Simulizi ndoa kuvunjika na kulipuka umaskini kifamilia

22May 2020
Na Mwandishi Wetu
Pemba
Nipashe
Simulizi ndoa kuvunjika na kulipuka umaskini kifamilia
  • Ya simanzi mama hadi mtoto
  • Faraja uchokonozi wa Tamwa

WAKATI serikali, wadau na wanaharakati wako katika vita vya haki za watoto kuondosha unyanyasaji, bado kuna mikasa ya aina hiyo inaendelea.

Hafla ya mradi unaohamasisha watoto kusoma, kisiwani Pemba. PICHA: MTANDAO

Mikataba kimataifa, kikanda na kitaifa inaelekeza wajibu wa kila mmoja kuwalinda watoto dhidi ya maovu na haja ya kuwapa huduma stahiki kama elimu, chakula, lishe bora na kuimarishwa kiafya.

Wajibu wa kumlinda mtoto kupitia serikalini na mashirika yasiyo ya serikali, yanatunga sera, sheria na miongozo ya utekelezaji na wawajibikaji wakuu ni wazazi na hasa wanandoa.

Uchunguzi wa Nipashe kisiwani hapa, umebaini bado kuna tatizo kubwa la unyanyasaji wa mtoto.

VIONGOZI SERIKALI

Mratibu wa Wanawake na Watoto wa Shehia ya Mjiniole, Pemba anasema wazazi wanapotengana, watoto wanakumbwa na mengi, ikiwamo kubakwa, mimba na ndoa za umri mdogo zinazowakosesha maendeleo.

Anasimulia mwaka jana alipokea kesi ya mama wa watoto wawili waliotelekezwa na mume tangu ujauzito wa mtoto wa pili mpaka umri wa miaka mitatu sasa.

“Wote ni watoto wa kiume, wa kwanza amefikia miaka tisa hajapelekwa skuli, linaloumiza zaidi nimegundua ameshaanza kufanyiwa ulawiti,” anasema.

Pia, ana simulizi ya mama wa watoto tisa, kati yao watano hawasomi; huku kesi nyingime ya namna hiyo, familia yenye watoto wanne wote hawajaenda shule.

“Kesi hizi zipo nyingi sana, lakini hawaripoti, isipokuwa mwaka jana nilipokea kesi tano,” anaeleza.

Ofisa Wanawake na Watoto Wilaya ya Wete, Siti Suleiman Juma, ana ufafanuzi: “Asilimia kubwa ya watoto wanaojishughulisha na ajira ni wanaoishi na mzazi mmoja, hivyo huathirika kisaikolojia kutokana na kukumbana na kadhia mbalimbali katika jamii.

“Inapotokezea baba ‘kamtalaki’ mama, basi awashughulikie watoto, unapowadharau watoto na wao watakudharau, kwani itakuwa umechangia kudumaza maendeleo yao, mama pekee hawezi kumudu majukumu yote.”

Siti ana mtazamo kwamba, changamoto za kinamama katika kesi hizo, wengi hasa wasiokuwa kazini hawajui mahali pa kupashughulikia.

Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Wete, Haroub Suleiman Hemed, ana lake: “Watoto wanaoishi na mzazi mmoja huduma zinakuwa ni tofauti na yule anayeishi na wazazi wawili, hukosa uwezo wa kujieleza kwa umakini, hukosa fursa, pia hukosa ukaribu wa wazee.”

Anawashauri wanandoa kuwa wavumilivu katika misuguano na inapobidi, watumie taratibu rasmi kama za kidini kusuluhishana, ili kudumisha malezi yenye maadili.

“Kuna mama wa Kipangani Wete ameachwa na watoto kwa zaidi ya miaka saba, baba wa watoto amehamia Tanga, hivyo mtoto wake alitaka kujitundika baada ya kukerana na mtoto mwenzake (jirani) kutokana na kumkebehi kwa maisha wanayoishi,” anasimulia.

Ofisa Ustawi wa Jamii huyo ana takwimu za kati ya Januari na Novemba mwaka jana, Wete ilipokea kesi 85 za kudai matunzo ya watoto, baada ya wazazi kuachana au kutelekezana na kati yake 69 zimepatiwa ufumbuzi, saba zilikuwa zinaendelea kushughulikiwa.

Pia, mwaka 2018 ofisi hiyo ilipokea mashauri 34 ya mivutano ya kimalezi na kesi 71 za kutelekezwa.

Naibu Mrajis wa Mahakama Kuu Pemba, Abdul-razzak Abdul-kadir Ali, anakiri kupokea kesi za baba wanaotelekeza watoto katika Mahakama ya Kadhi.

