Si Zuma peke yake anayejitanua kwa kumlalia mlipa kodi

06Apr 2016
Hekima Akilimali
Nipashe
Si Zuma peke yake anayejitanua kwa kumlalia mlipa kodi

KATIBA aliyojaribu kuikiuka na kuibeza ndiyo inayotoa fursa kwa rais wa Afrika Kusini wa sasa, Jacob Zuma, kubanwa mithili ya uchungu wa kuzaa na hata kuhatarisha kuendelea kubaki kwake madarakani.

rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma.

Hii ni kwa sababu kuna jitihada za kumwondoa madarakani kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu zaidi Afrika Kusini kumtia hatiani Rais Zuma kwa ukiukwaji wa sheria na maadili juu ya namna alivyokarabati kiunga chache kimoja vijijini.

Rais Zuma aliyekuwa akijibu au akijibiwa na wasemaji wake kwa kiburi na kujiamini kuwa yeye hajakosa, kuwa yeye ndiye rais kuwa yeye hagusiki na haathiriki na wahasimu wake wanaomlilia wivu sasa kabadilika. Akihutubia taifa, rais Zuma hafla alijawa na unyenyekevu mpya.

Hafla alifahamu kuwa akijikwaa tu katika namna ya ‘kudhibiti uharibifu’ uliotokea kutokana na maamuzi yake ya kupenyeza mkono katika hazina ya kodi akatumia kwa matumizi yake binafsi si katika yale mambo aliyoruhusiwa kufanya kikatiba kumemtia katika sufuria la supu na kukaangwa.

Bila shaka atakuwa naye anaonja machungu aliyomsilibu rais Thabo Mbeki kutokana na uchu wake wa kushika madaraka akaona mwenzake hafai yeye ndiye anafaa kuliendesha taifa la Afrika Kusini.

Hivyo, akafanya kishindo ndani ya chama kumtoa Mbeki na kujisimika yeye uongozi wa nchi na wa chama akiweka ‘marafiki na wabia wake’ kwenye nafasi nyeti. Nchi ikaanza kupoteza mwelekeo wa kiuchumi na hata kimaadili rais akihusishwa na baadhi ya utovu wa maadili.

Chama kilizidi kusambaratika na rais Zuma akajaribu kuwang’oa wale wote aliohisi wanapinga sera na mwenendo wake. Hata Julius Malema, kiongozi maarufu wa vijana wa chama tawala aliyemsaidia katika dhamira yake ya kumwondoa Mbeki akafanyiwa vitimbi na kuwekwa kando.

Tukumbuke kuwa moja ya mashtaka dhidi ya Malema pia alishutumiwa kwa kupokea milungula ambayo yalimwezesha kukarabati ‘kijumba chake’ hapo mjini kuwa ya kifahari.

Ushahidi wa picha ukasambazwa watu wajione na labla iwe rahisi kumhukumu na kumfungulia Malema kesi yake ilipofikishwa mahakamani.

Kumbe yale yale aliyomtuhumu mwenzake kumbe na yeye ana kilema kile kile. Hivyo, wakati tunasubiri kuona suala hili litafikia wapi tuchukue wasaa na kutambua kuwa tunachokishuhudia sasa Afrika Kusini si kitu kigeni na kinaonekana katika nchi nyingi ikiwamo hapa kwetu.

Kwa mfano, suala zima la Zuma kupatikana kajaa mashizi yanayoashiria alifunua chungu jikoni na hata baada ya baadhi ya wale aliotaka kuwagawia nyama iliyodokolewa kuja mbele na kumshtumu kuwa mikono yake na kinywa chake si kisafi, chama tawala kimejitokeza kifua mbele kumtetea bila kupepesa.

Hali hii inanikumbusha yanayojiri hapa nchini hasa pale taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) inapofichua dalili au matukio halisi ya ulaji au ufujaji au upotevu wa fedha za walipa kodi.

Mara ngapi tumeshuhudia wabunge, wakuchaguliwa na wakuteuliwa, kutoka chama tawala wakiweka kando matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kusimamia na kutetea maslahi ya nchi na kuwa wazalendo na badala yake wakatetea maslahi binafsi ya baadhi ya wanachama wao ‘wajanja’ wanaotuma chama kama kichaka cha kufanya uhalifu wa kibiashara.

