Simiyu ‘wakenua meno’ neema ya watoto kusajiliwa kwa simu

04May 2017
Mary Geofrey
Dar es salaam
Nipashe
Simiyu ‘wakenua meno’ neema ya watoto kusajiliwa kwa simu

UTAFITI wa Idadi ya Watu Tanzania (DHS) wa mwaka 2010, unataja kuwa ni asilimia 16 tu ya watoto walio na umri chini ya miaka mitano ambao wamesajiliwa, huku asilimia nane pekee, ndio wameshapatiwa vyeti vya kuzaliwa na mamlaka husika.

Idadi hiyo inatajwa kuwa ndogo sana, ikilinganishwa na hatua iliyofikiwa katika nchi nyinginezo za Afrika ya Mashariki.

Takwimu zinaonyesha kuwa Uganda imefanikiwa kwa asilimia 30; Kenya asilimia 60; na Rwanda asilimia 63. 

Ili kuongeza takwimu za watu wanaosajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa, serikali kupitia Mamlaka ya Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) wameandaa mpango maalum wa kusajili watoto chini ya miaka mitano kupitia simu za mkononi.

Matumizi ya teknolojia ya simu za mkononi katika kuchukua na kutuma taarifa za usajili katika kazidata (database) na Rita inafanikisha kurahisisha utunzaji na upatikanaji wa kumbukumbu. 

Ni dhahiri kuwa, kwa mikoa ambayo mpango huu ulianza kutekelezwa tangu mwaka 2013, takwimu zimebadilika sana
Hadi sasa, watu waliosajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa jumla yao ni watoto 830,000 wenye umri chini ya miaka mitano katika mikoa ya Mbeya, Simiyu, Mwanza, Iringa na Geita. 

Cheti cha kuzaliwa kimsingi ni haki ya mtoto ya kuzaliwa na utambulisho wa kwanza wa kisheria unaomsaidia mtoto kupata huduma nyingine za kijamii, kama vile afya na kujiunga shule.

Ni jambo linalozuia watoto hao kuingia katika ajira za utotoni, pia hutumika kupata hati kama za kusafiria na Kitambulisho cha Taifa. 

Kwa hali ilivyo na kutokana na takwimu, bila shaka wapo Watanzania wengi ambao watoto wao hawajasajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.

Huenda zinaweza kutajwa sababu nyingi, kuhusu tatizo hilo, lakini mfumo wa awali nao haukuwa rafiki na hasa kwa watu wanaoishi vijijini, ikilinganishwa na ilivyo sasa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa watoto milioni 230 wanazaliwa katika mazingira ambayo hayaonekani, ikimaanisha kwamba uzazi wao hausajiliwi. Kila mwaka kuna nyongeza nyingine ya watoto wasiosajiliwa duniani.

Kwa mujibu wa takwimu  zilizopo, asilimia 80  ya uzazi wa watoto wasiosajiliwa  hutokea  Afrika na hasa Tanzania, ikiwa ni sehemu mojawapo.

Katika nchi nyingi, watoto ambao familia zao ni maskini au wanaoishi katika maeneo ya vijijini, kwa kawaida imekuwa ni vigumu kwao kupata  usajili wa uzazi na kuwa na vyeti vya kuzaliwa.

Nchini Tanzania mchakato wa usajili wa uzazi ulioanzishwa kupitia Sheria ya Usajili na Vifo vya Mwaka 2002, inawataka wazazi kusajili watoto wao ndani ya siku 90 baada ya kuzaliwa.

Katika hatua ya kwanza, ni lazima wapate Tangazo la Uzazi kutoka hospitali au kituo cha afya mtoto alipozaliwa na kama ikitokea alizaliwa akiwa nyumbani, kuwepo taarifa kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji.

UNICEF inatambua  usajili wa uzazi, kama haki ya msingi ya kila mtoto kwa madai kuwa, usajili wa uzazi  unamaanisha  kwamba kunahitajiwa mpangilio mzuri wa huduma  kama vile elimu ya watoto na nyingine za kijamii.

MPANGO ULIVYOPOKEWA
Wakazi wa mikoa ya Geita na Shinyanga, walionufaika na mpango huo wa kupatiwa vyeti vya kuzaliwa watoto chini ya miaka mitano, wanaelezea jinsi walivyoupokea.
Wanaitafrisi kwamba ni huduma ya kipekee katika historia ya maisha yao ya kila siku.

Baadhi ya wananchi kutoka mikoa hiyo, kwa nyakati tofauti walisema kwamba wamekuwa wakisubiri huduma muhimu za kijamii kama hizo, lakini walikuwa wakikosa.

Wataalamu wa masuala ya maendeleo ya jamii wanasema kuwa, kutokuwa na cheti cha kuzaliwa kunaweza kukwamisha upatikanaji wa huduma bora za kijamii.

“Kwanza niseme kwamba huduma hii kwetu ni muhimu sana. Mara kwa mara tunasikia serikali ikituhimiza kuhakikisha kuwa watoto wana vyeti vya kuzaliwa, siamini kwamba kama kuna aliyechukia uwapo wa Rita na wadau wengine kama Tigo kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa hapa kwetu,” anasema Mama Kayenza mkazi wa Geita.

Burhan Hassan, ni mkazi wa Shinyanga anayesema, haimaanishi kwamba hapakuwepo mpango wa kumtafutia cheti cha kuzaliwa mtoto wake ambaye sasa ana miaka mitatu, bali anawashukuru wadhamini kurahisisha huduma hiyo, kupitia simu ya mkononi.

“Kama kila kampuni itakuwa na ubunifu wa namna hii, basi maendeleo yatafika sana huku vijijini kwetu. Haya tumezoea kuyasikia mjini, lakini kwa hili la kusajili na kupata vyeti vya watoto wetu vya kuzaliwa limenikuna sana,” anasena Hassan, huku akiwataka wananchi wengine wa Shinyanga kutumia fursa hiyo.

“Mara nyingi tumekuwa wepesi wa kukumbuka shuka kumekucha. Ningependa kuwashauri Wana- Shinyanga wenzangu kutumia fursa kama hizi zinapojitokeza na kuachana na imani za ajabu ajabu,” anaelezea.

Utafiti wa idadi ya watu Tanzania uliofanyika mwaka 2010, unaonyesha kuwa asilimia 16 pekee ya watoto walio na umri chini ya miaka mitano, ndio walikuwa wamesajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa na mamlaka husika.

Takwimu za Sensa ya mwaka 2012 nazo zinaainisha kuwa, asilimia 13.4 ya wananchi ndiyo waliyosajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.

Kutokana na takwimu hizo, kampuni ya simu za mkononi ni miongoni mwa wadau walioshirikiana na Rita na Unicef tangu 2012 kufanikisha utengenezaji wa mfumo maalumu, kupitia simu ya mkononi unaorahisisha utumaji wa taarifa za usajili wa watoto katika mfumo maalumu ya kuhifadhi kumbukumbu wa Mamlaka wa Rita.

Meneja wa Tigo Kanda ya Ziwa, Ally Maswanya, anasema walidhamini kwa kutoa nyingi za mkononi aina ya ‘smartphone’ kama sehemu ya mkakati wa kufanikisha lengo hilo la maendeleo ya kiuchumi nchini.

 
 
 

Habari Kubwa