Simba bado wababe wa Yanga ardhi ya Zanzibar

16Jan 2017
Mahmoud Zubeiry
Dar es Salaam
Nipashe
Simba bado wababe wa Yanga ardhi ya Zanzibar

MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi 2017 ilifikia tamati Ijumaa kwa Azam kufanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuwachapa Simba bao 1-0 katika mechi ya fainali kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Pongezi kwa kiungo Himid Mao aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 12 kwa shuti kali la umbali wa mita 25 baada ya kupokea pasi ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Baada ya pasi ya Sure Boy, Himid alisogea hatua mbili mbele akatisha kama anapiga, akasogea tena hatua moja na kupiga shuti kali lililompita kipa wa Simba, Mghana Daniel Agyei.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mafume Ali Nassor, nafasi nzuri zaidi ambayo Simba waliipata ni dakika ya 27 baada ya beki Abdi Banda kupiga shuti la mpira wa adhabu umbali wa mita 22, lakini kipa Aishi Manula akajituma kulifuata pembezoni mwa lango kushoto na kutoa nje.

Kipindi cha kwanza mabeki wa Azam walikuwa wana kazi rahisi ya kumdhibiti mshambuliaji pekee wa Simba, Juma Luizo, lakini kipindi cha pili walifanya kazi ya ziada baada ya kuongezeka Mrundi Laudit Mavugo.

Hilo linakuwa taji la tatu la Kombe la Mapinduzi kwa Azam FC baada ya awali kutwaa katika miaka ya 2012 na 2013, hivyo kufikia rekodi ya Simba waliokuwa wanaongoza kwa kutwaa mara nyingi katika miaka ya 2008, 2011 na 2015.

Sifa zaidi kwa kocha aliyeiongoza Azam katika mashindano haya, Iddi Nassor ‘Cheche’ ambaye ameweka rekodi ya kutofungwa hata bao moja baada ya kufukuzwa kwa Wahispania chini ya Zeben Hernandez.

Azam pia imeendeleza rekodi yake ya kuchukua Kombe hilo mara zote ilizoingia fainali, wakati kwa Simba hii ni mara ya tatu wanaingia fainali bila kuchukua Kombe kama mwaka 2012 na 2014.

Gumzo zaidi katika michuano hiyo ilikuwa mpambano wa mahasimu wa jadi, Simba na Yanga waliokutana katika hatua ya nusu fainali.

Simba ilifanikiwa kuendeleza ubabe wake mbele ya Yanga kwenye ardhi ya Zanzibar kwa kuwatoa kwa penalti 4-2 kufuatia sare ndani ya dakika 90.

Penalti za Simba zilifungwa na nahodha Jonas Mkude, kipa Daniel Agyei, Muzamil Yassin na beki Mkongo Janvier Besala Bokungu, wakati kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ aliokoa mkwaju wa beki Mzimbabwe Method Mwanjali.

Waliofunga penalti za Yanga ni Simon Msuva na kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko wakati kipa Mghana wa Simba, Daniel Agyei aliokoa penalti za Dida na Mwinyi Hajji Mngwali.

Katika mchezo huo ambao Nassor alikuwa mwamuzi wa kati akisaidiwa na washika vibendera Mgaza Ally na Mbaraka Haule, Waziri Sheha mezani chini ya usimamizi wa Ramadhan Nassor, timu zote zilishambuliana kwa zamu.

Yanga ndiyo waliokuwa wa kwanza kulitia majaribu lango la Simba dakika ya nane, baada ya nahodha Haruna Niyonzima, raia wa Rwanda kupiga shuti kali akiwa nje kidogo ya 18 lililodakwa na kipa Agyei.

Yanga tena wakalijaribu lango la Simba dakika ya 15, baada ya winga Simon Msuva kupiga mpira uliorudi kufuatia pigo la mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe kuokolewa, lakini kipa Agyei akaokoa tena akishirikiana na beki Method Mwanjali.

Simba wakajibu dakika ya 16 baada ya kiungo Mohammed Ibrahim kupiga shuti kali lililodakwa na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’.

Msuva tena akakaribia kufunga dakika ya 36 baada ya kumtoka kwa chenga nzuri beki wa kulia wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na kumlamba chenga ya mpira wa kichwa kipa Agyei, lakini alipobinuka ‘kibaiskeli’ kwa pigo dhaifu lililokuwa linaelekea nyavuni, beki Janvier Besala Bokungu akatokea na kuokoa.

Zikiwa zimesalia dakika mbili mpira kuwa mapumziko, Luizio aliyesajiliwa kwa mkopo Desemba mwaka jana kutoka Zesco United ya Zambia akaikosesha Simba bao la wazi zaidi dakika ya 43 baada ya kupiga nje mpira uliorudi kufuatia shuti la Mo Ibrahim kugonga mwamba.

Kwa ujumla Yanga ilimiliki mpira kipindi cha kwanza , huku Simba ikimiliki zaidi kipindi cha pili.

Huo ulikuwa mchezo wa tano kuzikutanisha timu hizo visiwani humo, baada ya mara ya mwisho Simba kuifunga 2-0 Yanga Januari 12, mwaka 2011 kwenye fainali ya michuano hiyo, mabao ya Mussa Hassan Mgosi dakika ya 33 na Shijja Hassan Mkinna dakika ya 71.

Kwenye ardhi ya Zanzibar Yanga imeshinda mara moja tu dhidi ya Simba mwaka 1975 kwenye fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati 2-0, mabao ya Sunday Manara na Gibson Sembuli (marehemu).

Mechi nyingine zote Yanga walifungwa na mbali na hiyo ya 2011 ya Mapinduzi, walifungwa kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 1-1, Simba wakitangulia kwa bao la Hussein Marsha na wao kusawazisha kwa bao la Said Mwamba ‘Kizota’ (marehemu) na nusu fainali ya Ligi ya Muungano 1-0, bao pekee la Damian Kimti zote mwaka 1992.

Mapinduzi 2017 imepita, Azam bingwa, Yanga bado wanyonge wa Simba ardhi ya Zanzibar.

Habari Kubwa