Simba ilivyoanza kusaka pointi tisa CAF

14Jan 2019
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba ilivyoanza kusaka pointi tisa CAF

MABAO matatu, mawili yakifungwa na Mnyarwanda, Meddie Kagere na Mganda, Emmanuel Okwi yameifanya Simba kuanza vyema safari yao ya kusaka pointi tisa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Iliichapa JS Saoura ya Algeria mabao 3-0 juzi Jumamosi na kujiweka kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Mabingwa kwenye Kundi D, huku Al Ahly ya Misri ikishika nafasi ya pili baada ya kuichapa AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mabao 2-0.

Lengo namba moja la Simba kuzipata pointi tisa za, yaani kushinda mechi zote tatu itakazocheza nyumbani. Kwa maana hiyo zimebaki pointi sita, kwa sababu tatu tayari wanazo kibindoni.

Lengo la pili ni kupata angalau sare moja ama mbili kwenye mechi za ugenini ambazo zitaifanya kutinga hatua ya robo fainali.
Mahesabu hayo ya Simba yanatokana na funzo la mwaka 2003 ilipotinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, lakini ikishindwa kusonga mbele kwa kushika nafasi ya tatu ikimaliza na pointi saba.

Mechi za nyumbani iliichapa Enyimba mabao 2-1, pia ASEC Mimosas bao 1-0, lakini sare ya bila kufungana dhidi ya Ismailia ndiyo iliyowaangusha Wekundu hao wa Msimbazi.

Simba VS JS Saoura
Ilikuwa ni mechi nzuri kwa Simba, kwani ilitawala mechi yote, na karibuni muda mwingi ilikuwa ikifanya mashambulizi makali kwenye lango la wapinzani wao.

Ingeweza kupata ushindi mnono zaidi ya huo kama baadhi ya wachezaji wake wangekuwa kwenye kiwango chao kilichozoeleka.
Nahodha, John Bocco hakuwa kwenye kiwango cha kawaida na aliikosesha Simba nafasi mbili ambazo zingeweza kuwa magoli.

Straika huyo ambaye kwa siku za karibuni amekuwa akilaumiwa na wanachama na mashabiki wa timu yake kuwa amekuwa akikosa sana magoli, alionekana kutosimama kwenye eneo lake la namba tisa, kiasi wakati mwingine krosi zilizokuwa zikipigwa kupita bila kuunganishwa.

Mabeki wa kati wa timu hiyo nao walikuwa hawana presha wakati Bocco alipokuwa ndani kwani waliweza kumdhibiti kirahisi.
Mchezaji mwingine ambaye hakuwa kwenye kiwango chake kilichozoeleka ni kiungo, Hassan Dilunga "HD".

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems kwenye mechi hiyo aliamua kupunguza straika mmoja, kutoka watatu ambao huwa anawapanga, hadi wawili Bocco na Okwi, akamuweka Kagere nje, huku Dilunga akiwa ndani kwa sababu moja tu ya kujaza viungo wengi kati.

Alijua kuwa timu za Kiarabu zina tabia ya kuwa na viungo wengi kati, hivyo naye alimuongea Dilunga ambaye huwa anaingia kipindi cha pili, aanze.

Hata hivyo, hakufanya kama ambavyo wengi walitarajia kwa sababu alipoteza mipira mingi na alicheza kwa taratibu sana tofauti na alivyozoeleka.

Waarabu walikula sahani moja na Chama
Mchezaji ambaye alipata shida kwenye mechi hiyo ni kiungo Mzambia, Clatous Chama.

"Intelejensia" ya JS Saoura iliwaambia kuwa Chama ndiye mchezaji hatari zaidi kwenye kikosi cha Simba, anayeamua timu ifanye nini kwa muda gani na icheze vipi wakati gani, hivyo walimuwekea watu wawili ambao kila anapochukua mpira wanamfuata. Wakati huo huo, mchezaji mmoja naye anakuwa tayari kutoa msaada kwa wenzake.

