Siasa ni kama utani wa jadi uhasama ni wa nini?

25Mar 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Siasa ni kama utani wa jadi uhasama ni wa nini?

KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakumbusha kuwa hii ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia, inayozingatia haki ya kijamii na kwa hiyo-wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote na serikali inapata madaraka na mamlaka kutoka kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, picha mtandao

Kutokana na maelezo hayo ya katiba ni wazi kwamba nchi zote zinazozingatia uongozi wa kidemokrasia nguvu ya madaraka hutoka kwa wananchi.

Hii inamaanisha kuwa wananchi ndiyo wenye nchi ndiyo wanaowachagua viongozi kupitia sanduku la kura.

Kwa hiyo ni muhimu sana kuheshimu maamuzi ya wananchi na kuzingatia demokrasia. Kuzingatia demokrasia huko kutatokana na watu wote ndani ya nchi kuamini kuwa taifa halina mmiliki maalumu bali wamiliki ni raia wenyewe.

Ikiwa kila mmoja atatambua kwamba demokrasia ndiyo msingi wa maendeleo utakuwa ni mwanzo mpya wa kuepusha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na chuki zinazotokana na migogoro ya kisiasa.

Kuheshimu demokrasia ni kuwajengea watu uzalendo katika taifa, maana wataona hakuna sababu ya kupigana na kuiharibu nchi ambamo kila mmoja wao anaishi, badala yake wataungana kujenga na kupenda taifa lao.

SIASA KAMA SOKA?

Siasa si uadui tuifanye kama soka. Mathalani, siku ya mechi ya Simba na Yanga Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, licha ya kwamba mashabiki wa pande zote ni marafiki, wakati wa pambano kila mmoja hukaa upande wake.

Wakifika uwanjani wapenzi wa Simba hukaa kwenye jukwaa lao na wapinzani wao au Yanga hujipanga pia kwenye jukwaa lao na watashangilia timu yao kikamilifu kulingana na mafanikio.

Hakuna uadui mechi ikimalizika kwa kufungana, sare au kufungwa inakubalika, si suala la kuanzisha uhasama bali marafiki wanaoshabikia timu tofauti huendelea na maisha na kuheshimiana kama ilivyokuwa hapo awali.

Ndivyo unavyotakiwa kuwa uhusiano wakisiasa maana hizo ndizo timu au vyama tunavyovishangilia lakini haimaanishi kuwa sisi ni maadui hata kama tunaunga mkono chama tawala au upinzani.

Nimeutoa mfano huo wa mchezo wa mpira kwasababu inawezekana tayari watu wamejifunza kutokana na siasa za chuki tulizo nazo katika mechi zetu, kwamba adui yako mwombee njaa. Kuombeana njaa huko ni kutokana na chuki miongoni mwetu na chuki siku zote huwa na chanzo.

Hakuna sababu ya kuwa na chuki za kisiasa kwani ni matokeo ya mwisho ya uvumilivu yaani kwa kuwa umemshindwa basi unajaribu anagalau kuonyesha hasira zako kwenye chuki, ukikataa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kisiasa, kijamii na hata kiuchumi.

NDANI YA VYAMA

Leo tumeanza kuona chuki katika vyama vyetu vya siasa wako watu hawazungumzi kabisa wamekosana kutokana na ushabiki wa vyama vya siasa, wengine ndoa zimevunjika kwasababu ya ushabiki wa vyama vya siasa.

Kutoka nje zaidi, mathalani, uhusiano wa kisiasa katika Afrika unajengwa katika taswira hasi ambayo imeonekana kutukosanisha, kutufitinisha na kutuvuruga wananchi bila sababu za msingi.

Kwa mfano Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nigeria na DRC je, kuna sababu za msingi za kutofanya wananchi wa nchi hizo wasielewane na kuishi kwa amani kama ndugu na jamaa?

Wapo watu wanaosema kuwa vurugu hizo za kisiasa hazipo Afrika tu bali hata katika mataifa mengine duniani.Ni kweli baadhi ya nchi za Ulaya zina vurugu za kisiasa lakini hoja haina msingi kwa sababu huwezi kuhalalisha mabaya na maovu kwa sababu wengine hufanya hivyo.

Ifike mahali Waafrika waone aibu na wa kuondoa aibu hiyo si wengine bali ni sisi wananchi pamoja viongozi wetu ambao tayari tupo na siasa hizo zinafanywa na walioko madarakani. Wafahamu kuwa chuki hazijengi, uvumilivu na upendo baina ya mashabiki au wanachama ndilo jambo la msingi.

