Simba kileleni kila kona, saba waunda Taifa Stars

07Nov 2016
Mahmoud Zubeiry
Dar es Salaam
Nipashe
Simba kileleni kila kona, saba waunda Taifa Stars

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Boniface Mkwasa ‘Master’ mwishoni mwa wiki ametaja kikosi kitakachomenyana na Zimbabwe katikati ya mwezi huu.

mkude.

Taifa Stars itasafiri hadi Harare, Zimbabwe kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa na wenyeji hao maarufu kama The Warriors, utakaopigwa Novemba 13, mwaka huu.

Katika kikosi cha wachezaji 24, alichokitaja Mkwasa, amechukua nyota saba kutoka klabu ya Simba.

Hao ni beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, viungo Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, Jonas Mkude, Muzamil Yassin, Shizza Kichuya, Jamal Mnyate na mshambuliaji Ibrahim Ajibu.

Ikiwa inaongoza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa pointi 35 za mechi 13, ikifuatiwa kwa mbali na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 27 za mechi 13 – si ajabu kuona Simba ikitoa wachezaji wengi Taifa Stars.

Kuwa na timu bora ni matunda ya kuwa na kocha bora na Simba wanatudhihirishia hilo baada ya uteuzi wa Mkwasa wa kikosi cha mchezo wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe.

Na hapo hapo, tunapata majibu kwa nini Yanga imeporomoka – kwani idadi ya wachezaji wake Taifa Stars imepungua na safari hii wameitwa wanne tu, ambao ni kipa Deogratius Munishi ‘Dida’, mabeki Mwinyi Hajji, Vincent Andrew wa Yanga na winga Simon Msuva.

Wachezaji wengine walioitwa Stars kwa ajili ya mchezo huo utakaofanyika Novemba 13 ni makipa: Said Kipao wa JKT Ruvu na Aishi Manula wa Azam FC.

Mabeki: Erasto Nyoni, David Mwantika wa Azam FC, Michael Aidan wa JKT Ruvu na James Josephat wa Prisons.

Viungo ni Himid Mao wa Azam FC na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting, huku washambuliaji John Bocco wa Azam FC, Elius Maguli wa Oman Club, Thomas Ulimwengu ambaye hajapata timu baada ya kumaliza mkataba wake TP Mazembe ya DRC na kundoka mwezi uliopita, Omar Mponda wa Ndanda FC na Nahodha Mbwana Samatta wa K.R.C Genk ya Ubelgiji.

Wakati akitaja kikosi hicho, Mkwasa alisema kwa sababu mbalimbali hususan majeruhi, amewaacha wachezaji Shomary Kapombe wa Azam FC, Hassan Kabunda wa Mwadui FC, Juma Abdul na Juma Mahadhi wa Yanga.

Kama wachezaji saba wa Simba wanachukuliwa Taifa Stars, maana yake wanabaki wanne ili kukamilisha kikosi cha kwanza. Na hao wanne katika kikosi cha Simba ambao hawajaitwa Taifa Stars ni akina nani?

Kipa raia wa Ivory Coast, Vincent Angban, beki wa kulia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Janvier Besala Bokungu, beki wa kati Method Mwanjali kutoka Zimbabwe na Juuko Murshid wa Uganda na washambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo na Muivory Coast, Frederick Blagnon.

Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog amekuwa akipata wachezaji 11 wa kuanzisha katika kikosi chake cha kwanza kutokana na Angban, Bokungu, Mwanjali, Juuko, Mavugo, Blagnon, Tshabalala, Mo Ibrahim, Mkude, Muzamil, Kichuya, Mnyate na Hajib na wanaobaki mara nyingi hutokea benchi miongoni mwao ni pamoja na Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto, Ame Ally ‘Zungu’ mara chache.

Na katika wachezaji wa kigeni wa Simba, Juuko na Mavugo wote huitwa katika timu zao za taifa na hata ambao hawaitwi kama Mwanjali, Bokungu na Blagnon ni wachezaji ambao ukiwatazama tu huna shaka na juhudi zao uwanjani na msaada wao unaonekana.

Mussa Chichi Ndusha, kiungo kutoka DRC ni mchezaji pekee wa kigeni ambaye hajatumika ipasavyo kwa sababu Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ilichelewa kutoka – lakini naye katika mechi chache alizocheza ameonyesha dalili za uchezaji mzuri. Tusubiri kumuona zaidi.

Hayo ndiyo majibu ya ubora wa Simba kwa sasa – kwamba ina wachezaji wazuri, wanaojituma uwanjani na wenye kiu. Haitoshi kuwa mchezaji mzuri na kusifiwa wewe fundi wakati huna jitihada za kuisaidia timu uwanjani, ndiyo maana Mkwasa amewaita Taifa Stars wachezaji walioonyesha juhudi.

Habari Kubwa