Kinachoisaidia Afrika Kusini ni uwepo wa Katiba ambayo imejaribu kuweka miundo na mifumo ya kusimamia na kufuatilia utendaji wa serikali na kuvipa vyombo husika meno na uhuru wa utendaji wakiongozwa na katiba na sheria za nchi.

Suala hili la kuwa na meno ya kuwajibisha au pale panapostahili kutenda ili kuhakikisha nafuu ya ukiukwaji sheria au taratibu unapofanyika ni jambo ambalo hapa Tanzania wabunge (na walioitawala Tanzania kwa njia rasmi na si rasmi), kamwe hawalikubali.

Tukumbuke namna suala hili kila linapoibuliwa linazimwa kwa sababu zisizo na mashiko alimradi serikali daima ijilinde hata kama inayoyafanya ni maovu au jinai kubwa.

Tume ya Utawala Bora na Haki za Binadamu, kwa mfano, unahitaji si tu meno, lakini pia pingu kutokana na ukweli kuwa taasisi nyingine zilizotizamiwa kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha utawala wa sheria kama polisi nao wanahusishwa na matukio makubwa ya uvunjaji haki za nchi na zile za binadamu.

Hili halina mjadala na limemulikwa vya kutosha na taarifa rasmi ya Tume kila mwaka pamoja na taarifa ya mwenendo wa Haki za Binadamu inayochapishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu pamoja na Kituo cha Sheria Zanzibar.

Kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake, tunamsikia Mwenyekiti wa Tume za Utawala Bora na Haki za Binadamu akiyasemea matukio mengi ya uvunjwaji wa haki. Na wala si kama Mwenyekiti huyo anaropokwa tu au kutumwa na maadui, bali Tume yake imefanya utafiti sehemu mbalimbali za nchi kufuatilia ukweli wa shutuma dhidi ya ukiukwaji wa sheria za nchi jambo ambalo hata mahakama zetu hazifanyi kwa ufanisi.

Mwisho wa juma lililopita, kulivuja taarifa kuhusu ‘kurasa za Panama’, orodha ya vigogo na washirika wao wanaohamisha fedha za wananchi au utajiri wao uliopatikana katika nchi husika, lakini wakauhamisha kwa madhumuni ya kukwepa kodi na hivyo kuinyima serikali fedha.

Hivyo, zile taarifa zilizowahi kutolewa na Benki za Uswiss kuhusiana na fedha zilizotoroshwa hapa Tanzania au yale matukio ya fedha nje za madikteta kama Mobutu na Abacha bado hayajakoma ndio kwanza yanashamiri.

Wanaharakati na wachambuzi wa mambo wanapotaka mfumo wa utawala na wa uwajibika ufanyiwe marekebisho ya msingi basi huu ndio ushahidi wenyewe. Haiwezekani kitu kile kile kikatokea mara kwa mara katika sehemu tofauti kisiashirie matatizo ya msingi na muundo au mfumo wa jambo. Na hili tunaliona si tu katika uwanja wa siasa na uchumi, lakini pia katika nyanja ya utawala.

Inakuaje asilimia kubwa ya marais katika kanda hii wakang’ang’ania madaraka kama vile roho zao zitaishi milele na wao ndio ‘wateule wa kudumu’ wa Mwenyezi Mungu? Inakuaje kuwa matukio ya ubadhirifu, ya ufisadi yanafanana kote labda utabadilisha wahusika tu, lakini maudhui ndiyo yaleyale? Inakuaje kuwa baada ya mchakato wa kuweka mifumo ya sheria na utawala barani Afrika na pia katika nchi husika wale walioapa kuisimamia katiba na sheria za nchi wamejitwisha mamlaka na madaraka yasiyohijika na yaliyojuu ya Sheria ya Msingi ya nchi?
Hakika Zuma hayuko peke yake na aibu hii si tukio la ajali; au jambo linalohusua Afrika Kusini tu.

Ni dalili ya ombwe la uongozi nchini. Pia ni hali halisi ya utawala katika nchi nyingi zinazozama katika uliberali wa kiuchumi bila ya kuwa na msingi thabiti wa kitaifa au nia njema ya kuvusha taifa na watu wake kufikia ustawi na neema.
Longa, haya si shere!

Habari Kubwa