Siku 3 Waziri Mbarawa Mbeya, Songwe zavuna tumaini la maji

16Jan 2020
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Siku 3 Waziri Mbarawa Mbeya, Songwe zavuna tumaini la maji
  • Jicho la kiprofesa lanasa ufisadi

MIJI ya Mbeya na Songwe nchini ina vyanzo vingi vya maji, lakini wananchi wake hawapati huduma ya maji ya bomba, kwa kiwango kinachotakiwa kutokana na sababu mbalimbali.

Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa, akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa wilayani Kyela, ikiwa ni ishara ya kuzindua mradi wa maji utakaowanufaisha wananchi wa vijiji vinane vya kata nne za wilaya hiyo. PICHA: NEBART MSOKWA

Mojawapo ni kukosa ni baadhi ya makandarasi kuchelewa kukamilisha miradi wanayopewa na serikali na kuna miradi imechukua muda mrefu bila kukamilika, ikiwamo yenye zaidi ya miaka 10 tangu ilipoanza kujengwa.

Baadhi ya miradi ambayo inayotoa huduma, nayo inakabiliwa na tatizo la uchakavu, kutokana na kuwa muda mrefu baadhi iliwekwa tamgy zama za ukoloni na baadhi, inalaezwa ilijengwa kuzingatia idadi ya watu waliokuwapo kipindi hicho, lakini sasa miundombinu inashindwa kukidhi mahitaji kutokana na ongezeko kubwa la watu.

Prof. Mbarawa ziarani.

Kati ya Desemba 10 na 13 mwaka jana, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, alifanya ziara ya kufunga mwaka katika mikoa ya Mbeya na Songwe, alikokagua maendeleo ya utekelezaji miradi ya maji ya serikali.

Katika baadhi ya maeneo, alizindua miradi ya maji iliyokamilika na wananchi wakaanza kupata huduma hiyo muhimu, walikuwa walioikosa kwa muda mrefu.

Ziara hiyo iliwapa matumaini makubwa wananchi wa maeneo alikotembelea kupata huduma ya maji ya bomba, kutokana na maagizo na maoni aliyoyatoa wakati wa ukaguzi huo wa miradi.

MKOANI SONGWE

Prof. Mbarawa alianzia ziara katika Mkoa wa Songwe ambapo alianzia katika Wilaya ya Momba, alipokagua mradi mkubwa wa maji ya kisima katika Kata ya Ndalambo, unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya-WSSA).

Huo ni mradi unaokusudiwa kuwanufaisha wananchi 11,000 wa kata hiyo na unatarajiwa kuongeza kiwango cha upatikanaji maji katika Wilaya ya Momba kwa kufikisha asilimia 48.

Kwa mujibu wa Meneja wa Mbeya-WSSA, Mhandisi Ndele Mengo, hadi Desemba mradi ulishakamilika kwa asilimia 95 na maeneo yaliyobakia ni machache ambayo ndani ya muda mfupi ujao watakamilisha na wananchi kuanza kupata maji.

Mengo anasema, mtandao wa maji hayo wenye urefu wa kilomita 6.9 umeshakamilika, nyumba ya kuhifadhi mashine ya kusukuma maji inayotumia umeme imekamilika kwa asilimia 90 na tayari umeme tumeshaingiza.

“Mradi utakuwa na vituo nane na vyote vimeshaandaliwa kwa asilimia 100, urefu wa matangi mawili yenye urefu wa mita 50 m ambayo moja limekamilika kwa asilimia 98 na lingine asilimia 97, lakini tunaendelea kutekeleza kwa kasi ili tumalize mapema,” anasema Mhandisi Mengo.

Prof. Mbarawa anasema, awali mradi ulikuwa unatekelezwa na makandarasi ambao kwa kiwango kikubwa walichangia kuchelewa kwa mradi huo na kuongeza gharama ambazo zilikuwa sio za msingi.

Anasema wakati wanatumika makandarasi mradi ulikuwa unagharimu Sh. milioni 577, lakini baada ya kuachana na makandarasi hao unatarajiwa kugharimu Sh. milioni 345 kutokana na kujengwa kwa kutumia mfumo wa akaunti ya dharura (Force Account).