Hii ilimfanya kushindwa kufanya vitu vyake, hata ile staili kutoa pasi na kuisubiri upande wa pili waliidhibiti vilivyo.
Kwa kiasi kikubwa Waarabu walifanikiwa kwa hilo, ikafikia wakati Chama akawa anarudi nyuma kupokea mipira ili kuwakimbia wachezaji wale na ili apate nafasi ya kuukokota mpira na kufanya vitu vyake kama kawaida.

Wachezaji waliokuwa kwenye ubora wao
Wachezaji waliocheza kwa kiwango cha hali ya juu kwenye mechi ya juzi Jumamosi tunaanza na Okwi.
Huyu alikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu zaidi toka michuano hii ianze Simba ilipocheza dhidi ya Mbabane Swallows jijini Dar es Salaam.

Mechi zote hizo hadi na Nkana FC, Okwi hakuwa kwenye kiwango cha juu kama alichokuwa nacho Jumamosi.
Aliwatesa na kuwapinduapindua Waarabu anavyotaka. Rejea bao la kwanza alivyowatesa wageni hao.

Lakini pia ndiye aliyetoa pasi za mwisho za magoli yote mawili kwenye mechi hiyo.

Paschal Wawa alikuwa kwenye kiwango cha juu na ilifikia wakati alikuwa akicheza kwa mbwembwe na madoido.
Inawezekana ni kutokana na kazi kubwa aliyokuwa akiifanya, Juuko Murshid ya kupambana na mastraika wasumbufu kina, Thomas Ulimwengu, kiasi kwamba yeye alikuwa na kazi ndogo tu.

Juuko na Meddie Kagere kama kawaida nao walikuwa moto, lakini pia kipa Aishi Manula naye alikuwa kwenye ubora wake kwani aliweza kuokoa mipira ya faulo za Waarabu, mipira ambayo mara nyingi Manula huwa inampa tabu kwenye mechi zingine.

Mohamed Hussein "Tshabalala" naye alionekana kufanyia kazi mapungufu yake yaliyoonekana kwenye mechi dhidi ya Nkana FC, ya kushindwa kukaba na kuruhusu mawinga kupita kama vile wanakwenda sokoni. Kwenye mechi ya Jumamosi alijitahidi kuhakikisha mawinga hawakatizi.

Pengo la Nyoni halikuonekana
Tayari kumekuwa na mitazamo tofauti kwa wanachama na mashabiki wa Simba juu ya Juuko na Nyoni nani aanze.

Alipoumia Erasto Nyoni wengi walikuwa na wasiwasi kiasi cha kumlaumu kocha kwa kumchezesha mechi ya Kombe la Mapinduzi wakati timu ina mechi ngumu mbele.

Hata hivyo kazi iliyofanywa na Juuko, iliwafurahisha Wanasimba na hakukuonekana pengo lolote la Nyoni, kiasi na wengine kusema kuwa Juuko ndiyo awe anasimama na Wawa kwani inaonekana kama wanaelewana zaidi kuliko Wawa na Nyoni.

UWANJA WATAPIKA

Kwa mara nyingine, mashabiki wa Simba walihudhuria kwa wingi uwanjani ili kuishangilia timu yao ambayo ndio inapeperusha pekee bendera ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa.

Idadi kubwa ya mashabiki hao wa Simba katika mechi za kimataifa, imeanza kuwa gumzo kwa wapinzani wao ambao hawaamini, klabu inaweza kuujaza uwanja huo wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 60,000.

Mbali na mechi za kimataifa, klabu hiyo imekuwa ikiujaza uwanja huo katika Tamasha la Simba Day ambalo linafanyika Agosti 8 ya kila mwaka kwa kuwatambulisha wachezaji pamoja na jezi mpya watakazozitumia katika msimu husika.

Kila la kheri Simba katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Habari Kubwa