kuanza kutoa huduma wakati na daraja la nne linalojumuisha vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kama Vikoba halibanwi kuwa na leseni bali kujisajili tu.

Katika usimamizi na uratibu wa daraja la tatu na nne, BoT, imekasimisha madaraka kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa ajili ya Saccos na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa ajili ya Vikoba.

Alizungumza mjini Morogoro wiki iliyopita wakati wa ufunguzi wa semina ya wahariri uliyoandaliwa na mamlaka za serikali zinazohamasisha umma kuhusu sheria hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James, alisema changamoto zilizoathiri usimamizi, udhibiti na ustawi wa sekta ndogo ya fedha ni taasisi za huduma ndogo za fedha kutoa mikopo kwa wananchi kwa vigezo na masharti magumu hivyo kusababisha madhara kwa wananchi, ikiwamo viwango vikubwa vya riba na tozo, kukosekana kwa uwazi wa masharti ya mikataba na mikopo.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha nchini, Dk Charles Mwamwaja, James alitaja changamoto nyingine ni utoaji holela wa mikopo uliosababisha limbikizo la madeni kwa wateja, utaratibu usiofaa wa ukusanyaji wa madeni unaosababisha wananchi kupoteza mali zao na kujitokeza kwa baadhi ya wananchi wasio waaminifu na wanaotumia mwanya wa kutokuwapo kwa sheria mahsusi kutoa huduma ndogo za kifedha.

Kwa mujibu wa james, mambo mengine yaliyoathiri ni kuwapo kwa baadhi ya taasisi za huduma ndogo za fedha zisizotoa gawio au faida kwa wanachama au wateja wanao weka fedha kati ya asilimia 25 hadi 30 kama dhamana ya mikopo na ukosefu wa takwimu au taarifa sahihi za uendeshaji wa taasisi za watoa huduma ndogo za fedha.

Pia kukosekana takwimu na taarifa tajwa na kusababisha Serikali kutojua mchango wa sekta ndogo ya fedha katika uchumi wa Taifa.

Aidha alisema tatizo jingine lililobainika ni ukosefu wa utaratibu wa kuwalinda watumiaji wa huduma ndogo za fedha na kuwapo kwa mianya ya utakatishaji wa fedha haramu kutokana na taasisi za huduma ndogo za fedha kutokuwa na utaratibu wa kisheria unaozitaka kutekeleza matakwa ya sheria ya udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu.

Katibu Mkuu huyo kadhalika, alibainisha kuwa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari watafikisha elimu hiyo kuhusu sheria na kanuni kwa makundi mengine mbalimbali ya kijamii ili wananchi waweze kutumia huduma ndogo za kifedha kwa weledi na kusaidia katika kupunguza umaskini.

Kwa upande wake, Dk. Mwamaja, anasema lengo la serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kunufaika na rasilimali nyingi zilizopo nchini kupitia fursa za kiuchumi na kwamba hilo litawezekana kwa kutumia sekta ndogo ya huduma za fedha.

Dk. Mwamaja anasema kuna umuhimu mkubwa wa kuwakumbusha wananchi kuzitumia huduma ndogo za fedha kufanya uwekezaji na kwamba fedha hazina thamani bila kuziwekeza.

“Halmashauri zina wataalamu ambao wanaweza kuwasaidia kuwaendelea na kwa kuzitumia fursa hizi zitawasaidia kuongeza kipato kuondokana na umaskini kwenye halmashauri zetu 185 nchini,” anasema Dk. Mwamaja.

“Sekta hii ni pana, lakini pia zipo fursa nyingi zinazotolewa kupitia mabenki, bima, hisa na mifuko ya kijamii, ni lazima wananchi washiriki kwa kuwapa elimu kuwa wakishiriki wanaweza kunufaika kiuchunmi na kuondokana na umaskini,” anasema Dk. Mwamaja, na kuongeza kuwa jambo la msingi ni kutolewa kwa ujumbe mzuri ambao hauna upotoshaji.

