Siasa za makundi CCM na hatima ya ‘team Lowassa’

25May 2016
Restuta James
Dar es Salaam
Nipashe
Siasa za makundi CCM na hatima ya ‘team Lowassa’

“KAMA ningeweka msimamo wa kukataa matokeo ya urais na kuwataka vijana na Watanzania wakatafute kura zao zilikokwenda, ni wazi kwamba nchi isingekalika,” ni kauli ya aliyekuwa mgombea urais, Edward Lowassa, akizungumza nyumbani kwake Monduli.

Katibu Mkuu CCM, Abdulrahman Kinana

Katika kauli hiyo aliyoitoa Jumamosi iliyopita, hakuficha azma yake ya kupeperusha bendera ya Chadema kwa mara ya pili kuwania kiti hicho, huku akijiamini kwamba hana shaka ya kuibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Ni hoja isiyohitaji mjadala kwamba msukosuko na msuguano katika kumpata mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM); na baadaye mchuano kati ya CCM na kambi ya upinzani kupitia bendera ya Ukawa na hata msuguano katika kambi ya upinzani; Lowassa ndio msingi mkuu.

Nani aliyetarajia Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba kujiengua ghafla, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa ‘kubwaga manyanga,’ au mkongwe wa Tanu aliyeasisi CCM akiwa na kadi namba nane, Komredi Kingunge Ngombale-Mwiru, akiongoza jopo la wana-CCM waandamizi akiwamo Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kujiunga na Ukawa wakiwa wana-Chadema?

Baadhi ya wana-CCM waandamizi alioambatana nao ni pamoja na Wenyeviti wa CCM wa mikoa; Mgana Msindai (Singida) na Khamis Mgeja (Shinyanga); Mawaziri Goodluck Ole Medeye, Makongoro Mahanga, bila kumsahau mwanadiplomasia aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Juma Mwapachu, ambaye hata hivyo amerejea CCM.

Ni wazi kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana umesababisha majeraha na makovu ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hii ni kwa sababu mchakato wa kupata wagombea wa nafasi mbalimbali kuanzia udiwani, ubunge na hata urais, ulighubikwa na mfumo wa kimakundi ambao umekuwapo ndani ya chama hicho kwa muda mrefu.

Sio tu uchaguzi wa mwaka jana, bali uhasama wa kuwania madaraka ulianza kujionyesha kuanzia kupata wawakilishi walioshiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, uliofanyika Desemba 14, mwaka juzi.

Wakati chama hicho kikiendesha kura za maoni ili kutafuta wawakilishi wake kulikuwa na malalamiko na manung’uniko ya kukiukwa kwa utaratibu ndani ya chama ili kubeba baadhi ya wagombea.

Manung’uniko yaliyoanzia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa yalikuwa kukosekana kwa daftari la mahudhurio ya wanachama walioshiriki kupiga kura. Kuanzia hapo ilionekana kwamba kura zilizopigwa hazikuwa halali au uchaguzi haukuwa huru wala wa haki.

Wakati sarakasi za kupata wagombea kwenye serikali za mitaa zikiendelea, chama hicho hakikuchukua hatua za maana kukemea mbinu ‘chafu’ katika kupata mgombea.

Kelele zikapigwa, mitandao na makundi yakajiimarisha kuelekea uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.

MCHAKATO WA URAIS
Hapa ndipo hasa CCM ilipasukia. Kwa utaratibu wa CCM, wanachama wanaojiona wana sifa za kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa wanaruhusiwa kuchukua fomu na kutafuta wadhamini kwenye mikoa mbalimbali.

Mwaka jana wanachama wa CCM 38 walichukua na kurejesha fomu za kuomba ridhaa ya chama kuwania nafasi hiyo.
Katiba ya CCM pamoja na mambo mengine, inaeleza kuwa Kamati ya Maadili ina jukumu la kuandaa taarifa kuhusu wagombea na kuipeleka Kamati Kuu (CC), kwa hatua zaidi.

Kazi ya CC ni kumsikiliza mgombea mmoja mmoja na kumuuliza maswali yasiyopungua matatu, kisha wajumbe hukaa na kupendekeza majina matano ambayo yanapelekwa Nec.

Hata hivyo, CC ilipelekewa majina matano na ikafanya maamuzi bila kuwaona wagombea wote 38 waliorudisha fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais na hata wagombea waliokatwa hawakuitwa kwenye kitengo cha maadili badala yake walihukumiwa bila kusikilizwa.

Utaratibu wa hatua kuanzia kwenye uchukuaji wa fomu, kutafuta wadhamini, kurejesha fomu na kuhojiwa kwenye Kamati Kuu umetumika ndani ya CCM tangu mwaka 1995.

Kukiukwa kwa utaratibu huo kuliibua mpasuko ndani ya Kamati Kuu kwa baadhi ya wajumbe waliokuwa wanamuunga mkono Lowassa, kujitokeza hadharani wakilalamika kuwa kanuni zimevunjwa.

Dk. Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa, waliutangazia umma kwamba hawakubaliani na kilichotendwa kwani kanuni za utendaji katika vikao vilivyotangulia Kamati Kuu zimekiukwa.

Kwamba ukiukaji ulitokana na Kamati Kuu kupatiwa majina matano, badala ya kupokea majina yote ya wanachama walioomba kuteuliwa, ili yenyewe ndiyo itoke na majina matano baada ya kuyafanyia uchambuzi.

Wajumbe hao walieleza kuwa waliuza kwa mwenyekiti imekuaje kanuni zinakiukwa, lakini hawakupata maelezo ya kuridhisha.

CC ilitakiwa kuwasilikiliza wagombea wote 38 waliorudisha fomu, kuwajadili na kutoka na mapendekezo ya majina matano kupeleka Nec; utaratibu ambao ulikiukwa.

Kwamba vikao vya vyombo mbalimbali ndani ya chama vimewekwa ili kutenda haki kwa wanachama wote na ndio maana kilichotokea Dodoma mwaka jana kilionekana kama ni dharau kwa wagombea waliochukua fomu na wanachama wote wa CCM.

Mmoja wa watu waliokosoa mchakato huo hadharani ni Komredi Kingunge ambaye alishauri kwamba chama hicho kikae meza moja kujadili kasoro zilizokuwa zimejitokeza ili kupata maridhiano.

Hata hivyo, Kingunge alieleza kutokuwa na tatizo na uteuzi wa Dk. John Magufuli pamoja na Mama Samia Suluhu Hassan.

Aliwatuhumu viongozi waandamizi wa CCM kuwa walikiuka ‘kwa makusudi’ katiba, kanuni na taratibu za chama kuanzia kwenye vikao vya Kamati ya Maadili, Kamati Kuu (CC) hadi Halmashauri Kuu (Nec).

Hata hivyo, alisema maamuzi ya Mkutano Mkuu uliopitisha Dk. Magufuli anayaheshimu kwa kuwa kasoro zilijitokeza CC na Nec.

Moja ya kauli za Kingunge ni kutaka wana-CCM wakae mezani kuzungumza kasoro zilizokuwa zimejitokeza, ili kujenga chama kilichokuwa kimepasuka.

Hata hivyo, CCM iliukataa ushauri wa Kingunge na hadi sasa hakuna kikao kilichowahi kujadili kasoro zilizojitokeza wala hakuna anayejua hatima kundi la Lowassa ndani ya chama hicho, akiwa ni miongoni mwa makada wenye nguvu na ushawishi mkubwa ndani ya CCM na nje pia.

Habari Kubwa