Sheikh Mohamed Ali Hamad, Kadhi wa Mahakama ya Wilaya Wete, anasema ni adimu wanawake walioachwa kufika mahakamani, badala yake hufika waliopo kwenye ndoa, amama wakidai huduma au kulalamikia kutelekezwa.

Anatoa mfano, mwaka juzi, zilipokewa kesi tisa za watoto kukosa matunzo na mwaka jana 15, kati yake 11 zilipatiwa maamuzi.

WAATHIRIKA WAFUNGUKA

Nafhat Salim Yahya, mkazi wa Limbani, Wete Kaskazini, anasisitiza kutengana wazazi kunaathiri maendeleo ya watoto kwa mahitaji muhimu, kama afya na elimu kwa ujumla.

“Mtoto aliyesoma anaweza kuajiriwa au kujiajiri mwenyewe kutokana na fani anayosomea na akili yake inafikiria maendeleo zaidi, lakini ambaye hakusoma akili yake inadumaa,” anafafanua Nafhat.

Hamad Ali Abdallah, mkazi wa Shehia ya Shengejuu, Wete, ana maelezo kwamba wazazi wanapoachana, maisha duni hasa kwa watoto huchukua nafasi.

Mkazi wa Shehia ya Mjiniole (29), aliyeachika akiwa na mtoto na ujauzito, anasimulia kukosa huduma ya baba wa watoto kwa zaidi ya miaka minne, hali iliyomkwamisha mtoto kuhudhuria masomo.

“Baba yao ni mwajiriwa wa serikali na nilimshtaki mahakamani ili angalau anipe pesa nimpeleke skuli, lakini hakutekeleza amri ya mahakama na kila akiitwa hafiki,” anaeleza.

Mama anaeleza kwa masikitiko ana mume mwingine sasa, ila shida kuu katika maisha mapya ni umaskini wa mume kumhudumia.

Mama wa miaka 46 mkazi wa Shehia hiyo, ana simulizi: “Siku zote walipokuwa wakirudi skuli, zaidi ya maji ya kunywa hawakuti kitu kingine humu ndani, hivyo walichoka hali hii na wakaniambia liwalo na liwe kuanzia leo hatuendi shule.

“Hatujui tunachokisoma, ni njaa tu kutwa na tukirudi hamna chakula. Bora tukusaidie kulima tupate angalau cha kutia tumboni.”

Mama kijana wa miaka 20 mkazi wa Wete, anaelezea maswahibu yaliyomfika kifamilia, baada ya wazazi kuachana akiwa na miaka 13, wao watoto walisambaratika hadi leo, huku wengine wakikabiliwa na matendo mbaya.

Anasimulia wanavyokabili maisha, ni kuranda vichakani na Pwani kuokota vinavyolika, hali iliyozaa dosari mdogo wake kubakwa.

“Kuna tatizo, sheria inazungumzia idadi ya pesa kuwa isizidi robo ya mshahara, hivyo kutokana na mshahara ulivyo mdogo hautoshelezi hasa kwa mama mwenye watoto wasiopungua wane,’’ anafafanua.

TAMWA & WADAU

Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) Pemba, Fat-hiya Mussa Said, anasema wamekuwa wakiwatetea kinamama na watoto, kuhakikisha wanaishi salama.

“Sisi Tamwa tunashirikiana na waandishi wa habari kuibua vitendo vya udhalilishaji, ikiwamo la kukoseshwa huduma, ili kinamama wahamasike kwenda kwenye vyombo vya sheria kudai haki zao,’’ anaeleza.

Anasema, baada ya kesi hiyo ya watoto waliotelekezwa kuibuliwa na wanahabari, walijitokeza wafadhili kuwapatia chakula cha kujikimu, sambamba na kuwatengenezea makazi ya muda.

Mratibu wa Jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE), Tatu Abdalla Mselem, ana ufafanuzi: “Mtoto ndiye anayekumbwa na athari za talaka kwani anakosa huduma zote alizokuwa azipate akiwa na wazazi wawili, lakini ile fimbo inaendelea kumpiga mtoto kwa kukosa huduma muhimu…ukizingatia mama atakayeachiwa ulezi hana huduma.”

Mkataba wa Kimataifa wa Kulinda Haki za Mtoto wa Novemba 30 mwaka 1989, uliotiwa saini na nchi 197 duniani ikiwamo Tanzania, unaeleza haki za watoto, kijamii, kisiasa na kiuchumi, kupinga udhalilishaji na utumikishwaji watoto.

Aidha, kuna nyenzo kama hiyo, Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto, uliopitishwa na Umoja wa Afrika (AU) mwaka 1990.

Habari Kubwa