SIMANZI NAOMI

20Jul 2019
Beatrice Moses
Dar es Salaam
Nipashe
SIMANZI NAOMI
  • *Ndugu wasubiri kipimo DNA
  • *Ikithibitika kuzikwa kwa heshima

MAPENZI yanaua. Ni msemo ambao unaweza kuhusishwa na matukio kadhaa na visa vya mauaji vinavyotokana na migogoro ya uhusiano wa mapenzi wakiwamo walio kwenye ndoa.

Kisa cha mauaji kinachotajwa kumkuta mwanandoa Naomi Marijani, (36) ni cha kusikitisha ambapo kwa hakika kimeacha maswali kadhaa ambayo ni kitendawili kinachongoja mahakama kukitegua.

Ni wazi kwamba ndugu, jamaa na marafiki kama wanajamii wanalazimika kusubiri mahakama kutoa maelezo iwapo Naomi mama wa mtoto mmoja ameuawa na mumewe anayetajwa kwa jina la Khamis Luongo,(38).

Inasubiriwa korti iufahamishe umma, kwa nini aliamua kumteketeza kwa mkaa na kufanya majivu yake mbolea ya mgomba.

Ni kwa nini alimshitaki mkewe kuwa ametelekeza mtoto wao wakati akijua kuwa ameshamuua?

Hayo ni miongoni mwa maswali ambayo Luongo atakapandishwa kizimbani anatarajiwa kuyajibu baada ya mahakama kumsikiliza na kujuua ukweli.

Zaidi kufahamu ni kipi kilimchochea kufanya mauaji hayo yanayoshangaza na kufikirisha wengi.

MAELEZO YA POLISI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Amon Kakwale, anazungumzia  tukio hilo, akibainisha kuwa asubuhi ya Mei 15 mwaka huu, katika eneo la Gezaulole Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es salaam, Luongo, anashukiwa kumuua mkewe.

“Mara baada ya mauaji hayo Luongo anaeleza kwamba alichukua mwili wa mke wake na kuuweka kwenye  shimo alilolichimba kwenye banda la kufugia kuku kisha aliweka mkaa magunia mawili na mafuta ya taa akawasha moto,” anasema Kamanda.

Luongo anatajwa kuwa ni mfanyabiashara, inayeelezwa kuwa baada ya kuuteketeza mwili huo alichukua mabaki kwa gari lake lenye namba T 206 CEJ  aina ya Subaru Forester.

Aliyapeleka shambani kwake kijiji cha Mlogolo huko Vikindu Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani na kuyazika, kisha akapanda mgomba juu yake.

Kamanda anabainisha kuwa baada ya kufukia majivu na kupanda mgomba alirudi nyumbani kwake akitangaza kuwa mke wake ametoroka nyumbani.

KUBAINIKA

Kakwale anasema siku nne baadaye, ilipofika Mei 19, Luongo alifungua jalada polisi kuwa mke wake ametoroka nyumbani na kupewa RB yenye kumbukumbu MJ/RB/234/2019 kutoka kituo kidogo cha Polisi Mjimwema.

“Baada ya kufanya hayo inaelezwa kuwa Luongo aliwajulisha ndugu jamaa na marafiki zake kuwa mke wake ametoroka nyumbani. Juni 12, mwaka huu alifungua jalada jingine KGD/IR/3617/2019 linalomlalamikia mkewe kumtelekeza mtoto, aitwaye Gadious Khamis mwenye miaka sita,” anasema Kamanda Kakwale.

HOFU YA NDUGU

Kamanda Kakale, anaongeza kuwa ndugu wa Naomi nao walifungua jalada katika kituo cha Temeke Juni 13 mwaka huu, kutoa malalamiko ya kupotea kwa ndugu yao wakiomba kufanyike uchuguzi.

“Upelelezi uliendelea. Luongo akiwa anaenda kuripoti Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi (RCO) Temeke hadi tarehe 15 Julai mwaka huu alipozuiliwa kwa mahojiano ya kina ndipo akaamua kusema ukweli kuwa alimuua mkewe.”

Yanayodaiwa kuwa ni mabaki ya mwili wa Naomi yalipatikana Julai 16 mwaka huu, huko sambani kwao, baada ya polisi kuelezwa kuwa ndiko eneo yalipozikwa.

Taarifa kutoka kwa ndugu wa Naomi zinabainisha kuwa ununuzi wa gari la mtumba aina ya Vitz unaweza kuwa sababu ya mauaji ya ndugu yao huyo.

Akizungumza na Nipashe kaka wa marehemu Wiseman Marijani, anasema kuwa Luongo alikuwa na mgogoro na mkewe baada ya kuona amenunua gari hilo bila kumwomba fedha.

