Si ya kuogopa, hayana sumu wala magonjwa…

16Mar 2019
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Si ya kuogopa, hayana sumu wala magonjwa…

MAINI ni kitoweo ambacho huenda hakina walaji wengi. Hilo halina mjadala liko wazi kwa wengi wetu, huenda pengine ni kutokana na bei kubwa kwenye mabucha au kuyahofia kuwa yana madhara.

Hata hivyo, mtazamo wa mjadala unajitokeza kwenye usalama wa afya kwa mlaji una pande mbili, baadhi wanasema hayafai na wengine wanakinzana na hoja hiyo kwa kuyala bila hofu wakiyatumia kila wakati.

Je, hoja hizo zinzowagusa walaji wa nyama, wapi pa kusimamia? Hapo ndipo mtaaluma bingwa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Nyama Tanzania, Profesa Philemon Lekule, anasema, maini ni chakula bora na muhimu kwa binadamu na hasa kwa kina mama wajawazito kwa sababu ya wingi wa virutubisho.

“Yamejaa protini, vitamini A na B12, madini ya chuma (Iron) ambayo ni muhimu kutengeneza damu na phosphorus, hivyo hukinga mwili na ukosefu wa damu (anaemia),”anasema Profesa huyu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).

Anaongeza kuwa maini ni muhimu husaidia kizazi, kwa hivyo maini hasa ya ng'ombe, kondoo na mbuzi ni bora sana kwa afya ya Mtanzania.

JUKUMU LA INI
Jambo kubwa linalowaogopesha watu kula maini ni madai kuwa yanatunza sumu na pia magonjwa yote mwilini yako ndani ya kiungo hiki mtaaluma anayatolea maelezo.

Mtaalamu huyu anasema kazi kubwa ya maini ni kuzalisha nyongo (bile) inayotumika kuyeyusha chakula. Aidha, yana jukumu la kuondoa lehemu mwilini na pia husafisha na kuondoa dawa na sumu mwilini.

Profesa Lekule anasema maini husaidia kumeng’enya protini, wanga na mafuta na pia ina jukumu la kutoa protini zinazogandisha damu kwenye majeraha.

Hivyo kama una upungufu wa madini au vitamin hizo unashauriwa kula maini. Lakini, anaonya kuwa ukila maini kwa wingi sana mfano kila siku inaweza kukusababishia kupata virutubisho hivyo kwa wingi mno vikazidi kiwango.

“Pia unaweza kula lehemu nyingi kutokana na maini kuzalisha lehemu na pia mabaki ya sumu iliyokuwa inaondolewa mwilini kama itakuwa imo ndani ya kitoweo hicho.” Anaonye mtaalamu huyu wa mifugo na nyama.

Anakanusha kuwa siyo kweli kuwa ukila maini unakula sumu na magonjwa ya mnyama awe mbuzi, kondoo, ng’ombe au kuku.

“Tahadhari ninayotoa tu hapa ni kwamba kwa ajili ya kuzuia gauti "gout" au maradhi ya ‘jongo’ ambayo inawasumbua sana wanaume uzeeni ni vizuri kujizua kula kwa vingi utumbo, maini na figo,” anatahadharisha msomi huyo.

MAINI KUTUPWA

Swali mojawapo ambalo wapinga ulaji wa maini wanaliuliza ni madai kuwa Ulaya na nchi zilizoendelea wanatupa maini inakuwaje yawe salama kwa Mtanzania?

Mtaalamu huyu anajibu kuwa siyo kweli kuwa Ulaya au mataifa yaliyoendelea maini hayaliwi bali kutupwa.

“Ulaya kwa kawaida yao, ‘offals’ au nyama za utumbo, figo, maini hutumika tofauti na hapa kwetu. Hutumiwa kutengenezea vyakula maalumu au vya binadamu ama vya mifugo. Haviuzwi kama nyama mfano inavyofanyika hapa kwetu kwenye mabucha.”

