Simulizi ‘msimamo’ na ‘uwazi’ zilivyo silaha kuishinda rushwa ngono

29Jul 2021
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Simulizi ‘msimamo’ na ‘uwazi’ zilivyo silaha kuishinda rushwa ngono
  • Uamuzi menejiment sheria tosha kumaIiza

LICHA ya sehemu muhimu kwa umma, vyumba vya habari vimo katika orodha ya kugubikwa na matukio ya ukatili kijinsia, wanawake.

Kinamama wanahabari wakiwa kazini. PICHA: MTANDAO.

Inafahamika, ukatili wa kijinsia unaangukia chochote kinachosababisha madhara ya mwili, kingono, kisaikolojia au mateso kwa wana jamii, kama kutishiwa maisha, kunyimwa uhuru hadharani au kwa kificho, kupigwa na madhara zaidi.

Karaha inaangukia mtu kushikwa maumbile, anataniwa, kuchekwa kulingana na maumbile katika hali ya kumdhalilisha.
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) chini ya mradi wa Wanawake katika Vyombo vya Habari, imeanzisha mpango mkakati kupunguza ukatili wa kijinsia katika vyombo hivyo.

KILICHOMO

Utafiti wa Nipashe umeibua uhalisia wa matukio katika vyumba vya habari. Mwanahabari kutoka Radio Wapo, Mwanahamisi (jina la pili tunalo), anaeleza sakata alipoanza kazi ya uanahabari, alivyokutana na madhila ya kijinsia kutoka kwa mhariri anayemsimamia.

Anasimulia magumu ya kupigiwa simu usiku wa manane na mhariri aliyekuwa na jukumu kumpangia kazi, (jina tunalo) kumshawishi kimapenzi., akiendeleza simulizi:

“Ananiuliza maswali ya karaha tena anazungumza zaidi ya saa tatu akilazimisha nizungumze yale masuala ya mapenzi.”

Mwanahamisi anaendelea: “Nilipoacha kupokea simu ndipo tatizo lilipoanza kuwa kubwa, kwa sababu nilikuwa nikifika ofisini ananitukana mbele ya kikao cha waandishi wa habari wenzangu kwa madai kuwa namdharau na simu zake sipokei.

“Alikuwa hasemi mbele za watu kuwa ananishinikiza kuongea naye mambo ya mapenzi. Alikuwa anadai sikupokea simu wakati alitaka kunipa majukumu ya kazi.”

Mwanahamisi anakumbushaa nukuu za kufokewa: “…mwandishi wa habari unazimaje simu yako, unaachaje kupokea simu? Unajua nilitaka nikuambie nini? Unajua nilitaka nikupangie kazi gani? Kama huwezi kupokea simu huna sifa ya kuwa mwandishi wa habari!”

Anasimulia namna kero ilivyoendelea kumuumiza na baada ya bosi wake kuacha kutoa kazi zake, ilimuingiza Mwanahamisi katika mazingira magumu.

 “Kwa sababu nilikuwa mdogo na nilihofia angenifukuza kazi kama ningemsemea kwa viongozi wakuu wa ofisi, niliendelea kuvumilia huku nikishikilia msimamo wangu kuwa sitaruhusu lengo lake litimie,”anasema.

Mwanahamisi anasema, ikabainika ni tabia yake kwa wanahabari wengi wanawake ofisini, huku kati yao ilifanikisha lengo, huku waliokataa walipitia ukatili mkubwa.

Anasema mwisho wa tabia hiyo ulifika baada ya wao kuanza kulalamika na ndipo walibaini wote walisumbuliwa.

“Bosi wetu, Mkurugenzi alisikia akatuita na kutuhoji mbele yake, kila mmoja alieleza alichofanyiwa na huo ndio ulikuwa mwisho wake wa kufanya kazi, kwani alifukuzwa,” anasimulia Mwanahamisi.

Mama huyo anasema, siyo wanawake wote wanaomudu kuvumilia kama yeye, maana wabishi wengi wameangukia kunyanyasika kimapenzi.

