Simiyu yahitaji vyumba 777 vya madarasa shule ya msingi 2018

14Nov 2017
Happy Severine
Nipashe
Simiyu yahitaji vyumba 777 vya madarasa shule ya msingi 2018

“BADO nafasi yetu katika elimu haipo vizuri sana kwani tuna changamoto nyingi zinazoikabili idara ya  elimu likiwepo suala  la uhaba mkubwa sana wa vyumba vya madarasa  na  hii ni kutokana  na ongezeko kubwa la wanafunzi-

Wanaojiunga na darasa la awali, la kwanza  na sekondari kuwa kubwa “ ndivyo anasimulia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka.

Mtaka anasema kutokana na uhaba huo ni vizuri kila mzazi aweke mkazo na msimamo juu ya elimu kwa watoto wao huku wakishirikiana na serikali kujenga miundombinu ya elimu bora kama ujenzi wa vyumba vya madarasa na madawati.

Anasema  serikali ya Mkoa wa Simiyu kwa sasa ina mzigo mzito ambao kamwe hauwezi kutatuliwa  na serikali pekee, isipokuwa kwa ushirikiano na wazazi.

Mtaka anabainisha kwamba hata kama serikali itajipanga vipi kujenga idadi yote ya vyumba vya madarasa vinavyotakiwa bila ushirikiano na wazazi, kamwe serikali peke yake haitaweza kuondoa tatizo hilo kwa asilimia zote.

Anasema wananchi wanatakiwa kutambua wajibu wao katika kuchangia ujenzi wa Vyumba vya madarasa ili kupunguza tatizo hilo katika shule za msingi na sekondari.

Anasisitiza kuwa ni vema wananchi wakahamasika kuchangia kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa kama wanavyochangia katika masuala mengine ili watoto wao wawe na mazingira mazuri ya kusomea.

“Kujenga vyumba vya madarasa siyo wajibu wa serikali pekee…ni wajibu wenu  wazazi, ni lazima wananchi wa Mkoa wa Simiyu mjenge vyumba vya madarasa kama mnavyojitoa katika mambo mengine… najua hamuwezi kushindwa kutoa angalau mfuko mmoja wa saruji kila kaya,” anasema.

UZAZI WA MPANGO
Aidha, Mkuu huo wa mkoa  amewataka wananchi kuzingatia suala la uzazi wa mpango kwa kuwa ongezeko kubwa la watoto ndio linalosababisha idadi kubwa ya wanafunzi ikilinganishwa na vyumba vya madarasa.

Anasema Rais (John Pombe Magufuli) amefuta gharama zote za elimu na kuifanya elimu kuwa bure, hivyo anawaomba wananchi kutotumia fursa hiyo kuongeza idadi kubwa ya watoto ambayo watashindwa kuimudu kwenye mahitaji ya msingi.

Mtaka anafafanua kuwa wengi wa wakinamama wamekuwa hawatumii njia za uzazi wa mpango wakiamini njia hizo kuwa na madhara juu yao na kwamba kutotumia kwao njia hizo kunasababisha ongezeko la wanafunzi kuwa kubwa sana.

Kwamba kunasababisha ongezeko la wanafunzi kuwa kubwa kiasi cha kushindwa kuhimili mahitaji ya vyumba vya madarasa na madawati.

Mtaka anasema kuwa mwaka jana Mkoa uliweza kufanikiwa kutengeneza madawati kwa asilimia kubwa zaidi na kuondoa tatizo la madawati lakini kutokana na idadi kubwa ya ongezeko la watoto kila mwaka imesababisha tatizo la vyumba vya madarasa na madawati kutoisha.

Hivyo amewaomba wananchi na madaktari kutoa elimu juu ya umuhimu wa kutumia uzazi wa mpango ili tatizo hilo liweze kumalizika.

Hata hivyo, anatoa tahadhari ili watu wasimuelewe vibaya juu ya kuzaa, akisema hajakataza ila la msingi wazae kwa mpango ili mahitaji muhimu na ya msingi yaweze kutekelezwa kwa watoto wao.

OFISA ELIMU

Naye Ofisa Elimu Mkoa wa Simiyu Julius Nestory anasema tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa ni kubwa na mpaka sasa kuna uhitaji wa vyumba 1,163 kwa ajili ya shule za msingi kwa mwaka ujao wa 2018.

Nestory anasema vyumba ambavyo viko tayari hadi sasa ni 386, hivyo kuna upungufu wa vyumba 777.

Anaeleza kuwa upungufu huo wa vyumba vya madarasa utawafanya wanafunzi wanaotarajiwa kuingia darasa la kwanza mwaka 2018 ambao ni 77,389 kukosa vyumba vya kusomea.