“Mpaka sasa tangu tumekabidhi mradi kwa Mbeya-WSSA, unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu tangu walipoanza kutekeleza. Hii ni hatua kubwa mno hata wataalamu wangu wa wizara ni mashahidi haijawahi kutokea mradi kutekelezwa kwa haraka hivyo,” anasema Prof. Mbarawa.

Waziri anadokeza, mbali na mradi kutekelezwa haraka, lakini ni wa uhakika kutokana na mabomba yanayotumika kuwa ya viwango vinavyotakiwa kutokana na kuchukuliwa moja kwa moja kiwandani.

Anasema makandarasi waliotekeleza mradi huo walimu walishafutiwa usajili na kwamba walikuwa wanatekeleza mradi mwingine katika makao makuu ya wilaya ya Momba, ambako serikali pia itatekeleza kwa utaratibu huo uliotumika huko Ndalambo.

Mjini Tunduma

Baada ya kutoka Momba, Prof. Mbarawa alielekea kutembelea miradi ya visima vitano virefu vya maji katika Mamlaka ya Mji wa Tunduma, ambavyo vimekamilika na tayari wananchi wanapata maji.

Visima alivyotembelea Prof. Mbarawa, vinazalisha maji yenye ujazo wa zaidi ya lita 30,000 kwa siku na kwa mujibu wa wataalamu, vimesaidia kupunguza tatizo la maji katika mji kwa kiwango kikubwa.

Meneja wa Mbeya – WSSA, Mhandisi Mengo anasema kutokana na idadi ya wakazi wa mji huo, bado wanahitaji kutafuta vyanzo vingine vitakavyowezesha kufikisha asilimia 85 ya kiwango cha upatikanaji huduma hiyo.

Meneja wa Mamlaka ya Maji Mijini na Vijijini (Ruwasa) Mkoa wa Songwe, Charles Pande, anasema tayari wameanza kufanya upembuzi wa chanzo kipya cha maji ya Mseleleko kutoka wilayani Ileje kwenda mji huo wa Tunduma.

Pande anasema, chanzo hicho kitasafirisha maji kwa zaidi ya kilomita 50 na endapo watafanikiwa kukikamilisha, kitamaliza kabisa tatizo la maji mjini Tunduma na vijiji vitakavyopitiwa na bomba, huku kukiwapo ziada.

“Kile chanzo ni cha uhakika na kina maji ya kutosha, ikitokea tukakikamilisha vizuri, basi tatizo la maji katika Mji wa Tunduma itakuwa ni historia,” anasema Meneja Pande.

Baada ya maelezo hayo, Waziri Mbarawa aliitaka mamlaka kuharakisha upembuzi huo, ili fedha za utekelezaji zitolewe mapema na wananchi waondolewe tatizo lililopo.

“Lengo la serikali ni ‘kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani’. Sasa naamini kabisa visima tulivyochimba kwenye mji huu havitoshelezi mahitaji, hivyo mnatakiwa mharakishe upembuzi ili tuanze utekelezaji,” anasema Prof. Mbarawa.

Maelekezo hayo ya waziri yalionyesha kuongezea nguvu Ruwasa kwenye utekelezaji wa mradi huo, kuwapa matumaini wananchi kupata huduma ya maji.

Wilaya Mbozi

Baada ya kutoka Mji wa Tunduma, safari ya Waziri Mbarawa ilielekea chanzo cha maji cha Vwawa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, ambacho kinatarajiwa kuwahudumia wananchi wa Mji wa Vwawa.

Ni mradi uliozinduliwa na Rais Dk. John Magufuli alipokuwa ziarani mkoani Songwe, uliokuwa bado haujaanza kupeleka maji kwa wananchi, lakini waziri akawapa wananchi matumaini ya kuanza kupata huduma kuanzia mwezi huu.

Aahidi maji hayo kuanza kusambazwa kwenye makazi ya wananchi mwezi Januari na alizitaka mamlaka zinazohusika kuanza kuweka baadhi ya miundombinu muhimu.

