Shujaa panya Magawa

15Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Shujaa panya Magawa
  • *Kazi yake imeokoa maelfu ya watu
  • *Dunia yaomboleza kifo chake

NI nadra kusikia kifo cha mnyama kinaombolezwa dunia mzima. Pengine panya kutoka Tanzania anayeitwa Magawa, ameweka historia kwa kuwa maarufu na kifo chake kuombolezwa duniani kote.

Panya huyo mkubwa anayetambulika kama shujaa, alitumika kutafuta na kutegua mabomu ya ardhini na vilipuzi vingine katika nchi zilizokumbwa na vita.

Kifo cha Magawa kiliwashtua watu wengi na katika muda mfupi baada ya kutolewa tangazo lake, mitandao ya kijamii ilivamiwa na watu kwa ajili ya kuomboleza na kusifia kazi yake iliyotukuka.

Taarifa ya kifo chake ilitolewa katika ukurasa wa instagran unaomilikiwa na shirika la Apopo ambalo linaendesha mradi wa utafiti wa panya katika Chuo Kikuu cha Sokoine mkoani Morogoro.

“Magawa alikuwa na afya njema wiki jana, lakini afya yake ilianza kudhoofika mwishoni mwa wiki hii na kuaga dunia akiwa na umri wa miaka minane,” ilisema taarifa hiyo.

Katika uhai wake, panya huyo alisaidia kugunduliwa kwa zaidi ya mabomu 100 ya kutegwa ardhini nchini Cambodia.

Kutokana na mchango wake huo na kunusuru maisha ya maelfu ya watu, Septemba 2020, alikabidhiwa Medali ya Dhahabu ya PDSA, ambayo ni tuzo ya juu zaidi ya ushujaa ambayo mnyama anaweza kupokea.

Hata hivyo, mwaka jana Magawa alistaafu na panya mwingine anayeitwa Ronin alichukua nafasi yake.

Pamoja na kuzaliwa na kukulia Tanzania, panya Magawa alikufa akiwa nchini Cambodia na mazishi yake yalifanywa hukohuko.

SIRI YA PANYA MAGAWA

Kulingana na watafiti kutoka Apopo, panya huyo mkubwa kutoka Afrika, alikuwa na uwezo mkubwa wa kubaini mabomu ya kutegwa ardhini.

Magawa ameweza kunusa mabomu 70 na silaha 38 ambazo hazijalipuka katika maisha yake.

Shirika la matibabu ya wanyama la Uingereza lisilokuwa la kiserikali (PDSA) lilimtuza medali ya dhahabu kutokana na kujitolea kwake kuokoa maisha kupitia kazi yake ya kubaini mabomu hatari yaliyotegwa ardhini nchini Cambodia.
Ndani ya nchi hiyo, inadhaniwa kuna mabomu zaidi ya milioni sita yaliyotegwa ardhini.

Panya huyo ambaye ana umri wa miaka nane mpaka anapoteza uhai wake, alipewa mafunzo na shirika lisilo la kiserikali la Apopo kutoka Ubelgiji, makao makuu yake yapo Tanzania. Shirika hilo limekuwa likiwalea wanyama wanaofahamika kama Panya buku ambao wana uwezo wa kugundua uwepo wa mabomu ya kutegwa ardhini.
Wanyama hao wanafuzu baada ya kuwapa mafundisho.

Ofisa Mkuu Mtendaji wa Apopo, Christophe Cox, amesema kifo cha Panya Magawa kimewapa nguvu ya kuwafundisha wengine, mpaka sasa wana panya 20 ambao wameanza kufundishwa na wanaonyesha matokeo mazuri.

Kulingana na Apopo, Magawa alizaliwa na kulelewa Tanzania akiwa na uzani wa kilo 1.2 na urefu wa senti mita 70.

Japo ni mkubwa kuliko spishi zingine za panya, Magawa ni mdogo na mwepesi kiasi kwamba hawezi kulipua mabomu akitembea juu.

Panya hao wanafundishwa kubaini kemikali iliyotumiwa katika vilipuzi, wanaweza kunusa na kugundua mabomu kwa haraka zaidi.

Magawa peke yake alikuwa na uwezo wa kusaka mabomu katika eneo lenye ukubwa wa uwanja wa mpira wa tenesi kwa muda wa dakika 20 pekee, jambo ambalo Cox anasema lingemchukua mtu mwenye kifaa cha kubaini vifaa vya chuma kati ya siku moja hadi nne.

Ili aweze kufuzu mafunzo, panya inawachukua takriban mwaka mmoja kabla ya kuwa na uwezo wa kugundua mabomu yaliyotegwa ardhini.

Panya huyo alikuwa na uwezo kutumia saa moja na nusu kwa siku nyakati za asubuhi kufanya kazi.

Mkurugenzi Mkuu wa PDSA, Jan McLoughlin anasema kazi yake katika shirika la Apopo ilikuwa ya kipekee na ya kuridhisha.

"Kazi ya Magawa imeokoa na kubadilisha maisha ya binadamu ambao wanaathiriwa na mabomu hayo ya kutegwa ardhini. Kila uvumbuzi alioufanya umepunguza hatari ya kujeruhiwa au kufariki kwa watu." anasema.

Kwa mujibu wa shirika lisilokuwa la kiserikali la kuondoa mabomu nchini Cambodia ( HALO Trust), zaidi ya watu 64,000 walijeruhiwa na wengine 25,000 kukatwa viungo vya mwili kutokana na milipuko ya mabomu ya kutegwa kuanzia mwaka 1979.

Habari Kubwa