Anataja mfano wa maini ya nguruwe kuwa huko Ulaya yanasagwa na kutengenezwa siagi kwa ajili ya kutumiwa kwenye mikate.
Anaeleza kuwa mara nyingi Ulaya hawatumii nyama ya mbuzi, wanakula zaidi ya kondoo, hivyo ni mila na jadi yao kwa hiyo isiwaogopeshe watu kula maini.

CHANZO CHA MARADHI?
Profesa Lekule anakumbusha kuwa maini yote yenye minyoo na ugonjwa iwe minyoo ya ‘liverflukes’ au ugonjwa mwingine popote pale hutupwa wakati wa kukagua nyama machinjioni.

Anasema hizo ni taratibu za kawaida kila mahali duniani na kusisitiza kuwa maini ni chakula bora na Watanzania wanastahili kutumia kitoweo hicho.

Gazeti hili lilizungumza na Dk. Engelbert Bilashoboka, Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Chakula (TFDA) Kanda ya Kati, kuhusu maoni yake kulingana na hofu ya watu waliyo nayo kuhusu ulaji wa maini.

Kama alivyosema Profesa wa SUA, pia naye anakanusha kuwa maini ni kitoweo hatari na kusisitiza kuwa si nyumba ya magonjwa kama ambavyo watu wanadhani wakiogopa kuwa endapo watayatumia watapata magonjwa, badala yake anasema ni kitoweo bora.

Anafafanua kuwa nyumba ya magonjwa inaweza kuwa ni sehemu yoyote ya mnyama mwenye maradhi na si kwenye maini. Hakuna mnyama anaweza kuishi na ini lenye magonjwa.

“Magonjwa yanayokutwa katika maini ni minyoo ya maini (fasciolosis) ambayo huyaharibu na kuyafanya magumu lakini haina madhara kwa binadamu,” anasema Dk. Bilashoboka.

Pili kuhusu maini kuwa na sumu anaeleza kuwa maini yanachuja sumu na ukweli ni kwamba yatakuwa hatari pale ambapo muda uliopangwa wa kuzuia mnyama kuchinjwa tangu alipochomwa sindano ya mwisho au tangu aliponyweshwa dawa ya mwisho hautazingatiwa.

“Ini linahitaji muda wa kuvunja sumu na ikishavunjika huchujwa na figo kama muda usipozingatiwa ini litakutwa na sumu jinsi ilivyo kabla ya kuvunjika,” anaonya mtaalamu huyo.

Anasema ni kitoweo salama kama mmiliki wa mnyama atazingatia muda wa kumzuia asichinjwe mpaka dawa iishe mwilini au kwa kitaalamu ‘drug withdrawal period’ na kuwashauri wanawake wajawazito, watoto na wenye upungufu wa damu kula kitoweo hicho.

MAINI VS MATEMBELE
Wakati wataalamu wanasisitiza usalama wa maini na kueleza kuwa ni chanzo cha lishe bora kwa wajawazito, wagonjwa na watoto ili kuwahakikisha damu ya kutosha, vitamin na chumvichumvi, baadhi ya wanawake Dar es Salaam wanaogopa maini na kukimbilia matembele.

Baadhi ya wajawazito waliliambia gazeti hili kuwa matembele huongeza damu kwa kasi ya ajabu kuliko maini. Huenda ni jambo walililoaminishwa ambalo linatakiwa kufafanuliwa kwenye kliniki za mama na mwana.

Wanadai kuwa wanayakaanga kwa muda mfupi au kuyachemsha na maji ya moto kidogo na kuyala au kutengeneza juisi yake. Hata hivyo, pamoja na ubora wake kiafya maini huuzwa ghali kati ya Sh. 8,000 na 10,000 kwa kilo na kuwa kitoweo cha familia zenye uwezo mkubwa kiuchumi.

Habari Kubwa