Ofisa huyo wa elimu anabainisha kwamba idadi hiyo ya wanafunzi 77, 389 wanaotarajiwa kuingia mwaka 2018 ni kubwa mno ikilinganishwa na wanafunzi 46,509 walioingia darasa la kwanza mwaka huu wa 2017.

Anasema kwa kuangalia takwimu hizo basi ni wajibu wa wananchi  kutambua kuwa wanalo jukumu la kuunga mkono jitihada za kukabiliana na upungufu huo wa vyumba vya madarasa ili kuleta maendeleo katika sekta ya elimu.

Kama ilivyo kwa Mkuu wa Mkoa, Nestory naye anataja sababu kubwa za uhaba wa vyumba vya madarasa uliosababishwa na ongezeko kubwa la wanafunzi ni ya wananchi kutokubali kutumia ipasavyo uzazi wa mpango hali inayosababisha ongezeko la watoto kila mwaka.

“Binafsi naweza nikasema wakazi wengi wa hapa hawajatilia mkazo matumizi sahihi ya uzazi wa mpango na ndio maana matatizo ya upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati hayawezi kumalizika kwa haraka mpaka pale watakapokubali na kupatiwa elimu ya kutosha juu ya uzazi wa mpango,” anasema na kuongeza.

“Sio kwamba elimu ya uzazi wa mpango haijatolewa, bali wakinamama wamekuwa waoga kutumia njia hizo wakihofia kuachika na waume zao kwani sifa ya mwanamke wa Mkoa wa Simiyu ni kuzaa idadi kubwa ya watoto.”

Aidha, kiongozi huyu wa elimu katika mkoa huo anataja sababu nyingine kuwa ni ile ya wanaume wengi Mkoani Simiyu kuwa na tabia ya kuoa wake zaidi ya wawili, hali inayofanya mtu mmoja kuwa na idadi kubwa ya watoto kila mwaka.

“Utakuta mtu mmoja ana wake watatu hadi wanne na kila mke ana watoto zaidi ya watano, hivyo kwa hesabu za kawaida mtu huyo atakuwa na watoto zaidi ya 10 ambao ni lazima watahitaji elimu …na kwa mazingira hayo vyumba vya madarasa kamwe haviwezi kutosha,” anasema.

SERA YA ELIMU BURE

Sambamba na sababu hizo, pia sera ya elimu bure imekuwa chachu ya ongezeko kubwa la wanafunzi mashuleni na hilo likijionyesha kwenye tofauti iliyopo kati ya idadi ya wanafunzi waliokuwa wakiandikishwa kabla ya sera hii kuanza na sasa hivi.

Nestory anabainisha kuwa jitihada za dhati zinatakiwa katika kuhakikisha wanafunzi wanajengewa uwezo wa kusoma katika mazingira mazuri.

HATUA ZA KUCHUKULIWA

Akizungumzia njia za kumaliza tatizo hilo Mkuu wa Mkoa huo  anasema serikali ya Mkoa imejipanga kufanya harambee kubwa ya kuchangisha fedha na vifaa vya ujenzi ili kutatua tatizo hilo.

Mtaka anasema harambee hiyo inatarajiwa kufanyika siku za karibuni ambapo itawahusisha wazaliwa wote wa Mkoa wa Simiyu, ambao wanaishi nje ya Mkoa huo ili kuhakikisha wanafikia lengo la kuwajengea wanafunzi hao mazingira mazuri.

MADIWANI

Kwa upande wao, baadhi ya madiwani wa Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu wameahidi kushirikiana na Mkuu wa Mkoa katika kuhamashisha uchangiaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika maeneo yao.

Wamesema watahamasisha kadri wawezavyo ili tatizo hilo liweze kupungua kama inavyofanya Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha ambayo imepiga hatua kubwa katika masuala ya uchangiaji wa shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

Mmoja wa madiwani, Robert Rweyo amekiri kuwepo kwa tatizo hilo kubwa na amewasihi wananchi kwa ujumla kuamka kifikra na mawazo katika kuandaa mazingira bora ya kujifunza na kujisomea kwa watoto wao.

WANANCHI

Mmoja wa wananchi mkoani humo Michael Paschal ameeleza kusikitishwa kwake na ugumu wa wananchi wa Mkoa wa Simiyu katika suala la kuchangia shughuli za maendeleo, ikilinganishwa na mikoa mingine.

Michael amewasihi na kuwataka wananchi wenzake waamke na kuanza kuhamasishana juu ya kufanya mabadiliko katika kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa ambavyo vitatumiwa na watoto wao kupata elimu.