Siasa iwekwe kando suala la machinga, mama lishe

31May 2021
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Siasa iwekwe kando suala la machinga, mama lishe

WIKI iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alitoa maelekezo ya kuwa na utaratibu wa wafanyabiashara ndogo maarufu kama machinga, na mama lishe ili kuhakikisha jiji limepangika.

Agizo hili limekuja kwa wakati mwafaka kwa kuwa jiji la Dar es Salaam, sasa linaonekana chafu na halina mpangilio kwamba mtu yeyote anaweza kufanya biashara kokote bila kuulizwa na yeyote na kutolipa kodi yoyote.

Kwa sasa njia za watembea kwa miguu hazipo ndiko wafanyabiashara hao wamejaa na mbaya zaidi walirudi hata katika maeneo wasiyotakiwa kama Posta, na kubwa ni siasa kupewa nafasi kubwa kuliko uhalisia, kwamba hawa ni wapiga kura wasibugudhiwe.

Ukienda Kariakoo idadi ya machinga imeongezeka kiasi kwamba hakuna pa kupita, na wamepanga bidhaa zao nje ya maduka, wateja wengi wadogo wanaishia kununua kwao huku wenye maduka ndiyo wanaolipa kodi.

Ukienda Mwenge idadi inaongezeka kiasi kwamba kwa sasa hakuna sehemu za maegesho ya magari, huku maeneo ya watembea kwa miguu yaliyojengwa hivi karibuni kutokana na upanuzi wa barabara ya Mwenge Morocco wameshajaa.

Ukienda Mbagala ndiyo kabisa wamejipanga hadi eneo la katika la hifadhi ya barabara na huku maeneo ya watembea kwa miguu yakimezwa yote.

Hali hii siyo ya kuridhisha kabisa kwani jiji linakuwa na miavuli au mifuko ya nailoni mingi iliyosambazwa ili kupata kivuli huku usiku wakisambaza umeme ili kupata mwanga, jambo ambalo ni hatari.

Wafanyabiashara wenye maduka wanalipa kodi, lakini wanashindwa kufanya biashara kiasi kwamba baadhi wamefunga maduka na kugeuza kuwa stoo za kuhifadhi mizigo, ambayo husambazwa kwa wafanyabiashara ndogo na sasa ile kodi ambayo serikali ilikuwa inapata haipati tena.

Ni muhimu sana kukawa na utaratibu kwa kuwapanga wafanyabiashara hawa kwa kuwa siyo kweli kuwa wanaruhusiwa kufanyabiashara zao kila mahali, ni lazima kuwe na nidhamu ya ufanyaji biashara, na siyo kwamba wakifanya hivyo ndiyo wapiga kura wazuri.

 

Haya yalifanyika kwenye mapito ya wanyama na maeneo ya mtawanyiko, ambayo yanapotea kwa kuwa vimesajiliwa vijiji, kufunguliwa mashamba na ofisi za serikali, kwa kisingizio cha wapiga kura.

Hali hii iko katika miji yote, na wakati utaratibu unafanyika ni muhimu kufungananisha sekta kama miundombinu mizuri na nishati, ili kuongeza mzunguko wa biashara kwenye miji midogo kwa ajili ya kupunguza wimbi la vijana wanaokimbilia mjini.

Mathalani, ukitembelea soko la Mabibo, Buguruni, Kariakoo na kwingine kuna idadi kubwa ya wavulana wanauza mifuko na kubeba mizigo, baada ya muda hao ndiyo hugeuka kuwa machinga na kuanza kupanga bidhaa kando ya barabara.

Kwa sasa masoko mengi yana idadi kubwa ya wafanyabiashara walio nje ya soko, mathalani soko la Mabibo licha ya miundombinu duni, lakini kwa sasa wafanyabiashara wanaanzia kwenye mchepuko wa barabara ya mwendokasi na wamefungua vibanda na kujaza mazao.

Kwa ujumla serikali inapoteza mapato mengi kwa kuruhusu watu hawa kuongezeka, na wapo ambao hawakubali kuonyesha wamekuwa kibiashara kwa kuwa wanajua kinachofuata ni kulipa kodi.

Agizo la kuwapanga ni muhimu sana likatekelezwa hata kwa kujifunza nchi nyingine ambazo zimefanikwa, kwamba waliweka kando siasa ya kwamba hawa wasibugudhiwe ni wapiga kura.

Ukitembelea Jiji la Bangkok, Thailand, wametenga maeneo ya mama lishe ambao wapo kwenye jengo kubwa katikakati ya mji, huku kwenye mitaa kuna eneo maalum na siyo kila mtu kujipangia bidhaa au kuanza kuuza chakula pale anakoona yeye kunafaa.

Pia, kwa machinga wamepanga vizuri sana kiasi kwamba unaingia kwenye jengo kubwa lina machinga wa kila aina, na ndicho kinatakiwa kufanyika kwamba Kariakoo kuwe na maduka ya wauzaji wakubwa na machinga ambao wako kwenye eneo moja.

Hali ya sasa inaumiza nchi kwamba wale wanatakiwa kufanyabiashara ili walipe kodi wanashindwa na sasa kuna ujanja wa kufunga maduka na kubaki na stoo ya kuhifadhi mizigo inayosambazwa kwa machinga, hali ikiachwa hivi siyo sawa.

 

Jiji la Dar es Salaam linapaswa kupangwa na ndiyo itakuwa mfano kwa miji na majiji mengine, kuacha hali ilivyo ni kuharibu muonekano ambao siyo lazima mgeni atembelee bali akiwa angani anaona jinsi tulivyokosa mpangilio.

Machinga ni Watanzania na wanahaki ya kutafuta kipato, lakini lazima kuangalia kasi ya vijana kukimbilia mjini, na kuhakikisha kuna kuwa na ukuaji sawa wa miji na majiji, na kujenga mazingira wezeshi kwa vijana kubaki vijijini kuzalisha na kupata mkate wa siku.

Wengi wanakimbilia mjini kwa kuwa ndiko kuna uwezekano wa kupata kipato, na bado shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji hazijajengewa mazingira wezeshi ya kuendelea kusalia waliko.

Mungu ibariki Tanzania