“Endeleeni kuwafungia wananchi dira za maji ili watakapokuwa wanalipia wawe wanaelewa vizuri matumizi ya maji, hii inasaidia kupunguza malalamiko yasiyokuwa na maana,” anasema Prof Mbarawa.

Matumaini ya wananchi kuwa kilio chao cha muda mrefu kutopata huduma ya maji kwa ufanisi, kikapata nuru ya kuanza kufurahia huduma hiyo. Aliwataka waendelee kuvuta subira.

Wilaya Kyela

Baada ya kumaliza ziara yake mkoani Songwe, Waziri Prof. Mbarawa, aliingia katika mkoa wa Mbeya, alianzia katika Wilaya ya Kyela, ambako alileta neema kwa wananchi kwa kuzindua mradi wa maji wa Kapapa Group ulioanza kutekelezwa muda mrefu.

Ni mradi unaoanzia katika chanzo kilichopo Busokelo wilayani Rungwe na unahudumia wananchi zaidi ya 13,000 wa vijiji nane kutoka katika kata nne za Ipinda, Mwaya, Talatala na Ikama, ambako kwa muda mrefu walikuwa hawapati huduma hiyo.

Kwa mujibu wa Prof. Mbarawa mradi huo umeigharimu serikali Sh. bilioni 3.55 na kutokana na mkandarasi wa awali kuchelewa kuukamilisha waliamua kusitisha mkataba na wakaikabidhi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya-WSSA) ambayo iliukamilisha ndani ya muda mfupi.

“Lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wa maeneo ya miji na wilaya wanapata maji kwa asilimia 90 na wa maeneo ya vijijini wawe wanapata maji kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2020,” alisema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa mbali na kuzindua neema hiyo kwa wakazi wa kata hizo nne, pia aliwashauri wananchi hao kuunda kamati za watumia maji kwa ajili ya kusimamia mradi huo ikiwa ni pamoja na kukusanya mapato na kufanyia marekebisho miundombinu.

Hata hivyo, aliwashauri kuendelea kutunza vyanzo vya maji ili kuhakikisha wanaendelea kupata maji katika kipindi chote cha mwaka na kuepuka kuyachafua maji hayo.

Halmashauri Busokelo

Akiwa katika Bonde la Mwakaleli, katika Halmashauri ya Busokelo wilayani Rungwe, Waziri Mbarawa alikerwa kutoka jijini Dar es Salaam kuchelewesha mradi wa maji wa bonde hilo kwa zaidi ya miaka 10.

Mradi huo unadaiwa kuwa ulianza kujengwa tangu mwaka 2008, lakini mpaka sasa wananchi bado hawajaanza kunufaika huku kukiwa na ubabaishaji wa mkandarasi katika kuutekeleza.

Mbali na kuchelewesha mradi huo, pia Waziri Prof. Mbarawa, alibaini ubadhirifu mkubwa wa fedha zilizotengwa kuujenga mradi huo, hivyo akaiagiza Polisi kuchukua hatua dhidi mhandisi huyo wa maji wa kampuni hiyo.

Pia, aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kuuchunguza mradi mzima, kwa maelezo baada ya kupitia mpango kazi mzima, alibaini dalili za ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma.

“Mradi mzima unagharimu Sh. bilioni sita na mpaka sasa wameshalipwa bilioni tatu, lakini hakuna kilichofanyika hapa. Nimepitia mpango kazi wao, unaonyesha hiki kibanda cha mabati wamekijenga kwa Sh. milioni 100,” analalamika Prof. Mbarawa.

Aidha, kutokana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mbeya (Mbeya-WSSA) kufanya vizuri kwenye miradi ambayo, ilipewa itekeleze, na Waziri Prof. Mbarawa, aliiagiza kuvunjwa mkataba wa mkandarasi huyo, ili itekeleze yenyewe.

Anasema, mradi utakapokamilika utawanufaisha wananchi wa vijiji 18 vya Halmashauri za Rungwe na Busokelo, ambao wameikosa huduma ya maji kwa muda mrefu.

Habari Kubwa