 

Anaeleza kuwa Naomi alinunua gari hiyo baada ya kuchukua mkopo kutoka kwenye fedha zinazotokana na kodi za wapangaji kwenye nyumba yao ya urithi walioachiwa na wazazi.

Familia hiyo imeanzisha utaratibu wa kukusanya fedha hizo na kukopeshana ili kuwa na miradi mbalimbali ya kujiendeleza.

“Naomi alinijulisha jinsi mumewe alivyotia shaka mahali alipopata fedha hizo za kununulia gari, alilalamika kuwa hakutaka kumwamini kuwa alikopa fedha za familia,” Marijani anaeleza.

Marijani anasema kwa nyakati tofauti amesuluhisha migogoro kadhaa ya dada yake na shemeji yake, lakini hakutarajia itafikia kugharimu uhai wa mdogo wake.

Anabainisha kuwa ingawa baadhi ya migogoro hiyo ilisababisha Naomi  aliyekuwa na shahada kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere cha Dar es Salaam kuacha kazi.

Wakati wa uhai wake Naomi alifanya kazi kwenye Shirika la Utafiti la Synovate na TNS Research international na Baraza la Mtihani la Taifa( NECTA).

NAOMI

“Nakumbuka mdogo wangu aliwahi kulalamika mambo mengi ikiwamo kuhusu wasichana kuondoka nyumbani ghafla na kumwachia mwanaye ndipo akaamua kujiajiri mwenyewe kwa kuanzisha duka la dawa ili pia kumhudumia mwanaye Gadiosa,”anasema.

Marijani anabainisha kuwa nduguye pia aliwahi kulalamika kuwa mumewe alikuwa anafanya mambo ya hatari kama kuwasha jiko la gesi na kuacha gesi kusambaa ndani kwa wingi. Naomi alipofika na kuwasha ili kupika moto ulilipuka lakini alisusurika.

“Nakumbuka ulikuwa mgogoro mkubwa kwa kuwa Naomi alikasirika na kulalamika sana kuhusu kitendo hicho,” Marijani anasema. 

Anasema baada ya kupata taarifa za kutoweka kwa ndugu yao walipata mashaka, baada shemeji yao kuwaambia kuwa alitoweka ghafla katika mazingira yasiyoeleweka.

“Kwanza tulimuomba Mungu sana,pia tutafanya juhudi mbalimbali za kumtafuta kama wanandugu, mazingira yaliyoonekana yalisababisha tuzidi kumhisi shemeji kuwa anajua ndugu yetu alipo,” alisema. 

JITIHADA

Juhudi zilizofanywa za kumtafuta Naomi ni pamoja na kutoa matangazo kwenye mitandao ya jamii, pamoja na kushirikisha mamlaka mbalimbali.

“Tunashukuru Mungu. Shemeji amekiri mwenyewe polisi kuwa amemuua na kueleza alichofanya na jinsi ambavyo tukio la mauaji limekuwa likimtesa likimjia kwa kurudia kichwani mwake hivyo kumkosesha amani,” Marijani anasema.

“Amewaeleza polisi kuwa alitumia siku tatu kuteketeza kwa moto mwili wa Naomi, ambapo alikuwa anaugeuza kama vile anachoma mishikaki, kisha kuchukua mabaki na kwenda kuyafukia kwenye shamba lao Mkuranga na kupanda mgomba,” Marijani anasema. 

KUANDAA MAZISHI

“Sasa tunasubiri uthibitisho wa vipimo vya DNA kutoka kwenye mabaki ya mwili wa ndugu yetu.Ikithibitika tutavikusanya na kuviweka kwenye jeneza jinsi vilivyo na tutamzika kwa heshima zinazostahili ili tuwe na alama ya kaburi lake,”anasema Marijani.

Mtaalam wa Saikolojia, John Ambrose maarufu kwenye mitandao ya jamii kama Johnsaikolojia anaelezea wivu wa mapenzi kwamba hujengeka kutokana na hofu na mazingira ya uhusiano ulivyoanza.

Anasema japo asingependa kuhusisha suala hilo tatizo la akili, lakini akaonya kuwa katika jamii kuna watu  wenye matatizo ya afya ya akili, wengine wakikabiliwa na msongo wa mawazo na hawajajishughulisha kupata tiba.

“Hii nayo imechangia matukio ya kikatili katika jamii. Utamaduni wa mtu kuwa na matatizo ya kisaikolojia na jamii au mhusika kuyapuuzia yamechochea mambo mabaya kutokea,’’anasema.