MANDELA NI KII

Aliyewahi kuwa Rais wa kwanza mweusi Afrika ya Kusini Nelson Mandela, pamoja na kwamba alifungwa gerezani kwa miaka 27 kwa sababu ya kupigania haki za watu weusi dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukandamizaji wa haki za binadamu hakuwa na chuki.

Alipotoka gerezani hakupigana na watesi wake wala kuwaadhibu. Baada ya kupata dhamana hiyo ya kuwa rais wa nchi mategemeo ya wengi hasa weusi wenyewe yalikuwa kulipa visasi kwa wale waliomfunga na kuwanyanyasa weusi.

Mandela hakufanya hivyo. Alitaka maridhiano, uvumilivu wa kisiasa na mshikamano wa kitaifa licha ya kufungwa miaka mingi gerezani , kuteseka na kunyanyaswa na makaburu.

Mandela hana tofauti na viongozi wengi wa Kiafrika ni kaka yao wanatakiwa tu kumwiga , waache kupigania maslahi yao binafsi badala yake wahudumu katika serikali kwa muda usiozidi miaka ule uliopangwa na katiba na kuachia madaraka kwa heshima, amani na utulivu.

Kama viongozi wa Sudani Omar al Bashir na Robert Mugabe wa Zimbabwe, wasingeumia na kukutana na sokomoko la nguvu ya umma inayotaka kuwaondoa madarakani.

Afrika iendelee kujifunza kwa Mandela mwenye busara na hekima ya hali ya juu na wakati wa uongozi na utawale wake hakutaka kulipa visasi kwa wale waliomtesa.

Badala yake baadhi yao alifanya nao kazi akiwa Rais nao wakiwa watendaji wake wa chini na kama angelikuwa ni mtu wa chuki, basi yangelifunguliwa magereza mengi ya makaburu pekee na kuwafunga humo na kama angelifanya hivyo , yeye pia angelikuwa kaburu tofauti yake na wao ingelikuwa ni rangi kwamba Mandela kaburu mweusi na wao makaburu weupe.

Viongozi wa Afrika ni lazima kukubaliana na kuamini kuwa utawala wa sheria na kuheshimu demokrasia havifanyika kwa hiari ni kwa mujibu wa katiba pekee. Hata hivyo si zama za kuamini kuwa wamezaliwa ili wawaongoze wengine na kwamba wao na watoto wao ndiyo watawala, kama inavyoendelea kwa baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki.

UTANI WA JADI

Wakati wa kuifanya siasa kama utani wa jadi umefika. Kwa maana kama wewe ni mshabiki wa timu ya Mtibwa Sugar ukumbuke utakapoiombea Simba ama Yanga isambaratike, Mtibwa itacheza na nani? Kama unaona faida na umuhimu wa kuwepo kwa Mtibwa Sugar vivyo hivyo itakuwa ni faida kuwepo kwa vilabu vingine kama, Simba na Yanga.

Maana huwezi kujitungia mtihani wewe mwenyewe na ukajisahihisha peke yako.

Katika moja ya machapisho yake Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema haya…“Pamoja na kwamba vyama ni vibovu, lakini vipo, kama vipo, basi muanze kujifunza maadili ya kuwa na vyama vingi na kama mna vyama vingi hampuuzi maoni ya wananchi’’ (Nyerere, J.K 1995 Nyufa).

Mwalimu alikuwa akisisitiza umuhimu wa kuvumiliana kisiasa huo haukuwa ujumbe kwa Tanzania pekee bali ni kwa bara zima la Afrika ambako bado kumekuwa na shida hasa kwenye kuzingatia demokrasia ambayo msingi wake mkuu ni wananchi wenyewe kuwa msingi wa kila jambo.

Demokrasia ikitendeka hakuna mtu atakaye kuwa na mawazo ya kishetani ya kusaliti ama kuiuza nchi kwa vipande vya fedha, mikataba mibovu ya madini na uwekezaji, ufisadi, uhujumu uchumi na ukandamizaji wa demokrasia wa aina yoyote.

Hivyo ni muhimu kuchunga demokrasia, uvumilivu wa kisiasa na kuendeleza utawala wa sheria katika nchi za Kiafrika ili kufikia azma ya kuwa na washirika wengi au vyama vingi vya kisiasa.

Habari Kubwa