Flora (jina la pili tunalo) anayefanya kazi Radio EFM, naye ana simulizi kwamba kabla ya kuajiriwa aliko sasa, safari yake ilipitia chombo kimojwapo nako anakakutana na ukatili kijinsia kutoka kwa mhariri aliyemsimamia.

Anasimulia alipomkatalia uhusiano, alianza kukutana na visa vilivyomkarahisha ashindwe kufanyakazi zake kwa weledi.
Flora anasema, bosi huyo alijenga tabia ya kufika mapema na hata kama muda wa kuripoti haujapita, alichora mstari kwenye daftari ili mama huyo aonekane kachelewa.

Anasema, pia bosi huyo alienda mbali kuanza kumkosoa wakati akifanya kipindi ‘mubashara’ kinyume na taratibu za kitaaluma.

“Nikiwa studio natangaza anaingia kudai nimekosea na kuacha mlango wazi ili tu anitoe kwenye lengo na kunifanya nionekane sijui kazi yangu,” anasema Flora, akidokeza kwamba, hakuweza kumrip0ti, akihofia kufukuzwa. Mkataba wake wa kazi ulipoisha alienguliwa.

“Nilishindwa kuendelea na ajira yangu kwa sababu nilionekana ni mchelewaji, sijui kutangaza na sipo makini katika utekelezaji wa majukumu yangu, hivi vyote vilisababishwa na yule bosi wangu,” anasema Flora.

Beatrice Munisi, mwanahabari wa kujitegemea, ana simulizi alivyotumikia gazeti moja, akikumbuka ukatili wa bosi wake. Naye anangukia sumulizi za awali: “Nilikuwa sijaajiriwa, nafanya kazi na kulipwa kulingana na kazi. Kwa hiyo, kwa sababu alikuwa hazitoi nilikuwa nakosa malipo.”

Anaeleza bosi aliamuuongezea adhabu, ya kumpangia kufanya kazi za mahakamani pekee na licha ya yeye kutii, kazi zake hazikutumiwa, hadi pale alipojisikia.

“Niliteseka sana kisaikolojia, pia kiuchumi niliyumba kiasi kwamba nilitamani kuacha kazi nifanye shughuli nyingine. Lakini, niliendelea kujipa moyo kwa kuendelea kuvumilia zaidi ya mwaka mmoja,” anaseme Beatrice.

Baada ya mwaka mmoja, anasema bosi huyo alihamishwa kikazi kwenda kituo cha mbali na ndio ukawa mwanzo wa uhuru wake kufanya kazi kwa ufanisi kiuchumi na uhuru binafsi.

Katika kipindi chote cha mpito anataja ‘alibebwa’ na biashara ndogo aizofanya.

WAHARIRI WANASEMAJE

Mhariri, Isaac Kijoti, anakiri kuwapo mambo ya aina hiyo, akiwa na ushuhuda wa malalamiko na siyo taarifa rasmi.

“Kama yupo anayefika hatua ya kusema au kuripoti ngazi za utawala basi ujue huyo amefikia hatua ya kuacha kazi. Vinginevyo vitendo kama hivi haviripotiwi moja kwa moja,” anasema Kijoti.

Anasema kukosekana uthubutu wa kuripoti mikasa uanchangiwa na kuhofia ajira, kwa maana wanaweza kufukuzwa kazi.

Pia, anasema kinamama wanashindwa kuripoti kwa sababu wahariri wana mamlaka makubwa kwenye chombo cha habari.

“Utaona kabisa aliyemshtaki ataendelea vipi kufanya naye kazi, ndio maana wanaamua kunyamaza na kuvumilia,” anasema Kijoti.

Mhariri wa Habari wa gazeti la Majira, Stellah Arron, anakiri ukatili kijinsia kwenye vyumba vya habari hayaripotiwi, kwa sababu wanaofanyiwa wanahofia kupoteza ajira zao.

Pia anadokeza, pia kuwapo dhana wanawake kuripoti matukio hayo ni kujidhalilisha, hivyo wanaamua kubaki wakimya.

