Simba ikifanya hivi, Al Ahly itafia Taifa

11Feb 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba ikifanya hivi, Al Ahly itafia Taifa

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba kesho inatupa karata nyingine tena  dhidi ya Al Ahly kutoka nchini Misri.

Simba inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao  5-0 dhidi ya timu hiyo ya Al Ahly, Februari 2 nchini Misri. Kwa ilivyoonekana ni kwamba Wamisri hao si watu wa mchezo-mchezo, wanaoweza kushinda hata ugenini kama Simba  haikujipanga vizuri.

Katika mechi ya kwanza, kikosi cha Simba kilionekana kuwa na  matatizo au mapungufu mbalimbali kiuchezaji.

Hata hivyo, kinachowapa matumaini wanachama na mashabiki wa Simba ni kwamba wapo kwenye ardhi ya nyumbani, hivyo wana uwezo mkubwa wa kupata ushindi.

Yafuatayo ni mambo ambayo wachezaji wa Simba wanapaswa kuyazingatia  wawapo uwanjani mbele ya maelfu ya watazamaji wao ili kushinda...

 

1. Kusoma mchezaji wa wapinzani wao

Kwanza kabisa wachezaji wa Simba watatakiwa kuwasoma wapinzani wao wamekuja na mfumo gani. Mara nyingi timu za Kiarabu zinapocheza kwenye viwanja vya ugenini huwa na mfumo wa kuzuia  zaidi na kushambulia kwa kushtukiza wakiwa na kasi ya ajabu.

Kinachotakiwa ni wachezaji wa Simba washambulie kwa pamoja na kurejea nyuma kwa pamoja kusaidia bila kutegeana kwani mabeki  wa Simba peke yao wanaonekana hawawezi kumudu kasi ya mawinga wa Al Ahly.

 

2. Kutumia nafasi zitakazopatikana

Kwa siku za karibuni Simba imekuwa ikikosa sana nafasi inazozipata  za kufunga mabao. Hili linasababisha baadaye kuja kuadhibiwa na wapinzani wao ambao  wanaonekana wanajua sana kutumia nafasi na madhaifu yao.

Mastraika wa Simba wanapaswa kuwa makini na kutumia nafasi za kufunga mabao, hasa dakika za mapema ili 'kuua' mchezo mapema. Mfano Simba ikiweza kutumia nafasi mbili tu kupachika mabao,  inaweza kabisa kuwafanya Al Ahly kutokuwa kwenye kasi yao ya  kawaida na pia kuamua kuondoka nyuma kusaka mabao na hii inaweza tena ikawa nafasi zaidi kwa Simba kupachika mabao mengine  kama ilivyokuwa dhidi ya JS Saoura ya Algeria.

 

3. Mabeki kutokaba kwa macho

Hii imekuwa kama ni tabia sasa kwa mabeki wa Simba. Wanaonekana kama ni watu ambao wanaogopa kupigwa chenga,  hivyo kuwaacha washambuliaji wa timu pinzani kwanza wamiliki mpira na kuanza kuwafuata tena kwa woga, hivyo kupigwa chenga  kirahisi.

Kama mabeki wa Simba wanahitaji Al Ahly isipate bao kwenye mechi hiyo, wanapaswa kuwasumbua pale tu wanapoletewa mipira. Starika au winga anayepata usumbufu pale anapopasiwa mpira anakuwa hana akili ya kufanya maamuzi ya haraka kwanza mpaka amalizane na beki.

Lakini kama wanakuwa wako huru na kuruhusiwa kufanya  wanavyotaka, basi watakuwa kwenye wakati mgumu mno.

 

4. Wawe makini kwenye krosi, faulo

Mabeki wa Simba pia wanatakiwa wawe makini mno kwenye mipira ya juu, hasa kwenye krosi zinazopigwa.

Waarabu mara nyingi ni wazuri sana kwenye mipira ya vichwa, hasa mabeki wanapokuwa wazembe kuokoa mipira ya krosi kama wa Simba. Ukiangalia sana, Juuko Murshid na Pachal Wawa huwa si  wazuri sana kwenye mipira ya vichwa, hivyo kama wanataka ushindi ni lazima wajirekebishe.

Lakini pia Simba wanatakiwa kuwa makini na mipira ya faulo. Waarabu pia ni wazuri mno kupiga na kufunga kupitia aina hiyo ya mipira.

Faulo kwa Waarabu kwao ni kama 'nusu penalti', hivyo mabeki wawe makini na rafu zisizo na msingi karibu na eneo la hatari.

 

5. Wachezaji kutokaa sana na mipira

Moja ya tatizo kubwa kwa wachezaji wa Simba ni kukaa na mpira kwa muda mrefu bila sababu yoyote.

Kuna baadhi ya wachezaji wa Simba wakipata mpira ndiyo wanaanza kufikiria wafanye nini, kitu ambacho ukikutana na wachezaji kama wa Al Ahly wenye uzoefu mkubwa hawakupi muda huo kabla ya  kukunyang'anya.

Wachezaji wa Simba hawana stamina kama wa Al Ahly, hivyo kukaa na mpira muda mrefu wanajikuta wakinyang'anywa kirahisi sana.

Kinachotakiwa kwa wachezaji hao ni kucheza kwa kasi, huku kila mchezaji akitumia muda mfupi tu kukaa na mpira kabla ya kumpasia  mwenzake.

Kabla mabeki wa Al Ahly hawajajua nini kitakachofanyika, basi  mpira uko kwa mwingine. Hii itasababisha wapinzani wasiweze kupata muda wa kujipanga ili kuokoa hatari.

Wakati mwingine kinachowaangusha Simba ni mtu mmoja kukokota mpira kwa muda mrefu, na pasi fupi fupi zisizo na malengo, huku  wakicheza kwa kasi ndogo, jambo linalosababisha wapinzani kupata muda wa  kujipanga, hivyo hata shambulio wanalofanya linakuwa halina  madhara kwa sababu tayari mabeki na viungo wa timu pinzani wanakuwa wameshajaa nyuma.

Habari Kubwa