Simba, Yanga, Azam kutangazwa Afcon

09Jan 2017
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Yanga, Azam kutangazwa Afcon

MACHO na masikio ya mashabiki wa soka Afrika, yataelekezwa nchini Gabon kuanzia Januari 14 kwenye fainali za Mataifa ya Afrika.

Jumla ya timu za mataifa 16 zitapambana kutafuta bingwa wa Afrika mwaka huu.

Wachezaji mbalimbali wa Kiafrika, wamemiminika nchini humo kutoka kona zote za dunia kwa ajili ya michuano hiyo.

Wapo wanaocheza Ligi Kuu ya England, Hispania, Italia, Ufaransa, Uturuki, Ubelgiji, Uswisi, Marekani, Uholanzi, Urusi, Ujerumani na kwingineko.

Pia kuna wachezaji waliotoka Bara la Asia wakicheza soka la kulipwa huko, lakini wengine hapa hapa Afrika.

Ingawa Tanzania haishiriki michuano hiyo, lakini Ligi Kuu Tanzania Bara haipo nyuma katika kutoa wachezaji wanaoshiriki michuano hiyo ya Afcon 2017, na watazitangaza klabu zao za ligi kwa ujumla.

Wachezaji hao ni wale waliochaguliwa na mataifa yao yaliyofuzu kwenda kuzitumikia nchini zao, hawa hapa...

1. Juuko Murshid-Uganda (Simba)
Beki huyu wa kati wa klabu ya Simba atakuwa ni mmoja wa wachezaji watakaoshiriki michuano hiyo, kutoka kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Ni mchezaji aliyepenya kwenye mchujo wa kocha wa timu hiyo, Mserbia Milutin Sredojevic 'Micho'.

Ni mmoja wa mabeki ambao wameisaidia sana Uganda 'The Cranes' kutinga hatua hiyo, kwani alikuwa akiitwa mara zote kwenye hatua ya makundi.

Ni mchezaji mwenye sura mbili. Akiwa kwenye Ligi Kuu Bara, anatajwa kuwa ni beki anayecheza kibabe zaidi na kuogopewa na mastraika wengi.

Hata hivyo, huwezi kudhani kama ni yeye, akiwa kwenye timu yake ya taifa kwa jinsi anavyocheza kistaarabu zaidi.

Staili zote mbili, hazimfanyi kuwa beki mwenye uwezo mkubwa na mwiba kwa mastraika.

Beki huyo mwenye miaka 26, alisajiliwa na Simba miaka mitatu iliyopita.

2. Vicent Bossou-Togo (Yanga)
Mwingine anayecheza soka nchini Tanzania na amekwenda Afcon 2017 ni Vocent Bossou.

Huyu pia ni beki wa kati kama ilivyo kwa Juuko Murshid. Lakini anaichezea Yanga ambayo ni mahasimu wakubwa wa Simba. Amechaguliwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Togo.

Bossou, ni beki anayemaliza msimu wa pili sasa kwenye klabu ya Yanga, lakini awali alikuwa hakubaliki.
Mechi za mwanzo alionekana mzito na mashabiki hawakusita kumwita garasa.

Hata hivyo, alianza kubadilika pole pole na kuondokea kuwa beki mhimili mkubwa wa Yanga, hasa baada ya beki aliyekuwa tegemeo kwa wakati huo, Nadir Haroub 'Cannavaro' kuwa majeruhi.

Hadi leo ndiye beki wa kati tegemeo kwa Yanga. Hata hivyo kuna wasiwasi kama anaweza kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza kama ambavyo mwenzake Juuko kwenye kikosi cha Uganda.

Hii ni kutokana na timu hiyo kuwa na mabeki wengi kutoka nje ya Bara la Afrika, wanaochezea klabu kubwa Ulaya.

3. Bruce Kangwa-Zimbabwe (Azam)

Ni winga wa kushoto wa klabu ya Azam FC. Huyu naye atakuwapo nchini Gabon akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Zimbabwe.
Ni mmoja wa wachezaji walioitoa kimasomaso Ligi ya Tanzania nayo kutoa wachezaji ambao wameitwa na timu zao za taifa na kwenda Afcon.

Hata hivyo, wenyewe Wazimbabwe wamemwita kama beki wa kushoto na si winga, ingawa wanaweza kumtumia vyovyote vile watakavyoona inafaa.

Kangwa ni mchezaji ambaye alisajiliwa msimu huu na Azam FC, na ni mmoja wa wachezaji wa kigeni ambao angalau wanaonekana kuisaidia timu hiyo kwa sasa.

Habari Kubwa