Kutokana na sheria hii kuipa BoT mamlaka ya usimamizi pamoja na kumpa Waziri mwente dhamana ya Fedha na Mipango mamlaka ya uhamasishaji, utelekezaji wa sheria na kanuni zake utaweza kuitambua, kuiboresha, kuiendeleza na kuiwezesha sekta ndogo ya huduma za fedha baada ya utekelezaji wake kuanza Novemba 1, mwaka huu.

Kuna mazuri mengi ya kuiweka katika mstari sekta hii ikiwamo kuwalinda watumiaji na watoa huduma. Kwa mfano kwa upande wa madaraja ya tatu na nne; kwa maana ya Saccos na Vikoba ambayo yalikuwa na changamoto kubwa kanuni zimekuja na dawa ya kuzitibu.

Josephat Kasamalala, mjumbe wa kikosi kazi cha kuhamasisha sheria hiyo kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, anataja baadhi ya mambo yaliyoko kwenya kanuni hizo kuwa ni kuzitaka Saccos kutoa gawio kwa wanahisa wake, kitu ambacho hakikuwapo katika vyama viongi.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, Saccos zitatakiwa kuongeza mtaji pale itakapotokea chama husika mtaji wake kuanza kupungua. Vile vile, inaweka muda kwa vyama hivyo kuwa na mkaguzi wa hesabu kwa kipindi kisichozidi miaka mitatu.

Vikoba navyo vimewekewa kanuni za kuhakikisha kuwa vinakuwa endelevu na vinatoa huduma katika mazingira ya uwazi, tofauti na kabla ya kuja kwa sheria hiyo mpya.

Zahara Msangi, mjumbe wa kikosi kazi cha uhamasishaji wa sheria mpya kutoka Tamisemi, ambayo imekasimiwa mamlaka na BoT kusimamia vyama hivyo, anaeleza kuwa kanuni ya 18 inaziruhusu Mamlaka za Serikali za Mitaa kukifutia usajili chama chochote kilichosajiliwa na kukaa muda mrefu bila kutekeleza majukumu.

Kanuni pia zinavikataza vikundi hivyo kuwa na matawi, haviruhusiwi kupokea amana na vinatakiwa kufungua akaunti benki kwa ajili ya kumbukumbu, tofauti na sasa ambapo fedha za wanachama zinatunzwa katika akaunti binafsi au kwenye vibubu.

Msangi anafafanua zaidi kuwa chini ya sheria hii, Vikoba vinatakiwa kuwasilisha taarifa serikalini kila robo mwaka, kutakiwa kufanya uchaguzi wa viongozi, kitu ambacho hakifanyiki sasa, hivyo kusababisha baadhi ya wanakikundi kuwa viongozi wakati wote, na matokeo yake kukosekana uwajibikaji na vikundi kufa.

Kanuni pia zinaitaka mamlaka (Tamisemi) kufuatilia vikundi kwa kuangalia changamoto na kujiridhisha na uendeshaji wa shughuli zao.

Mayosa anasema kuwa kuna adhabu kadhaa zilizoainishwa kwa wale ambao watakwenda kinyume cha sheria hii. Kwa mfano, upande wa Saccos ni faini ambayo si chini ya Sh. milioni 10 na si zaidi ya Sh. milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka miwili na isiyozidi mitano. Upande wa Vikoba faini si chini ya Sh. milioni moja au isiyozidi Sh. milioni 10.

Sheria hii imekuja wakati mwafaka, ambao makundi mengi ya jamii yanahitaji huduma za sekta ndogo ya fedha ambazo zina uwazi, kuaminiana na zinazotambulika. Kinachotakiwa ni kwa watoa huduma kuomba leseni ambayo itakuwa inatolewa ndani ya siku 60 na vikundi vya Vikoba kuomba usajili na kusajiliwa ndani ya siku 14.

Jambo la msingi na muhimu ni kwa kikosi kazi kutoa elimu ya umma kwa wadau na umma kwa ujumla ili kuwapo uelewa kuwa lengo la sheria hii ni zuri la kutambuliwa kwa sekta, kusimamiwa, kuendelezwa na kuwalinda watumiaji na watoa huduma.

Habari Kubwa