“Mfano ukiripoti mhariri fulani amekutaka kimapenzi, akachukuliwa hatua, ukienda ofisi nyingine kufanya kazi, yule bosi atamuambia bosi mwingine kuwa una tabia mbaya na huna uwezo wa kufanya kazi.

“Sasa inategemea mapokezi ya huyo bosi mpya, lakini hasara inakuwa kwa mwandishi anaendelea kupitia ukatili,” anasema Stellah.

Anasema katika kipindi chake cha kuwa mhariri anayewapa majukumu wanawake, amekutana na matukio hayo na amewasihi kuwapuuza wanaowafuata, waendelee kutekeleza majukumu yao.

Anashauri elimu utolewe kwenye vyombo vya habari kudhibiti matukio hayo.

SERA/ MUONGOZO MCT

Sera ya Jinsia Kwenye Vyombo vya Habari ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), mwaka 2019, inataja baadhi ya unyanyasaji kazini uliokithiri kazini ni wa ngono, kinamama wanaishia kutishiwa, kufedheheshwa na kutukanwa.

Ni sera inayoanika namna ya kuukabili, ikiwamo kulifikisha suala kwa msimamizi wao au Idara Rasilimali Watu.

TAMWA JE?

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Rose Reuben, anasema wanatekeleza mradi huo wakifahamu kuwapo tafiti zinazoonyesha zipo rushwa ya ngono katika vyumba vya habari.

“Wakati huo huo, wanahabari wameonekana kuwa kimya kuhusu matukio hayo, aidha kwa kuogopa kupoteza ajira zao au pengine wakichelea kuaibika,” Reuben anasema.

Anasema ni hali inayoshusha utu, kudhalilisha waathirika, kuwapa msongo wa mawazo na kutojiamini kazini, huku matukio mengi hayaripotiwi.

Rose anakiri TAMWA inatambua Sheria ya Rushwa ya Ngono inayosimamiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU).

“Tunataka wanahabari wapaze sauti zao, tuvunje ukimya, wayazungumze yanayowasibu na kuondoa kabisa ukatili wa kijinsia aina hii,” anasema Rose.

Anarejea watafiti kimataifa, Barton A na Storm, (2014) walibaini asilimia 48 ya wanahabari wanawake waliohojiwa walikiri kukumbana na  rushwa ya ngono ofisini na asilimia 83 kati ya hao, hawakuyaripoti matukio hayo.

Anaeleza haja ya waathirika kujengewa uwezo wa kukusanya vidhibiti vya uhakika vinavyosaidia vyombo kusimamia udhibiti ea mikasa hiyo, kupitia ushirikiano na serikali, taasisi za habari, pia jinsia.

TAKUKURU

TAKUKURU katika kudhibiti rushwa ya ngono kazini, ilisaidia kutafiti kwa lengo kuwezesha upatikanaji taarifa za kisayansi kusaidia kukabili vitendo hivyo katika taasisi za elimu ya juu nchini.

Kurejea Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007, TAKUKURU ina wajibu wa kuzuia rushwa katika taasisi za umma na binafsi kwa kufanya chambuzi za mifumo katika taasisi ili kubaini mianya ya rushwa na kisha kutoa ushauri wa namna bora ya udhibiti.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali, John Mbungo, katika uzinduzi wa ripoti hiyo, Juni mwaka jana, alisema vita ya rushwa nchini, bado ya ngono ina malalamiko.

Anatoa sababu ya kuwapo huko kunachangiwa na sababu nyingi, ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka; mikakati dhaifu ya kutekeleza sheria za rushwa ya ngono; uelewa duni; kutotambua kina na athari za tatizo rushwa ngono; na jamii kuionea aibu.

Hapo inatajwa zao lake ni waathiriwa wa rushwa ngono wanaendelea kuumia kimya kimya na wanaotenda wanaendelea na vitendo hivyo, bila kuchukuliwa hatua stahiki kisheria.