SHUWEA SALUM:Kutembeza uji mitaani kumempaisha mjini Mtwara

26Feb 2016
Juma Mohamed
Mtwara
Nipashe
SHUWEA SALUM:Kutembeza uji mitaani kumempaisha mjini Mtwara

KATIKA simulizi ya kawaida, kumshuhudia mjasiriamali mdogo anayemiliki ardhi yenye thamani au kuwa na jengo kubwa katika miji mikubwa huonekana ni jambo gumu na hasa mmiliki akiwa na biashara ndogo kama uji.

Shuwea Salum ‘Mama Uji' akiosha vitendea kazi vyake baada ya kumaliza biashara. (PICHA: JUMA MOHAMED).

Katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, mtu akimiliki kiwanja au jengo naye ‘huangaliwa mara mbili’ na wenyeji wa mji kwa maana ya kwamba amefanikiwa kimaisha.

Miongoni mwa watu hao ambao katika orodha ya maisha wameweza kumiliki mali kadhaa katika Halmashauri ya Manispaa Mtwara – Mikindani, ni Shuwea Salumu au maarufu kama ‘Mama Uji’ mjini Mtwara.

Huyo ni mjasiriamali maarufu anyeendesha shughuli zake katika eneo la Ligula, mahali kunakozungukwa Uwanja wa Michezo wa Nangwanda Sijaona.

Mbali na biashara ya kuuza uji ambayo kwa wengi huonekana ni ‘ubangaizaji wa kimasikini’ lakini katika tafsiri ya ukweli wa mafanikio yake amepiga hatua yasiyofanana na biashara yake ya uji.

Biashara ya uji wa ulezi inayofanywa na Shuwea, anaiendesha kwa kuitembeza mtaani, jambo lililompa umaarufu wa jina hilo la ‘Mama Uji.’

Shuwea anasema alianza kufanya biashara ya uji miaka sita iliyopita katika katika eneo la Nangwanda, akianza na bei ya kikombe kimoja Sh.200 na kisha alipandisha hadi Sh. 300 na sasa ni sh. 500. Anatoa sababu za kupanda gharama za mahitaji ya kuandaa uji.

Sasa Shuwea si yule aliyeanza miaka sita iliyopita. Anatamba yumo katika orodha ya wakazi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wanaoanza ujenzi wakati wowote, huku akishandaa vifaa na mahitaji kamili ya ujenzi.

Mbali na ujenzi, Shuwea ambaye ni mama wa watoto watatu anataja mengine ni namna anvyomudu kulipa ada za watoto hao, mmoja akiwa amehitimu kidato cha nne mwaka jana, mwingine amejiunga kidato cha wa mwisho anasoma daras la kwanza.

“Kipindi ambacho biashara ilikuwa nzuri kwa siku ilikuwa narudi na Sh.40,000 lakini kwa sasa hivi nimepunguza kipimo kutokana na uchumi wenyewe umeshuka na pesa imekuwa ngumu, hivi sasa narudi na Sh. 25,000 au ikizidi sana Sh.30,000,” anasema Shuwea.

Anaongeza kuwa: “Ulezi nasaga tu unga kama kilo 20 hivi, natumia muda wa wiki mbili. Kwa siku nauza chupa 10 ambazo zinaingia vikombe saba, nauza na maandazi. Sina biashara nyingine zaidi ya uji.”

UNDANI WA BIASHARA

Anasema katika nyendo za biashara yake anakutana na wateja wenye kila aina ya tabia, njema na mbaya ambazo kuna wakati zinakwaza biashara yake.

Shuwea anasema kuna baadhi ya wateja wakorofi hata anaingia mgogoro nao katika suala la malipo wakilazimisha kutomlipa.

Ili kuepuka rabsha hizo za nafsi na kibiashara, anasema kuna wakati analazimika kukwepa kuwapitishia huduma ya uji anaouuza.

Sababu ya kujikita katika ujasiriamali huo wa kuuza uji, Shuwea anasema ni mtihani wa kimaisha uliompata baada ya kuachika katika ndoa na biashara ilikiwa jaribio la kuishi bila ya kumtegemea mume.

“Wakati nimeanza ni pale baada ya kuachika na kuona ugumu wa maisha ndio nikaona nianze hii biashara, yaani kujaribu kama nikifanya hii biashara je nitauza au…

“Lakini baadae nikaona nina wateja na hapa Umoja (Nagwanda) nilipoanza, sijui kulikuwa na mabanda matano tu ndio yalikuwa yamefunguliwa.

“Hakukuwa na watu wengi, kwa kweli kama ilivyokuwa sasa hivi. Nilianza na uji chupa mbili kabla ya sasa kufikia hizo chupa 10” anatamka Shuwea.

MATARAJIO

Dira yake ya baadaye, anasema ni kubadiisha biashara kwa kuuza nguo za kike aina ya Madera ambazo atakuwa akizifuata jijini Dar es Salaam na kwenda kuziuza vijijini Mtwara.

Shuwea anasema kuwa baada ya
kuachika katika ndoa mbili tofauti akieleza katika ‘mazingira magumu na kunyanyasika’kwa sasa hafikirii kuolewa tena hadi afikie hatua anayoieleza kuwa “atakapojiridhisha” na “kujiweka sawa kimaisha” ili aingie katika ndoa akiwa binafsi amesimama vyema kiuchumi.

“Hivi sasa kwa sababu nilishapata changamoto za wanaume kunitelekeza, sitokubali mpaka pale nitakapofanikisha malengo yangu,” anasema na kuongeza:

Charles George, ambaye ni Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (Mtwarefa), ni mteja wa Mama Uji anayesifu huduma na ubora wa uji wake, mvuto wake unawafikia watu wengi.

CHANGAMOTO

Licha ya jitihada za Shuwea ‘kutoka’ katika biashara kupitia kupitia mauzo ya uji, anasema anakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa kukosa ofisi ya kuendeshea biashara yake.

Pia, anasema kutokana uhalisia wa amekosa msaidizi wa kumshikia biashara pale anapopatwa na dharura na jitihada zake zinakwamishwa na kila anapoomba msaidizi, wengi wanakwepa kukubali wakuona ni kazi ya aibu.

Pia, Mama Uji anakiri hajawahi kuhudhuria mafunzo ya aina yoyote kuhusu ujasiriamali.

Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF Kanda ya Kusini, Kwame Temu, anasema kutakuwepo programu maalumu ya kukutana na wadau wa sekta zisizo rasmi, wakiwamo wajasiriamali wadogo inayomfaa Mama Uji.

Habari Kubwa